GST YAWASILISHA MATOKEO YA UTAFITI WA AWALI WA MADINI MKOANI SINGIDA KATIKA WILAYA YA MKALAMA

Na.Samwel Mtuwa - Singida.

Leo Machi 8,2021 Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) imewasilisha matokeo ya utafiti wa awali wa upatikanaji wa Madini mbalimbali mkoani Singida katika wilaya ya Mkalama.

Akizungumza kwa niaba ya Mtendaji Mkuu wa GST Mhandisi Migodi Mkuu John Shija alisema kuwa matokeo haya ya utafiti wa awali yameonesha uwepo wa madini mbalimbali Kama vile Madini ya Dhahabu, Chokaa , Shaba na Madini ya Jasi.

Kwa upande wa Madini ya Chokaa yaliyopo katika maeneo ya Miganga matokeo ya utafiti yameonesha ubora wa Chokaa kiwango cha CaCO3 kwa asilimia 98.66 ambapo kwa mujibu  wa kitaalamu na tafiti mbalimbali zilizofanyika, kiwango hiki ni cha juu cha ubora kufikia ubora wa chokaa safi.

Katika maeneo ya Mpambala utafiti  umebaini  uwepo wa madini ya dhahabu yaliyopo katika kiwango Cha 2.089 g/ton ambapo  kiwango hiki inabidi kifanyiwe utafiti zaidi kujiridhisha na ubora wake ili kubaini bila shaka kama miamba hiyo ya dhahabu inafaa kwaajili ya wachimbaji wadogo.

Katika Madini ya Jasi yanayopatikana katika eneo la Dominiki , Utafiti umeonesha kuwa madini haya yapo katika ubora wa daraja la pili (Grade Two) ambapo madini kwa kiwango hicho cha ubora yanaweza kutumika kwa matumizi ya mbolea.

Kwa upande wa Madini ya Shaba matokeo yameonesha Madini haya yapo katika ubora wa asilimia 54 ambayo kitaalamu yanaonekana yapo  katika kiwango Cha juu.

Kwa mujibu wa Mhandisi Shija alisema kuwa, Sheria ya Madini RE 2018 inataka  wachimbaji kuongezea thamani madini haya kabla hayajasafirishwa kwenda nje ya nchi.

 Hivyo, wachimbaji wadogo ni muhimu kwao kuyaongezea thamani madini hayo ya shaba kwa kuweka viwanda vya kuongeza thamani na kutoa ajira kwa watanzania hasa walio vijijini ambako ajira ni za shida badala ya kuyauza yakiwa ghafi na kuwakosesha watanzania fursa ya ajira.  

Utafiti huu wa awali umefanyika katika maeneo 11 ya wilaya ya Mkalama.

Zifuatazo ni picha mbalimbali za tukio husika:





 


No comments: