MADALALI WA MAGARI ARUSHA WALIA UKATA BAADA YA MLIPUKO WA UGONJWA WA CORONA


Na Seif Mangwangi, Arusha

MADALALI wa magari jijini Arusha ambao wamekuwa wakinunua na kuuza magari kwa wateja mbalimbali na wao kujipatia fedha kutokana na mauzo wanayoyafanya wamesema janga la Corona limeathiri kwa kiwango kikubwa biashara hiyo.

Wakizungumza jijini hapa, madali hao wamesema tangu mlipuko huo ulipotokea kazi biashara imekuwa ngumu baada ya wanunuzi wa magari kupungua na wao kujikuta wakikosa kazi na kulazimika kutafuta njia mbadala za kupata fedha za kujikimu.

Akizungumza kwa niaba ya madalali wenzake wa magari jijini Arusha, Robby Mmari amesema mwanzoni ugonjwa ulipotangazwa kuingia nchini biashara ilibadilika, hivyo wakawa wanapatikana wateja wa kununua magari madogo badala ya ununuzi wa magari makubwa kama hapo mwanzo.
"Ugonjwa ulipotangazwa tu kuingia nchini, tulipata wateja kadhaa wa kununu magari madogo kama IST na Passo ya Sh.milioni nne, tano hadi sita ambayo hayatumii mafuta mengi katika kuziendesha, lakini pia wengi walikimbilia kununua gari hizo ili kuwasaidia kwenye usafiri wakiepuka mikusanyiko,"amesema.

Ameongeza watu wengi walilazimika kununua gari hizo ndogo baada ya kuelezwa kuwa ugonjwa wa Corona unaambukizwa kwa njia ya kugusana hivyo waliamua kuepuka magari ya jumla na kununua gari ndogo watakazoendesha wenyewe kwenda kwenye shughuli zao.

"Pia wengine waliokuwa wananunua magari madogo ni wale wenye kumiliki gari kubwa kama Toyota Cruiser, Prado, Suzuki ambazo kwa kawaida zinatumia fedha nyingi sana kuziendesha, kwa hiyo walikuwa wanabana matumizi baada ya uchumi kuanguka,"anasema.Anasema pamoja na hali ya ugonjwa huo nchini kutengemaa, wao kama madalali wameendelea kuathirika kwa kuwa wateja wanaonunua magari wamepungua sana tofauti na kabla ya mlipuko wa ugonjwa huo.

Alipoulizwa kuhusu wateja wao wengi walikuwa wakifanyakazi katika sekta gani, Mmari anasema sekta ya utalii na madini ndio iliyokuwa kimbilio lao kwani utalii ukipanda watu wengi walikuwa wakinunua gari aina ya Toyota Cruiser lakini hivi sasa hawanunui.

"Wateja wetu wengi walikuwa ni wa sekta ya utalii na madini, tulikuwa tunauza sana Toyota Cruiser ila sasa hivi hawanunui tena na badala yake wako wachache wanauza gari zao lakini pia kwa gharama ndogo sana ili waweze kupata kipato cha kuendeshea familia baada ya utalii na sekta ya madini kuanguka na kukosa ajira,"amesema.

Kwa upande wake Peter Masawe anayefanya kazi yake ya udalali wa magari katika eneo la Kaloleni Jijini hapa anaiomba Serikali kuangalia namna ya kurekebisha uchumi wa wafanyabiashara wa Arusha ili na wao kupitia wafanyabiashara hao waweze kupata kipato kama zamani kupitia kazi hiyo ya udalali.

 

Robby Mmari Dalali maarufu wa magari Arusha akiwa shambani baada ya mlipuko wa corona akijaribu maisha mengine kujipatia kipato

No comments: