BASHUNGWA AAHIDI KUPIGANIA HAKI ZA WAANDISHI, ASISITIZA UZALENDO



 Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Innocent Bashungwa.


Na A Suleiman Msuya


WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Innocent Bashungwa amesema atatumia nafasi yake kutetea haki za waandishi wa habari nchini huku akisisitiza uzalendo na utaifa kwa kada hiyo.

Kauli ya Waziri Bashungwa inakuja baada ya kuwasikiliza waandishi walioshiriki mjadala wa pamoja kuhusu changamoto wanazopitia katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku.

Wakiwasilisha maelezo yao waandishi walimueleza Waziri Bashungwa kuwa pamoja na wao kuwa na sifa za kitaaluma  asilimia 80 ya wamiliki wa vyombo vya habari  wahatoi mikataba ya ajira, wenye mikataba utekelezaji wake ni wakusuasua, sheria za kazi hazizingatiwi.

Aidha waandishi walimueleza waziri kuwa waandishi wengi wanafanya kazi kama vibarua kwa muda mrefu huku wakidhibitiwa kama waajiriwa.

Akijibu hoja hizo za waandishi Waziri Bashungwa amesema uamuzi wa kukutana na waandishi ni kutoa fursa kueleza hali halisi ili ajue anaanzia  wapi.

Amesema sekta ya habari ni muhimu kwa maendeleo ya nchi hivyo ni jambo la aibu na kusikitisha iwapo kuna haki zinakiukwa bila hatua kuchukuliwa.

"Nimewaita hapa ili tuelezane hali halisi mnayopitia ili sisi kama wizara tuweze kuchukua hatua stahiki," amesema.

Bashungwa amesema haingii akilini watu wanafanya kazi hatarishi na wamesomea ila hawana mikataba hivyo kuahidi kushirikiana Ofisi ya Waziri Mkuu Ajira na wadau wengine ili muafaka uweze kupatikana kwa haraka.

Waziri huyo amesema wizara ina jukumu la kutatua changamoto wanazopitia waandishi kwa kuzungumza nao ili kuwa kitu kimoja kwani ni wadau muhimu kwa nchi na wananchi.

 Aidha, amewataka wamiliki wa vyombo vya habari kuzingatia sheria ya kazi inavyotaka katika kutekeleza mikataba ya wafanyakazi na kwamba hawatosita kuchukua hatua za kisheria kwa mwajiri anayekiuka taratibu.

Halikadhalika Waziri Bashungwa amemtaka Katibu Mkuu wa Wizara hiyo kuhakikisha baraza la habari na bodi ya habari vinaundwa ili waandishi waweze kupata eneo la kufikisha matatizo yao.

Pamoja na kuahidi kutetea haki za waandishi Waziri Bashungwa amewataka waandishi wajiendeleze kielimu ili kukidhi hitaji la Sheria ya Habari namba 12 ya mwaka 2016 inayotaka sifa ya mwandishi wa habari awe na elimu ya diploma.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Abdallah Ulega amesisitiza uzalendo na utaifa kwa waandishi wa habari.

Ulega amesema waandishi wanapaswa kuandika mazuri ambayo yanafanyika hapa nchini ili yaweze kujulikana na kuvutia wawekezaji ikiwemo sekta ya wanayoisimamia.

"Nyie ni watu muhimu sana katika kusukuma gurudumu la maendeleo naomba mtumie kalamu zenu kuyalezea mazuri yanayofanywa na Serikali  inayoongozwa na Rais John Magufuli.

Lakini kwa umaalum zaidi sekta hii tunaomba muitangaze sana kwani ina kundi kubwa ambalo linahitaji mchango wenu kwa mfano Januari 12, 2021 tunacheza na DRC Congo tunaomba mtangaze nachambua mchezo huo," amesema Naibu Waziri Ulega.

No comments: