Diwani Kivukoni amuomba JPM majengo yaliyoachwa wazi na Wizara Dar Dodoma

 

 

**************************************

NA MWANDISHI WETU, DAR

DIWANI wa Kata ya Kivukoni, Sharik Coughle (CCM), amewasilisha maombi  katika kikao cha Baraza la Madiwani la Halmashauri  Manispa ya Ilala, kumuomba Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania , Dk. John Pombe Magufuli, kumkabidhi baadhi ya majengo yaliyokuwa yakitumika na ofisi mbalimbali kabla ya  kuhamia Dodoma.

Diwani huyo aliomba Rais Dk. Magufuli  amkabidhi majengo hayo ambayo yako wazi  ili yatumike kwa shughuli mbalimbali za kijamii.

Alisema  Kata yake ya Kivukoni ina shule moja tu ya msingi ambayo ni Bunge lakini haina shule ya sekondari ya kata, haina  zahanati wala kituo cha afya, ofisi ya kata  pamoja na huduma zingine za msingi.

Alibainisha kuwa hali hiyo ni kutokana na  kata hiyo kuwa kati kati ya  Jiji la Dar es Salaam, hivyo kuto kuwa na eneo la wazi la kujenga  majengo ya huduma hizo.

“Kwa kipindi kirefu baada  ya Rais Dk. Magufuli kuhamishia makao makuu Dodoma, majengo mengi yako wazi katikati ya jiji.  Yanaendelea kuchakaa.

Ninamuomba  Rais. Dk. Magufuli, kupitia Baraza hili atukabidhi  badhi ya majengo  ili tuyatumie kwa kuanzisha vituo vya afya, shule ya sekondari  na msingi  na huduma zingine muhimu kwa wananchi wa Kata ya Kivukoni,”alieleza Choughle.

Diwani huyo alisema, Kata ya Kivukoni ambayo  ndani yake  ipo  Ikulu ya  Magogoni, haina  maeneo ya wazi  ambayo yanaweza kutumika kwa ujenzi wa  huduma muhimu kama hizo  hivyo ni vema majengo yaliyopo ambayo yako wazi yakatumika.

“Manispaa ya Ilala inatenga fedha nyingi kujenga shule mpya na hata kuongeza madarasa, hospitali  na vituo vya afya, kama itampendeza Rais basi tunaomba  majengo haya  yaliyo wazi  yatumike kwa huduma hiyo ili kupunguza hata gharama za ujenzi,”alisema Choughle.

Alibainisha  kuwa anaamini Rais Dk. Magufuli   ni msikivu na anaweza kulitathimini ombi hilo kwani majengo mengi ya serikali  ambayo awali yalikuwa yakitumika  kwa shughuli mbalimbali jijini Dar es Salaaam yamebaki kama magofu.

“Naiomba Manispaa ya Ilala kupitia baraza hili tukufu  iliwasilishe hili kwa Rais Dk. Magufuli ili tupate majengo hayo.

Kivukoni tunahitaji shule, vyuo vya ufundi, zahanati, vituo vya afya,hospitali, ofisi ya mtendaji na  huduma nyingine. Tunaweza kupewa jengo moja kwa shughuli za kiutendaji na jengo lingine kwaajili a shule au zahanati,”alieleza Shoughle.

Alisema Shule ya Msingi Bunge ambayo ni tegemeo, imefurika wanafunzi na miundo mbinu yake imechaka hivyo  kuna umuhimu wa kata hiyo kuwa na shule nyingine ya msingi atakayo punguza msongamano katika Shule ya Msingi Bunge.

“Bunge  ya sasa siyo ile ya zamani. Imechakaa na  watoto ni wengi. Inapoteza hadhi yake ya ubora. Kama tutapata jengo la kuanzisha  shule nyingine ya msingi basi Bunge itapumua,”alisema Choughle.

Diwani  wa Kata ya Kinyerezi, Leah Mngitu, aliunga mkono hoja hiyo   na kuliomba baraza kutilia uzito  kwani huduma za wananchi ni muhimu.

“Hili ni wazo zuri na tunaomba liingizwe kwenye umbukumbu za kikao,”alisema Leah.

Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala, Omari Kumbilamoto, alisema tayari Diwani Choughle alishaliwasilisha ombi hilo katika ofisi yake na linaendelea kufanyiwa kazi.

No comments: