WAKULIMA MANG’OLA WALIA KUPOROMOKA KWA BEI VITUNGUU


Na Seif Mangwangi, Arusha
 
WAKATI Wataalam wa afya duniani wakiendelea na harakati za kutafuta tiba ya mlipuko wa Covid -19, athari za ugonjwa huo zimeendelea kuonekana nchini Tanzania hasa katika sekta ya Kilimo.
 
WAKULIMA wa kitunguu katika eneo la Kata ya Mang’ola lililopo wilayani Karatu jijini Arusha, wamesema bei ya kitunguu imeporomoka na kuwasababishia hasara kubwa tofauti na matarajio yao.

Wamesema kuporomoka huko kwa bei ni baada ya kuibuka kwa janga la Corona duniani , kwani kwa sehemu kubwa vitunguu ambavyo vinalipwa katika eneo hilo soko lao kubwa liko kwenye nchi jirani zikiwemo za Kenya ya Uganda ambao wamekuwa wakinunua kwa bei ya juu tofauti na bei ya ndani.

Wakizungumza leo baadhi ya wakulima katika bonde hilo maarufu nchini kwa uzalishaji wa vitunguu vyenye ubora wa hali ya juu katika ukanda wa Afrika Mashariki wamesema Corona imewaathiri kwa kiwango kikubwa wakulima wa vitunguu, kabla ya kuibuka kwa Corona walikuwa wakipeleka vitunguu hivyo hadi nchi za Ulaya, hivyo walikuwa wakinufaika na kilimo hicho kiasi cha kuvutia watu wengine kujihusisha nacho.

Given Kessy ni mmoja wa  wakulima katika bonde hilo anasema tangu ugonjwa wa Corona ulipoingia nchini hali ya mauzo ya kitunguu imeshuka kwa kasi kubwa kutokana na kutegemea soko la ndani ya nchi.

Amesema wakulima katika bonde hilo wamepata hasara kubwa kutokana na mauzo ya kitunguu kuwa ya bei ya chini ambayo hailingani na hali halisi ya gharama ambazo wamekuwa wakizitumia tangu kutayarisha shamba hadi kuvuna.

"Nimelima ekari moja ambapo hadi hivi sasa nimeshatumia si chini ya Sh.Milioni 6, fedha  ambayo nilitegemea kuipata na faida yake baada ya kuuza kitunguu kwa faida, lakini bei zilizopo sokoni hivi sasa zinatisha, ni ndogo na haziwezi kurejesha gharama nilizotumia kulimia,"amesema.

Kwa upande wake Mkulima Emmanuel Laizer anasema tangu kulipuka kwa Corona, wakulima wa vitunguu bonde la Mang’ola wamekuwa wakipata hasara kutokana na gharama kubwa wanayoitumia kukuzia zao hilo.

"Nimekuwa nikilima maeneo mbalimbali nchini, kama hapa Mang’ola na Singida, ila gharama za hapa ni kubwa sana kulinganisha na gharama za Singida, kitunguu cha hapa ni kizuri sana na kwa kawaida bei yake pia ni ya ghali, ila baada ya ugonjwa wa Corona kuibuka hali imekuwa tofauti, tumekuwa tukipata hasara tu badala ya faida,"amesema.

Ameongeza baadhi ya wakulima wakubwa na wenye uwezo wamekuwa wakilazimika kuvuna vitunguu vyao na kuvihifadhi kwa muda katika  maghala (store) kutokana na tatizo hilo la kushuka sana kwa bei  na kukosekana kwa wanunuzi wa vitunguu hivyo.

Ameiomba Serikali kuangalia namna ya kuwapatia masoko mengine nje ya nchi mbali ya Kenya na Uganda ili waweze kufidia gharama ambazo wamekuwa wakiingia wakati wa kulima zao hilo lakini pia kufanya mawasiliano na viongozi wa Kenya ili wanunuzi wa zao hilo waruhusiwe kuingia nchini kama mwanzo.

"Bei ya gunia moja la kitunguu maarufu kama neti ya Magufuli iliyokuwa inauzwa Sh.100,000 hadi 200,000 imeshuka na hivi sasa inauzwa kati ya Sh. 30,000 hadi Sh.50,000.Hata hivyo hali imebadilika tangu kulipotokea Corona, wanunuzi kutoka katika nchi hizo walisitisha safari zao hasa nchini Kenya ambapo mpaka wa Tanzania na nchi hiyo ulifungwa ili kuzuia kuenea kwa maambukizi,"amesema.

Shamba la kitunguu baada ya kuvunwa na vitunguu kupakiwa kwenye magunia tayari kuuzwa.

No comments: