NAMUNGO FC YAONESHA MATUMAINI YA KUFUZU MAKUNDI KOMBE LA SHIRIKISHO AFRIKA
Na Bakari Madjeshi, Michuzi TV
KLABU ya Soka ya Namungo imeonesha matumaini ya kufuzu makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya ushindi mnono wa bao 6-2 dhidi ya Clube Desportivo 1ยบ de Agosto ya Angola katika mchezo wa 32 bora (Play Off) ya Michuano hiyo uliopigwa kwenye dimba la Azam Complex, Chamazi jijini Dar es Salaam.
Mchezo huo wa mkondo wa kwanza umepigwa kwenye dimba hilo huku CD de Agosto wakiwa wenyeji kama uamuzi wa Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF) kuamua michezo yote miwil kuchezwa Tanzania kutokana na kadhia ya maambukizi ya virusi vya COVID-19.
CD de Agosto, wageni kutoka Angola lakini wakiwa wenyeji wa mchezo huo walianza kufunga bao la kwanza katika dakika ya 12 na Brian Moya aliyefunga kwa mkwaju wa Penalti bao la pili dakika ya 51.
Wakiwa na faida ya kucheza nyumbani, Mabao ya Namungo FC yalifungwa na Hashim Manyanya dakika ya 32 ya mchezo, mabao mawili yakifungwa na Sixtus Sabilo dakika ya 38 na 59, Larient Lusajo dakika ya 55 na Eric Kwizera dakika ya 66, Stephen Sey dakika ya 71 ya mchezo.
Kocha Mkuu wa Namungo FC, Hemed Suleiman Morocco amesema siri ya mafanikio ya ushindi huo ni udhaifu walioonyesha wapinzani wao, Agosto katika mchezo huo.
“Walikuwa hawana spidi, kwa hiyo wachezaji wangu walitumia udhaifu wao kuwaadhibu mabao 6, walikuwa hawana haraka ila ni wazuri. Tutaenda kufanya marekebisho kidogo kwa makosa tulioonyesha katika mchezo huu kabla ya mchezo wa marudiano”, amesema Hemed Suleiman.
Kwa matokeo hayo Tanzania tunaweza kushuhudia idadi kubwa ya michezo ya Michuano ya Kombe la Shirikisho endapo timu hiyo itafuzu makundi ya Michuano hiyo mikubwa ngazi ya Pili upande wa Klabu, mchezo wa pili utachezwa Februari 25, 2021 katika Uwanja huo huo wa Azam Complex, Chamazi jijini Dar es Salaam.
No comments: