SERIKALI KUTUMIA MBINU YA MAKAMBI KWA WANAFUNZI WASICHANA KUWAWEZESHA KUFIKIA MALENGO
SERIKALI kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu chini ya Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania imepanga kutumia Mbinu ya kuwaweka kwenye Kambi wanafunzi wasichana balehe wanaotoka kwenye kaya masikini, kwa kuwapa Mafunzo ya namna ya Kujikinga na VVU na UKIMWI, Stadi za Maisha na Mafunzo ya masomo ya Sayansi na Hisabati, ili waweze kufanya vizuri kwenye masomo, kujitambua, kujiamini na kuweza kutimiza malengo yao.
Kwa mara ya Kwanza Ofisi ya Waziri Mkuu, kupitia Tume ya Kudhibiti
UKIMWI Tanzania imeratibu kambi ya majaribio ya siku tano, kuanzia
tarehe 4-8 Januari, 2021, Jijini Dodoma, kwa wanafunzi wasichana 105
wa shule 18 kutoka kaya masikini zilizo chini ya mpango wa TASAF za
Halmashauri ya wilaya ya Bahi, jijini Dodoma.
Akiongea wakati wa kufunga kambi hiyo Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu
(Sera na Uratibu), Bi. Dorothy Mwaluko amebainisha kuwa kufanikiwa kwa
majaribio ya kambi hiyo kutawezesha serikali kupitia ya Tume ya
Kudhibiti UKIMWI Tanzania, kuendesha kambi za namna hiyo kwenye
Halmashauri nyingine hapa nchini ili kuweza kuwasaidia wanafunzi
wasichana balehe wanaotoka kaya masikini kuweza kutimiza malengo yao.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Bahi, Mwanahamisi Munkunda,
amefafanua kuwa wilaya hiyo wamepanga kuwa na utaratibu wa kuwa na
kambi za wanafunzi wasichana balehe kila baada ya miezi sita kwa
wanafunzi 1,324 walioko ndani ya shule. Aidha, ameeleza kuwa wilaya
hiyo tayari inao mfuko wa elimu wa Halmashauri ambao utawaendeleza
kieleimu wanafunzi hao hadi elimu ya chuo kikuu.
Naye Kaimu Mkurugenzi Idara ya Mwitikio wa Taifa, Tume ya Kudhibiti
UKIMWI Tanzania, Audrey Njelekela, amefafanua kuwa Kambi hiyo ni
sehemu ya Utekelezaji wa mradi wa TIMIZA MALENGO unaowalenga Wasichana Balehe na Wanawake Vijana walioko ndani na nje ya shule kutimiza malengo yao. Kwa sasa mradi huo unatekelezwa katika Halmashauri 10 nchini za mikoa ya Dodoma, Singida na Morogoro ambapo mikoa ya Tanga
na Geita imeongezwa kwenye mradi huo. Amesisitiza kuwa Mradi wa kambi
utatekelezwa pia katika Halmashauri za mikoa hiyo.
Wakiongea kwa nyakati tofauti baada ya kufunga Kambi hiyo Mratibu wa
Mradi huo wa Kambi Salum Kilipamwambu ambainisha kuwa Tafiti za elimu
ya sekondari zinaonesha wanafunzi wasichana wa sekondari wamekuwa
wakishindwa kuhitimu masomo yao kwa kukosa uelewa na kutojitambua na
kujiamini, naye, Mwajuma Hamisi kutoka shule ya sekondari Kigwe, Bahi
jijini Dodoma, ameeleza kuwa mafunzo hayo yamewawezesha kujitambua,
kujiamini na wameongeza weledi kwenye masomo ya sayansi na Hisabati
hivyo wataweza kufanya vizuri kwenye masomo na hatimaye kuweza
kutimiza elimu.
No comments: