HUWEZI KUTENGANISHA KODI NA MAENDELEO-MKUU WA WILAYA MBARALI

 

Mkuu wa Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya Mhe. Reuben Mfune akizungumza na wafanyabiashara (hawapo pichani) wakati wa semina ya wafanyabiashara hao iliyoitishwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wakati wa kampeni ya elimu kwa mlipakodi ambayo imemalizika wilayani humo.
Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya Bw. Elly Jogofu akizungumza na wafanyabiashara (hawapo pichani) wakati wa semina ya wafanyabiashara hao iliyoitishwa na Mamlaka hiyo wakati wa kampeni ya elimu kwa mlipakodi ambayo imemalizika wilayani humo.
Afisa Msimamizi Mkuu wa Kodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Makao Makuu Bw. James Ntalika akiwaelimisha wafanyabiashara wa Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya wakati wa kampeni ya elimu kwa mlipakodi ambayo imemalizika wilayani humo.
Afisa Msimamizi wa Kodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Makao Makuu Bi. Ernester Shirima akimuelimisha mfanyabiashara wa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Makongolosi Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya wakati wa kampeni ya elimu kwa mlipakodi ambayo imemalizika mkoani humo.
Afisa Msimamizi wa Kodi Mwandamizi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Makao Makuu Bi. Julieth Shehiza akimuelimisha mfanyabiashara wa Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya wakati wa kampeni ya elimu kwa mlipakodi ambayo imemalizika wilayani humo.

Afisa Msimamizi Mkuu wa Kodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Makao Makuu Bw. James Ntalika akimuelimisha mfanyabiashara wa Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya wakati wa kampeni ya elimu kwa mlipakodi ambayo imemalizika wilayani humo.

 (PICHA ZOTE NA VERONICA KAZIMOTO)

………………………………………………………………………………………………………………
Na Veronica Kazimoto,Mbarali

Mkuu wa Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya Mhe. Reuben Mfune amewaambia wafanyabiashara wa wilayani hapa kuwa, ni vigumu kutengenisha kodi na maendeleo kwani maendeleo ya nchi yoyote ile duniani hutegemea kodi.

Ameyasema hayo wakati wa semina ya wafanyabiashara hao kufuatia kampeni ya elimu kwa mlipakodi inayoendeshwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ambayo imelenga kuwaelimisha masuala mbalimbali yanayohusu kodi, kusikiliza changamoto zao za kikodi na kupokea maoni kwa ajili ya kuboresha huduma za TRA. 

“Kodi huiwezesha Serikali kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo hapa nchini. Kwa mfano ujenzi wa barabara za lami, ujenzi wa reli ya kisasa, ujenzi wa zahanati na ununuzi wa dawa na mengine mengi, yote haya yanatekelezwa kwa kutumia kodi zinazolipwa na ninyi wananchi, alisema Mhe. Mfune. 

Mhe. Reuben Mfune amewasisitiza wafanyabiashara hao kujenga tabia ya kulipa kodi kwa hiari na kutumia vizuri mashine za kielektroniki za kutolea risiti kwa kutoa risiti kila wanapouza bidhaa na huduma mbalimbali.

Naye, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara wilayani hapa Bw. Michael Mwaiteleke amesema kuwa, kampeni hii licha ya kutoa elimu ya kodi lakini pia inajenga urafiki kati ya wafanyabiashara na TRA na hivyo kuongeza uhiari wa ulipaji kodi nchini.

“Tunaipongeza TRA kwa kuona umuhimu wa kututembelea kwenye maduka yetu na kutuita kwa ajili ya kutuelimisha masuala ya kodi. Hali hii inajenga urafiki kati yetu sisi na TRA na inatupa hamasa ya kulipa kodi kwa hiari na kwa wakati”, alisema Bw. Mwaiteleke.

Kwa upande wake Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania wilayani hapa Bw. Elly Jogofu amewaambia wafanyabiashara hao kwamba, wawe huru wakati wowote kumuona ofisini kwake au kumpigia simu kwa ajili ya kutatua changamoto zinazowakabili zinazohusiana na kodi.

“Ofisi yangu iko wazi na namba yangu ya simu mnayo, hivyo naomba mkikutana na changamoto yoyote ya kikodi, msisite kuja kuniona ofisini au kunipigia simu,” alieleza Bw. Jogofu.

Kampeni ya elimu kwa mlipakodi mkoani Mbeya imemalizika na timu ya maafisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania inayofanya kampeni hiyo inaelekea mkoani Njombe kwa ajili ya kuanza kutoa elimu ya kodi katika mkoa huo.

No comments: