FORVAC yatoa mashine ya kuongeza thamani ya mazao Ruvuma

Na Albano Midelo

PROGRAM ya kuendeleza mnyororo wa thamani wa mazao ya misitu(FORVAC) imekiwezesha kijiji cha Sautimoja kilichopo wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma kununua mashine ya kisasa ili kuchakata mbao na kuongeza thamani.

Mratibu wa FORVAC Mkoa wa Ruvuma Marcel Mtunda akizungumza mbele ya waandishi wa habari baada ya kuona utendaji wa mashine hiyo,amesema mashine hiyo ya kuchakata magogo ni ya kisasa na inaweza kutembea kwenda hata msituni kuchaka magogo.

Amesema mashine hiyo ambayo imenunuliwa nchini Canada kwa shilingi milioni 70, inapochakata mbao,ubao unaotoka unakuwa na ubora wa hali ya juu ukilinganisha na mbao ambazo zimechakatwa na mashine nyingine.

“Mbao zilizochakatwa na mashine hii, zina soko kubwa na bei yake ni ya juu tofauti na mbao zilizochakatwa na mashine nyingine hali hiyo ndiyo imeifanya mashine hii kuwa na sifa tofauti ikiwemo kuzalisha mbao nyingi zenye ubora kwa haraka’’,alisema Mtunda.

Mtunda amesema program ya FORVAC katika Mkoa wa Ruvuma inafanyika katika wilaya tano ambazo ni Tunduru, Namtumbo, Songea,Mbinga na Nyasa na kwamba FORVAC imedhamiria Kuongeza faida za kiuchumi, kijamii na kimazingira kutokana na usimamizi endelevu wa raslimali za misitu 

Kwa upande wake Mtaalam wa Misitu wa Mradi wa FORVAC Alex Njahani  amesema katika nchi nzima mradi huo unatekelezwa katika wilaya 11 zilizopo mikoa ya Tanga,Ruvuma,Lindi na Dodoma

Hata hivyo amesma hadi sasa mashine mbili tu kuchakata mbao  zimenunuliwa katika  mikoa ya Ruvuma na Lindi na kwamba lengo ni kuhakikisha kuwa mashine hizo zinatolewa katika maeneo yote ambayo yanatekelezwa mradi wa kuvuna msitu.

Emanuel Msoffe ni Mratibu wa Taifa wa mradi wa FORVAC amesema ununuzi wa mashine hiyo ya kisasa umekidhi malengo ya FORVAC ya kuongeza thamani mazao ya misitu.

“Mashine zilizonunuliwa siku za nyuma zilikuwa na kiwango cha asilimia 30 cha kufikia ule ubora unaohitajika,lakini mashine hii imefikia kiwango cha asilimia 63,tunataka kwenda zaidi ya asilimia 80’’,alisisitiza Msoffe.

Kwa mujibu wa Msoffe,takwimu zinaonesha kuwa jumla ya hekta 469,000 za misitu zinapotea kwa mwaka ambapo amesema upoteaji huo pia unachangiwa na utumiaji wa mazao ya mistu usiokuwa sahihi hivyo mashine hiyo ni msaada mkubwa kulinda misitu.

Naye Yusuf Kiangio Mtalaam wa mashine hiyo,amsema mashine hiyo ni kiwanda kidogo kwa kuwa imeweza kutoa ajira kwa vijana waliopo katika kijiji cha Sautimoja hivyo kutekeleza kwa vitendo lengo la serikali ya viwanda. 

Amesema mashine hiyo imeongeza thamani ya mbao na faida kubwa imepatikana katika maeneo ambayo mashine hiyo imetumika Kilwa mkoani Lindi na Tunduru mkoani Ruvuma. 

Amesema mashine ya kuchakata mbao Kilwa imewezesha kijiji kupata milioni 126 ukilinganisha na mapato ya milioni 26 zilizopatikana kabla ya kutumia mashine hiyo.

“Kwa mashine inayotumika katika kijiji cha Sautimoja kwa magogo yenye meta za ujazo 125 kabla ya kutumia mashine hii huwa wanapata shilingi milioni 30,lakini baada ya kuuza mbao zenye ujazo huo kupitia mashine hii wamepata shilingi milioni 90’’,alisema.

Kutokana na matokeo hayo mashine hiyo imekuwa na ufanisi mkubwa katika kuongeza  thamani ya mnyororo wa mazao ya misitu.


Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma

Desemba 6,2020  



No comments: