KITUO CHA KUPOZEA UMEME MLANDIZI KUONGEZA UWEZO WA UPATIKANAJI UMEME MVA 120
Na Mwamvua Mwinyi,Pwani
KITUO Cha kupozea umeme kilichopo Mlandizi ,mkoani Pwani kinatarajia kuongeza uwezo wa upatikanaji wa Umeme MVA 120 ,ifikapo mwezi march mwaka huu na baadae itaongezeka na kufikia MVA 240 kwa mwaka 2022.
Lengo kuu la kuongeza kasi katika upatikanaji wa nishati ya umeme imetokana na mahitaji makubwa ya umeme viwandani na majumbani kutoka 60 mwaka 2015 na kufikia 117.8 mwaka huu.
Hayo yamebainika wakati mkuu wa mkoa wa Pwani ,mhandisi Evarist Ndikilo alipokwenda kutembelea kituo hicho ambacho kiliungua na kusababisha changamoto ya upungufu wa umeme ambapo kimefanyiwa maboresho na kuongeza transfoma itakayowashwa mwezi ujao na kuongeza upatikanaji wa umeme wa MVA 120.
Ndikilo alisema, ameridhishwa na kasi ya shirika la umeme Tanesco chini ya meneja mhandisi Mahawa Mkaka ,kutekeleza kwa vitendo mpango mkakati unaoendana na mahitaji ya umeme na hatimae kufikia adhma ya mkoa ya UKANDA wa viwanda .
"Kituo hiki kinapeleka pia umeme maeneo ya viwanda Zegereni kwenye viwanda 25 na majumbani, Bandari kavu ya Kwala na kina hudumia wateja 182,000 kati ya hao ni viwanda vya kati na vikubwa 322 ,hongereni sana 'alieleza Ndikilo .
Aidha,aliitaka Tanesco kushughulikia changamoto ya Mkuranga kuendelea kupata umeme kituo cha umeme Mbagala wakati wilaya hiyo imesheheni kwa viwanda hivyo iondokane na kutegemea umeme katika kituo hicho.
Hata hivyo Ndikilo alielekeza taasisi nyingine wezeshi ya DAWASA na ile inayohusika na barabara kuendana na kasi ya mkoa kuinua sekta ya uwekezaji kwa kufikisha huduma muhimu maeneo ya viwanda .
Awali akitoa taarifa ya utekelezaji na maboresho ,meneja wa Tanesco mkoani Pwani ,mhandisi Mahawa Mkaka alisema,mwaka 2018-2020 walikuwa wakihudumia viwanda 1,275.
" Tunaishukuru serikali ya awamu ya tano kwani tumeweza kuwa na miradi mingi ikiwemo mradi wa REA III awamu ya kwanza uliogharimu bilioni 37 na kufikia wateja zaidi ya 6,000,mradi wa Peri-Urban bilioni 65 na kuunganisha maeneo 178 na mradi wa ujazilizi ambao unatarajia kuanza bilioni 10 ambapo maeneo 116 yatafikiwa"alifafanua Mkaka.
Mkaka alieleza, miradi ya Tanesco kwa mwaka wa fedha 2021-2022 itagharimu bilioni 10.2 kwa ajili ya kuboresha sekta hiyo na kusogeza huduma ya umeme maeneo 121.
No comments: