WANAFUNZI WINO SEKONDARI WAANZA KUKAA BWENI

 Na Muhidin Amri, Madaba
WANAFUNZI wa shule ya sekondari Wino Halmashauri ya Madaba mkoani Ruvuma wameondokana na hadha na usumbufu wa kuishi mbali na shule na wengine kupanga vyumba uraiani kufuatia wakala wa misitu TFS kupitia shamba la Wino kukamilisha ujenzi wa bweni moja la wavulana.

Wanafunzi wa shule hiyo hasa wavulana walilazimika kupanga vyumba  kwenye nyumba za wenyeji kutokana na ukosefu wa mabweni hali iliyochangia kushuka kwa taaluma,matukio ya wizi na kukithiri kwa utoro  kwa wanafunzi.

Mkuu wa shule ya Sekondari Wino Benaya Mkumba alisema  kuwa ujenzi wa bweni hilo ulianza tangu mwaka 2017  kwa wazazi na jamii kusimamisha boma, hata hivyo walishindwa kukamilisha kwa kukosa fedha kwa ajili ya kununua vifaa vya viwandani kama bati,nondo na saruji.

Hata hivyo Mkumba alisema, baada ya muda mrefu tangu kuzimama kwa ujenzi huo wakala wa misitu TFS kupitia shamba la miti Wino umesikia kilio chao na kutoa bati 100 zilizosaidia kuezeka bweni hilo pamoja na ofisi moja ya walimu,saruji kwa ajili ya kupiga lipu ndani na nje pamoja na  sakafuni.

Alisema mbali na vifaa hivyo  TFS imetoa rangi na kutengeneza madirisha  yote ya bweni  ambalo limeanza kutumika kulala wanafunzi wa  madarasa ya mitihani yaani wanafunzi wa kidato cha  pili na nne ili wawe jirani na shule na kupata muda mwingi wa kusoma.

Mkumba alisema kukamilika kwa bweni hilo kumesaidia sana  kudhibiti nidhamu ya wanafunzi,kuongezeka kwa taaluma na kupunguza gharama ya  maisha kwa wanafunzi  kupanga vyumba  kwa wenyeji wa maeneo hayo.

Wakiongea huku wakibubujikwa na machozi ya furaha  baadhi ya wanafunzi Faluja Halfan wa kidato cha nne na Sixtus Nuru wa kidato cha pili wameishukuru TFS kukamilisha ujenzi wa bweni hilo kwani umewaondolea hadha ya kuishi mbali na shule pia kumaliza  changamoto ya kupanga vyumba jambo lililochangia sana kushuka kwa taaluma kwa wanafunzi.

Faluja Halfan alisema,  hatua hiyo imesaidia wanafunzi kupata nafasi nzuri ya kuhudhuria masomo kwa wakati tofauti  na  siku za nyuma ambapo wakati mwingine walichelewa vipindi  kutokana na umbali wa eneo walilokuwa wanaishi hadi kufika shuleni.

Sixtus Nuru mbali na kuishukuru TFS  kutokana na mchango  huo alisema kukamilika kwa bweni hilo kutapunguza  utoro na matukio ya wizi yaliyokuwa yanafanywa na baadhi ya wanafunzi watukutu  wasiopenda kusoma na wenye tabia mbaya.

Alisema wakati mwingine baadhi ya wanafunzi walilazimika kuacha shule kutokana na mazingira mabaya  hasa sehemu za malazi na hivyo  kurudi nyumbani kutokana na  sehemu ya malazi kutokuwa rafiki,lakini kwa sasa hakuna mwanafunzi atakaye acha shule kwani mazingira ni mazuri na rafiki kwa ajili ya kujisomea.

Kwa upande wake meneja wa shamba la Wino Lucas Manyonyi alisema kwa kipindi cha miaka mitano  imeweza kutoa msaada wa vifaa  vya ujenzi vyenye thamani ya shilingi milioni 15 kwa baadhi ya shule za msingi na sekondari,ofisi za serikali za kijiji, nyumba za ibada na mkakati wao ni kuendelea kufanya hivyo kadri bajeti itakavyoruhusu.

Alisema, kwa kutambua na kuthamini michango ya jamii  katika kulinda na kutunza mazingira,wakala kupitia shamba la miti Wino umeendelea kushirikiana na jamii kwa kusaidia mambo mbalimbali ikiwemo kutoa miche ya miti,mbegu za miti pamoja na viriba kwa shule za msingi na sekondari na vikundi vya wakulima wa miti.
MWISHO.
Bweni la wavulana katika Shule ya Sekondari Wino Halmashauri ya wilaya ya Madaba mkoani Ruvuma ambalo ujenzi wake uliibuliwa na wananchi wa kata ya Wino  kwa lengo la kuwaondolea usumbufu wanafunzi wa shule hiyo kupanga vyumba mitaani ambalo  wakala wa huduma za misitu TFS kupitia shamba laWino limemalizia kujenga  kwa kutoa bati,rangi na kutengeneza madirisha ambapo sasa wanafunzi 58 wanalala katika Bweni hilo.
Picha na Muhidin Amri.

No comments: