WIZARA YA MAJI YAAHIDI KUMALIZA KERO YA MAJI KWA WANANCHI
Na Woinde Shizza, Michuzi Tv-ARUSHA
Wizara ya maji haitakuwa kero kwa wananchi kwani watafanya kazi usiku na mchana kuhakikisha wanatatua changamoto zote za maji.
Hayo yameelezwa na Waziri wa maji Jumaa Aweso wakati akizungumza na watumishi wa sekta ya maji wa mkoa wa Arusha ambapo alisema kuwa kazi ya kushughulikia matatizo ya maji haijawashinda wanaweza kutekeleza na fahari yao itakuwa ni kuona wananchi wanapata maji.
Alieleza kuwa maendeleo ya sekta ya maji yanaanza na watumishi hivyo wakashirikiane katika kutatua matatizo ya maji huku wakitekeleza majukumu yao kwa ukamilifu ili kutimiza hadhma ya upatikanaj wa maji safi na salama kwa wananchi.
Alisema dhamira ya serikali ni kupatikana kwa huduma muhimu ya maji safi salama ya yakutosheleza wananchi ambapo serikali imekusudia kutenga bajeti ya utekelezaji wa miradi ya maji ikiwamo mradi mkubwa wa maji unaoendelea kutekelezwa mkoani Arusha.
“Kazi haijatushinda tutafanya kazi usiku na mchana kuhakikisha maji yanapatikana maeneo yote yaliyo katika Mpango na katika hili niwaambie tu kuwa mhandisi yoyote ambaye anayefikiria kuwa yupo kwaajili ya kukwamisha wizara ya maji ajue kuwa anajikwamisha mwenyewe,”Alisema Aweso.
Alisema uhuni unaofanywa na baadhi ya watendaji ili kuhujumu miradi hivyo wakahakikishe wanafanya kazi inavyostahili ili kutekeleza adhima ya Rais lakini pia ilani ya chama cha mapinduzi (CCM) kwa kuhakikisha wananchi wote wamapata huduma ya maji.
Kwa upande wake mkuu wa Mkoa wa Arusha Iddi Kimanta aliwataka watumishi wa secta ya maji kutekeleza wajibu wao kazini na sio kusubiri kusukumwa kwani maji ni moja ya sekta ambayo inamgusa mtu moja kwa moja.
Aliwasihi kuisaidia serikali kutekeleza majukumu yake kwa weledi wa hali ya juu pamoja na kuwashirikisha viongozi wa serikali changamoto zinazowakabili.
Naye Mkurugenzi wa mamlaka ya maji na usafi wa mazingira (AUWSA) Mhandisi Justin Rujomba aliahidi kukabidhi mradi wa maji wa Moita ifikapo April 9 mwaka huu ambapo watatekeleza kwa wakati na kwa ubora.
No comments: