WAZIRI MHANDISI CHAMURIHO AITAKA NCC KUMALIZA MGOGORO KIDATU-IFARAKA

 



Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Dkt.  Leonard Chamuriho akimsikiliza Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Morogoro Mhandisi Nkolante Ntije, wakati akimweleza  hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa barabara ya Mikumi-Ifakara kwa kiwango cha lami, sehemu ya kidatu –Ifakara (km 66.9), wakati Waziri huyo alipokagua mradi huo mwishoni mwa wiki mkoani humo.

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Leonard Chamuriho akitoa maelekezo  kwa wakandarasi wa Kampuni ya Reynolds construction Company (RCC) wanaojenga barabara ya Kidatu-Ifakara(KM 66.9 ) mkoani Morogoro, wakati alipotembelea mradi huo mwishoni mwa wiki Mkoani Humo.

Muonekano wa hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa Barabara ya Dumila-Kilosa –Mikumi, sehemu ya Rudewa-Kilosa (Km 24). Mradi huo unatarajiwa kukamilika Agust mwaka huu.

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Dkt. Leonard Chamuriho (mwenye shati la kitenge) akimsikiliza Msimamizi wa Mradi wa wakala wa barabara Tanzania (Tanroads) Mkoani  Morogoro Mhandisi Robert Mwita akitoa maelezo  ya maendeleo ya ujenzi wa Barabara ya Dumila-Kilosa-Mikumi ;sehemu ya Rudewa –Kilosa(Km 24), wakati Waziri huyo alipokagua mradi huo mwishoni mwa wiki mkoani Morogoro.

************************************************

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Dkt. Leonard Chamuriho, ameliagiza Baraza la Ujenzi la Taifa (NCC), kukutana na Wizara ya Fedha na Mipango, Mkandarasi na  Mhandisi Mshauri ili kutatua changamoto  za kimkataba zilizopo katika ujenzi barabara ya Mikumi-Ifakara, sehemu ya Kidatu-Ifakara yenye urefu wa Km 66.9.

Akizungumza mara baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa barabara hiyo Mkoani Morogoro Waziri Mhandisi Chamuriho amesema uwepo wa hizo unachangia ucheleweshaji wa ukamilishaji wa mradi huo na hivyo kuwacheleweshea wananchi maendeleo.

“Kutoelewana kati ya Wadau wote wanaojenga barabara ni tatizo ambalo linasababisha mradi kutojengwa kwa kasi, tunahitaji changamoto hizo mzikamilishe na mradi ukamilike kwa wakati’ Amesema Waziri Mhandisi Chamuriho.

Waziri Mhandisi Chamuriho amewaagiza Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kuhakikisha changamoto zote zinazoanishwa baada ya kikao cha wadau zinatekelezwa  kwa kuzingatia makubaliano.

Kwa upande wake Meneja wa wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Morogoro Mhandisi  Nkolante Ntije amemuhakikishia Waziri Mhandisi Chamuriho kuwa watatakeleza maelekezo na kuwasilisha taarifa Wizarani ndani ya muda mfupi.

Katika hatua nyingine Waziri chamuriho amekagua ujenzi wa barabara ya Dumila –kilosa-Mikumi ;sehemu ya Rudewa-Kilosa (km24) na kuridhishwa na maendeleo ya ujenzi wake na kuwataka  wakandarasi wazawa Umoja –Kilosa JV  kuongeza kasi ili mradi ukamilike kwa wakati.

Kwa upande wa Msimamizi wa Mradi huo  Mhandisi Robert Mwita amesema kuwa Pamoja na uwepo wa  changamoto za mvua , Mradi unaendelea kutekelezwa na unatarajiwa kukamilika mapema mwezi wa nane mwaka huu.

No comments: