RAIS MAGUFULI AWAPUNGUZIA ADHABU WAFUNGWA 256 WALIOHUKUMIWA KUNYONGWA, AWATAKA MAWAZIRI KUFANYA MAAMUZI


RAIS Dk John Magufuli amewapunguzia adhabu wafungwa 256 ambao walikua wamehukumiwa kunyongwa na badala yake amewapunguzia adhabu hiyo badala yake watatumikia kifungo cha maisha.

Msamaha huo ameutoa leo katika siku ya kumbukumbu ya Uhuru ambapo pia alikua akiwaapisha mawaziri na manaibu waziri aliowateua hivi karibuni ambapo pia amewapunguzia adhabu wafungwa wengine 3316 ambao wana makosa ya kawaida.

Akizungumza katika uapisho huo ambao amewaapisha mawaziri 21 na manaibu waziri 22 huku Naibu Waziri mmoja wa Madini akishindwa kuapa ambapo Rais Magufuli amesema watajaza nafasi yake kwa sababu ameshindwa kusoma kiapo chake.

Amewataka mawaziri waliochaguliwa kufanya kazi kwa ushirikiano na manaibu na siyo kuwanyima fursa manaibu wao lakini pia akiwataka kufanya maamuzi hata kama ni mabaya badala ya kukaa kimya bila kufanya maamuzi.

" Msikae ofisini nendeni kwa wananchi mkatatue changamoto zao, kama ni waziri wa maji kashughulikie kero ya maji kweli, msiwe mawaziri wa kupiga picha tu na kuweka WhatsApp, mzingatie pia na maadili hasa ya kitanzania.

Wizara ya Elimu niwatake mkalifanye somo la Historia kuwa la lazima vijana wetu wafundishwe historia ya Nchi yetu hii itasaidia hata kuongeza uzalendo. Tamisemi kuna shida pia, Jafo umefanya kazi kubwa kwenye kuzunguka lakini bado unapaswa kusimamia ubadhirifu wa fedha katika Halmashauri zote," Amesema Rais Magufuli.

Amemuagiza Waziri wa Tamisemi, Selemani Jafo kumsimamisha kazi Mkurugenzi wa Halmashauri ya Geita ambaye alinunua gari lake la kutembelea lenye thamani ya Sh Milioni 400 kinyume na utaratibu.

Rais Magufuli amewapongeza mawaziri hao na kuwataka kufanya kazi wakimtangulize Mungu ili waweze kutimiza yale yote ambayo yameelekezwa na Ilani ya Uchaguzi sambamba na muongozo wa baraza la mawaziri.

Katika tukio hilo la uapisho Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi na Utawala Bora, Kepteni George Mkuchika ndie aliyekua wa kwanza kuapa kiapo hicho na kufuatiwa na Waziri wa Ardhi,  William Lukuvi.

Akizungumzia jinsi alivyofanya uteuzi huo, Rais Magufuli amesema wamezingatia nafasi za Mikoa, maadili na mienendo binafsi huku akiwataka wasijione kwamba wao ni bora zaidi ya wengine kwani wana akiba kubwa ya watu ambao wanaweza kuteuliwa katika nafasi hizo.

Rais Dk John Magufuli akimuapisha Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof Joyce Ndalichako katika hafla ya uapisho wa Baraza la Mawaziri leo Ikulu Chamwino mkoani Dodoma.
 Rais Dk John Magufuli akimuapisha Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-Tamisemi, Selemani Jafo kuwa waziri katika wizara hiyo katika hafla iliyofanyika Ikulu Chamwino, Dodoma.

No comments: