RC BYAKANWA AUNGWA MKONO MIHAMBWE



Na Mwandishi wetu Mihambwe

Mkuu wa Mkoa Mtwara Mhe. Gelasius Gasper Byakanwa ameungwa mkono na Wananchi wa Tarafa ya Mihambwe na viunga vyake kupitia kampeni aliyoianzisha ya kuondoa mapori na kuongeza uzalishaji wa zao la Korosho na mazao mengineyo.

Hayo yamejidhirisha kupitia mkutano uliofanyika Kijiji cha Misufini uliotangaza rasmi kampeni hiyo ambapo RC Byakanwa amesisitiza ni lazima kila Mtu apanie kuongeza uzalishaji kwa kupanda kwa utaratibu, kupandikiza Mikorosho na kufufua mashamba yaliyotelekezwa. 

"Kila Mwananchi ni lazima awe na shamba la kulima na alime kisasa ikiwemo kupanda kwa utaratibu, kuondoa mikorosho mizee na kulima mazao mchanganyiko. Nataka Watu mfanye kazi usiku na mchana." alisisitiza RC Byakanwa.

RC Byakanwa aliambatana na timu ya Wataalamu wa kilimo ambao walienda kutoa elimu ya namna ya kuongeza uzalishaji wa Korosho na Wananchi wengi wamempongeza RC Byakanwa kwa ubunifu wake huo kwani ilikuwa ni kiu yao ya siku nyingi kupata elimu ya kilimo kufuatia uzalishaji wa Korosho kuzidi kushuka siku hadi siku.

"Mkuu wa Mkoa Mtwara Mhe. Byakanwa  amevunja rekodi ya viongozi wote kwa kutuletea elimu ya kuongeza uzalishaji wa Korosho, Wananchi wa Tarafa ya Mihambwe tunamuunga mkono sana kwa hili. Nami nipo tayari kabisa shamba langu litumike kama shamba darasa kwani nimechoka kila siku uzalishaji kuzidi kupungua." Alisema Ndugu Awadhi Rashid mkazi wa Kijiji cha Mihambwe.

Akizungumza na Mwandishi wetu baada ya mkutano huo, Afisa Tarafa Mihambwe Emmanuel Shilatu amempongeza sana RC Byakanwa kwa kuja tena kivingine ambapo safari hii amekuja kuongeza uzalishaji wa Korosho.

"Mhe. Byakanwa ni kiongozi mbunifu sana. Alianza na kampeni ya shule ni choo ambayo ilifanya vyema sana na leo hii kero ya vyoo shuleni imepungua sana. Leo hii kaja na kuongeza uzalishaji wa Korosho ambayo natumai itasaidia sana kumkomboa Mkulima wa Korosho. Kampeni hii inaenda kukata kiu ya elimu ya kilimo bora cha Korosho na hivyo tunatarajia uzalishaji kuzidi kuongezeka. Kwa niaba ya Wakazi wa Tarafa ya Mihambwe tunampongeza sana na tunamuunga mkono Mhe. Byakanwa." Alisema Gavana Shilatu.

RC Byakanwa amekuja na kampeni ya kuondoa mapori na kuongeza uzalishaji ambapo imelenga kuondoa mikorosho mizee na isiyozaa, kuondoa mikorosho iliyopandwa bila ya utaratibu, kufufua mashamba yaliyotelekezwa na kuanzisha mashamba mapya sanjali na kuongeza uzalishaji wa mazao mengineyo.




 

No comments: