WANAOKWAMISHA KUAZISHWA KWA VIWANDA VINGI VYA KUCHAKATA MIWA NCHINI WAONYWA


Na John Nditi, Morogoro

SERIKALI imebaini uwepo wa mkakati wa kukwamisha kuanza kwa ujenzi wa viwanda vingi vya kuchakata miwa ya wakulima ili nchi isijitosheleze kwa uzalishaji wa sukari nchini .

Hivyo imewaonya watu wenye nia hiyo pamoja na viwanda vya sukari vinavyoshiriki kukwamisha kuanzishwa kwa viwanda vingi vya kuchakata miwa kuacha mara moja njama hizo vinginevyo wanakuwa wanakalia kaa la moto.

Waziri wa Kilimo, Profesa Adolf Mkenda, alitoa onyo hilo alipotembelea Kiwanda cha Mkulazi II na kuzungumza na wakulima wa miwa kutoka vijiji vya Msowero, Malangali, Mvumi,Wami Dakwa na Mbigiri vilivyopo katika wilaya ya Kilosa.

Alisema kuwa kuna taarifa za uhakika kuwa baadhi ya watu wasioitakia mema nchi wanakwamisha jitihada za kuanzishwa kwa kiwanda cha kuzalisha sukari cha Mkulazi II hatua ambayo inayoendelea kuwaumiza wakulima wa miwa kwa mazao yao kutupwa kwa kukosa wanunuzi wa uhakika

“Nawahakikishia ninazo taarifa kwamba sasa kiwanda kitakamilika na kuanza kazi haraka, kwa hiyo wakulima msiwe na wasiwasi na soko la miwa” Profesa Mkenda aliwahakikishia wakulima wa miwa bonde la Mbigiri wilayani Kilosa.

Waziri alisema kuwa, anayezuia kiwanda hiki cha Mkulazi II kisianze kazi serikali itachukua hatua kali na Serikali itapambana na changamoto zote zilizopo kuhakikisha kuwa kiwanda kinafanya kazi.

“ Naomba niwashukuru wakulima kwa uvumilivu mpaka hapo tulipofika na changamoto nyingi,lakini nawahakikishia ninazo taarifa sasa kiwanda hapa kitakamilika na kitaanza kufanya kazi na serikali haitawaangusha “alisema Profesa Mkenda.

Waziri Mkenda , alisema ; “ sisi wote tutasimama nao zile changamoto ambazo zingine hawajazisema tutapambana nazo,anayezuia kiwanda hiki kisifanye kazi ‘tutampasua’ tunajua nini kinaendelea tunapambana na mambo mengi sana hiki kiwanda kitaanza kazi” alisema Profesa Mkenda.

Waziri Mkenda , alisema kwa muda wa miaka mitatu sasa tangu mwaka 2018 wakulima wa miwa wa Bonde la Mbigiri wilaya ya Kilosa wamekuwa wakihangaika kuuza miwa yao kutokana na kiwanda cha Mkulazi kushindwa kukamilika huku wakulima wakiendelea kudaiwa mikopo ya fedha walizokopeshwa na Benki ya Azania

“ Anayesimama kuzuia hiki kiwanda kisifanye kazi sSerikali itamshangaza kwa kuwa inapambana na mambo mengi makubwa na imekuwa ikishinda”alisema Profesa Mkenda.

Waziri huyo alivitaka viwanda vya sukari vya Kilombero na Mtibwa vianze kujitathimini kutokana na kushindwa kununua miwa yote ya wakulima wa nje kutokana uwezo mdogo wa uchakataji wa miwa huku serikali ikiwapa vibali vya kuagiza sukari kutoka nje ili kuziba pengo linalojitokeza.

“ Tuna maslahi kama serikali kuhakikisha kwamba tunajitosheleza kwa sukari , maslahi yetu katika soko la sukari yanarandana na maslahi mapana ya mkulima wa miwa kupata soko na serikali kujitegemea kwenye sukari” alisititiza Profesa Mkenda.

Naye Mbunge wa Jimbo la Mikumi ,Dennis Londo,akizungumza kwa niaba ya Mbunge wa Jimbo la Kilosa,Profesa Palamagamba Kabudi ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,alisema licha ya wakulima wake kuhamasika kulima miwa lakini hawana uhakika wa soko la miwa kwa kipindi cha miaka mitatu.

Mbunge huyo ,alisema kukosekana kwa uhakika huo kunatokana na kucheleweshwaji wa ukamilishwaji wa kiwanda cha Sukari Mkulazi II na matokeo yake miwa yao kwenda kuuzwa kiwanda cha Mtibwa kwa bei ya chini ya Sh : 60,000 hadi Sh : 65,000 kwa tani moja ukilinganishwa na gharama za uzalishaji.

Mkulima wa miwa wa Mbigiri Salome Mbilinyi ,alisema walihamasishwa kulima miwa katika mashamba yao walikuwa wakilima mahindi lakini miwa hiyo imeshindwa kufunwa miaka mitatu bila kuuzwa.

Mkulima mwingine Saidi Mazunde wa Mbigiri alisema licha ya jitihada uongozi wa Mkulazi kuwatafutia soko katika kiwanda cha Mtibwa baada ya kuuza miwa hiyo wamekuwa wakikatwa benki ya Azania riba kubwa ya asilimia 50 badala ya asilimia 25 ya makubaliano na nyingine ya asilimia sita (6) ya adhabu ya kuchelewesha mkopo.

Mazunde , alisema kuwa tatizo la kudaiwa kukatwa riba ya asilimia sita zaidi limetokana na mkataba kati ya Kampuni ya Mkulazi , AMCOS na wakulima kuwa kitakapoanza kiwanda wakulima wote watauza miwa yao huko , lakini sasa ni miaka mitatu kiwanda hakijaanza na mkulima anaonekana kupewa adhabu.

“ Hii asilimia 6 ya riba ya adhabu tunaomba ibebwe na Mkulazi kwa kuwa ndio waliotushawishi tulime kwa kuwa wataanzisha kiwanda hapa Mbigiri” alisema Mazunde.

Hata hivyo ,alisema kutokana kukosekana kwa soko hivi sasa baadhi ya wakulima wa miwa wameanza kung’oa miwa na kupanda mazao mengine ya kujikimu na kumuomba Waziri huyo kusimamia uanzishwaji wa kiwanda hicho haraka.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ,Kilimo,Mifugo na Maji,Dk Christine Ishengoma, aliwasihi wakulima wasikate tamaa kuacha kulima miwa na wasing’oe miwa yao au kuanzisha kilimo cha mazao mengine kutokana na kiwanda kuchelewa kuanza.

Dk Ishengoma aliwataka wawe wavumilivu kwa kuwa Serikali ya awamu ya tano imepokea kilio chao kwa Waziri wa Kilimo kuja kuwasilikiza . “Wakulima wangu msife moyo mkachukua hatua za kuchimbua miwa,Tunataka kilimo kimkomboe mkulima hivyo kwero zenu zitapatiwa ufumbuzi haraka.” Dk Ishengoma.

 Waziri wa Kilimo, Profesa Adolf  Mkenda, akizungumza na wakulima wa miwa  kutoka vijiji vya Msowero, Malangali, Mvumi,Wami  Dakwa na Mbigiri  vilivyopo katika wilaya ya Kilosa  mkoani Morogoro alipotembelea  Kiwanda  cha Mkulazi II kilichopo wilayani humo.

Baadhi ya viongozi wa Serikali na Taasisi za Umma pamoja na wadau wa tasnia ya Sukari wakimsililiza Waziri wa Kilimo, Profesa Adolf  Mkenda, ( hayupo pichani) wakati akizungumza na wakulima wa miwa  kutoka vijiji vya Msowero, Malangali, Mvumi,Wami  Dakwa na Mbigiri  vilivyopo katika wilaya ya Kilosa  mkoani Morogoro alipotembelea  Kiwanda  cha Mkulazi II kilichopo wilayani humo.




Mmmoja wa wakulima wa miwa wa bonde la Mbigiri wilayani Kilosa , mkoa wa Morogoro akitoa kero zake na za wakulima wenzake kuhusiana changamoto mbalimbali katika kilimo cha miwa .( Picha na John Nditi).


 

No comments: