WAZIRI GWAJIMA AIPONGEZA HOSPITALI YA MUHIMBILI KWA KUWA NA HUDUMA ZA UBINGWA WA HALI YA JUU
***********************************************
Na Emmanuel Malegi-DSM
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima ameipongeza Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa kuwa na huduma za ubingwa wa hali ya juu ambao haupatikani katika nchi nyingi za kiafrika.
Waziri Gwajima ametoa pongezi hizo leo wakati alipofanya ziara katika Hospitali hiyo ili kuona hali ya utoaji wa huduma hususan katika vitengo mbalimbali kama kitengo cha huduma za dharura, wodi ya wagonjwa mahututi, wodi za watoto n.k.
“Nimeamua kuja hapa Muhimbili kwanza kuona hali ya utoaji wa huduma, kuona mafanikio na changamoto lakini pia kuona mwelekeo wao kwa ujumla. Kifupi napenda kutambua mchango wao mkubwa katika kuboresha huduma za afya nchini na zaidi huduma za ubingwa na ubingwa wa hali ya juu”. Amesema Dkt. Gwajima.
Dkt. Gwajima amesema katika kipindi cha miaka mitano Hospitali ya Muhimbili imechangia kwa kiasi kikubwa kuokoa fedha za Serikali kwa kupeleka wagonjwa wa rufaa nje ya nchi kutokana na huduma nyingi za kibingwa kuanza kupatikana Hospitalini hapo.
Aidha, Dkt. Gwajima amesema Hospitali hiyo ya Taifa imejipanga vyema katika kipindi cha miaka mitano ijayo ambapo kutaanzishwa huduma ya kupandikiza uroto wa mifupa (Bone marrow transplant) huku wataalamu wa kufanya kazi hiyo wakiwa tayari wameshafika na baadhi ya vifaa vikiwa tayari vimefungwa na hivi sasa kinasubiriwa kifaa kimoja kifike ili huduma hiyo ianze kutolewa kuanzia mwezi Machi mwakani.
Pamoja na kujiridhisha na huduma mbalimbali zinazotolewa katika Hospitali hiyo, Dkt. Gwajima pia ametembelea ujenzi wa jengo litakalotumiwa na wagonjwa binafsi wenye haraka (Fast Track Services) ambalo Serikali imetoa zaidi ya Bilioni nne za kufanikisha ujenzi huo ambao upo katika awamu ya kwanza.
Dkt. Gwajima ameipongeza Hospitali hiyo kwa kuwa na huduma ya kutoa misamaha kwa wagonjwa wasiojiweza lakini amewataka wananchi kufuata taratibu zilizowekwa ili kupata misamaha hiyo kuliko kulalamika. Pia ameendelea kusisitiza wananchi wajiunge na mifuko ya bima ya afya ya CHF iliyoboreshwa na NHIF ili waondokane na gharama kubwa za matibabu pindi wanapopata changamoto za afya.
Halikadhalika Dkt. Gwajima amewataka watumishi wa afya kutanguliza mbele kutoa huduma kwa wagonjwa kwanza halafu gharama za matibabu zifuate badae, lengo likiwa ni kuzuia vifo vinavyoweza kutokea kwa ucheleweshaji wa kupata matibabu.
Hospitali ya Muhimbili inatoa misamaha ya matibabu takriban Milioni 800 hadi 900 kwa mwezi.
No comments: