PROF. ELISANTE: TUNAHITAJI UCHAKATAJI ZAIDI WA MAZIWA
Na Bakari Madjeshi, Michuzi TV
KATIBU Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel amesema uchakataji wa Maziwa unahitajika zaidi nchini kutokana na uhitaji mkubwa maziwa hayo katika jamii ya Watanzania.
Prof. Elisante ameyasema hayo wakati wa Bonanza la Maziwa lililoandaliwa na Bodi ya Maziwa nchini kwa kushirikiana na Wizara ya Viwanda na Biashara sambamba na Wadau wa Maziwa nchini kote, amesema ili uchakataji huo uongezeke lazima kuwepo na Soko la ndani na Nje.
“Viwanda vya Maziwa vimefika 99, Maziwa yanazalishwa mwaka 2020 ni Lita Bilioni 3.01, Unywaji wa Maziwa kila siku ni zaidi ya Lita Bilioni 8.3 hivyo tunahitaji kuongeza zaidi Ng’ombe wa Maziwa ili kuongeza wingi wa uzalishaji”, amesema Prof. Elisante.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara nchini (TANTRADE), Bi. Latifa Khamis ameahidi kuendelea kuhasisha unywaji wa Maziwa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa uzalishaji wa Maziwa, amesema wako tayari kutoa maeneo ndani ya viwanja vya Sabasaba ili kutoa fursa kutangaza na kuhasisha unywaji wa maziwa kwa jamii.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Godwin Gondwe kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam ametoa wito kwa vijana wa Jogging kuendelea kuhimiza Jamii kufanya mazoezi ili kuepukana na magonjwa mbalimbali yasiombukiza sambamba na unywaji wa maziwa kwa wingi.
Mwenyekiti wa DAR JOGGING CLUB, Ramadhan Namkoveka amewataka Wanajogging hao kuendelea kunywa maziwa kwa wingi na kuweza kufikia kiwango kinachohitajika na Serikali. “Dhumuni kubwa tufanye mazoezi, tunywe maziwa kwa sababu kwenye maziwa kuna vitu vingi ikiwemo virutubisho Protein na vingine vingi tu”, ameeleza Namkovemba.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel akizungumza na Wana Jogging katika Viwanja vya Sabasaba jijini Dar es Salaam ikiwa na Bonanza la Maziwa lililofanyika viwanjani hapo sambamba na uhamsishaji unywaji wa maziwa.
Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Godwin Gondwe akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam katika Bonanza la Maziwa lililofanyika viwanja vya Sabasaba jijini Dar es Salaam.
Msanii wa Bongo Fleva nchini, Shetta aka Baba Kayla akiwa katika moja ya mazoezi yaliondaliwa na Bodi ya Maziwa kwa dhumuni la uhamasishaji unywaji wa maziwa.
No comments: