CHANGAMOTO ZINAZOWAKABILI WENYE UGONJWA WA KISUKARI HADHARANI


Kukosekana kwa dawa za kisukari kwa zaidi ya miezi mitatu sasa licha ya kulipia fedha kila wanapokwenda kliniki na uelewa mdogo kwa baadhi ya watoa huduma kuhusu ugonjwa wa kisukari kumetajwa kuwa moja ya changamoto zinazowakabili wagonjwa wa kisukari.

Aidha, kukosa chakula wanachohitaji kutokana na hali mbaya ya kiuchumi ya familia zao na wazazi kutosindikiza watoto kliniki kumetajwa pia kwamba ni changamoto zinazowasukuma vijana wanaougua kisukari kuingia makundi yasiyofaa hata kuanzisha uhusiano wa kimapenzi wao kwa wao.

Hayo yamebainishwa na watoto na vijana wanaougua ugonjwa wa kisukari, , wakati wa mafunzo kuhusu ugonjwa huo, huku wazazi na walezi wakifundishwa namna kuwatunza vyema wenye kisukari, iliyofanyika katika kliniki ya ugonjwa huo, kwenye Hospitali ya Mkoa wa Temeke, Dar es Salaam leo.

“Tunafika kliniki, tunalipa shilingi 6000, lakini dawa hatupati,” alisema Emmanuel Mbaga, mmoja wa vijana wenye kisukari na kuongeza:

“Ni bora pesa hiyo tungeongezea na kwenda kununua dawa kwenye maduka ya dawa, kwani sisi vijana na watoto wenye aina ya kwanza ya kisukari maisha yetu yanategemea dawa au sindano za kichocheo cha insulin kila siku mara mbili au tatu.”

Hata hivyo alisema, katika maduka, dawa hizo huuzwa kwa kati ya sh.18, 000 hadi Sh. 25,000 kwa dozi ya mwezi, jambo ambalo familia nyingi zenye wagonjwa wa kisukari zinashindwa kumudu kununua.

Kwa upande wake Omari Ahmad (9), alisema: “Kwa sasabu mama anakosa pesa, tunapewa chakula kidogo, pia tunaishi na maumivu kwani kila siku hulazimika kuchoma sindano za kisukari. Sindano zinauma.”

Naye Hamad Mtambo (74) anayeishi Vihanzi Wilaya ya Mkuranga, mkoani Pwani,  aliitaja changamoto nyingine kuwa baadhi ya watoa huduma za afya kutokuwa na elimu sahihi kuhusu kisukari na kukosekana kwa kliniki kwenye baadhi ya hospitali na vituo vya afya hasa vijijini, hivyo kulazimika kuzifuata mbali huduma za kliniki za kisukari na kuomba madaktari waende pia vijijini.

“Sisi tulio vijijini tunapata masmo tofauti, mtoa huduma huyu atakuambia fanya hivi, yule atasema ufanye vile, naona kuna uelewa mdogo kwa baadhi ya watoa huduma, kilini hakuna, wakati mwingine unapewa dawa bila bomba la sindano, unaambiwa hilo bomba ukanunue, tena hadi uwe na la mfano,” alisema.

Meneja mipango wa Chama cha kisukari Tanzania, Happy Nchimbi alisema chama hicho kitaendelea kutoa elimu kwa watoa huduma kuhusu ugonjwa huo ili kuwawezesha kutoa huduma bora zaidi kwa wagonjwa, akiwataka wazazi kuzingatia mafunzo na maelekezo ili kuwalea vyema watoto wenye kisukari.
 
Awali, katika mada yake kuhusu namna ya kuwalea vyema watoto na vijana wenye kisukari, muuguzi kutoka Chama cha Kisukari Tanzania (TDA), Elizabeth Likoko aliwaeleza wazazi na walezi kuwa wagonjwa hao wanahitajika kupata milo sita kutoka makundi matano ya vyakula kwa siku, ambayo ni protini, mbogamboga, matunda,wanga na mafuta kidogo ili kujenga miili na kuwalinda wasiishiwe na sukari mwilini.

Hata hivyo, wakitaja changamoto za malezi ya watoto wenye kisukari, wazazi hao walisema ni jambo gumu kutekeleza hilo kutokana na hali ya uchumi kuwa mbaya, lakini pia wengi wao kukosa elimu ya namna bora ya ulaji kwa wagonjwa wa kisukari hasa watoto na vijana.

“Kwetu wazazi na walezi pia tunachangamoto. Tunashindwa kupata milo sita, kiuchumi ni shida, hatua uwezo.lakini hutokea pia wagonjwa kung’ang’ania aina za vyakula wanavyotaka wao au kutofuata   vijana,” alisema mama Fikirini Tumaini.

Kwa upande wake, Dk. Honesta Kapasika, Mtalam wa ugonjwa Kisukari  wa watoto, alisema ipo changamoto ya upatikanaji wa dawa za kisukari kwa sasa, lakini wahusika wanaifanyia kazi.

Alisema licha ya changamoto hiyo, kuna tatizo la wazazi kutowasindikiza watoto na vijana wao kliniki, hivyo watoto kusema mambo mengi kwa madaktari na watoa huduma badala ya wazazi, akawataka wazazi kuwafuatilia kwa karibu na kuwasaidia watoto wao wenye kisukari.

Baadhi ya wazazi, walezi wa vijana na watoto wenye kisukari wakifuatilia mafunzo ya namna bora ya kuishi na kuwahudumia watoto na vijana wenye ugonjwa huo katika kliniki iliyoandaliwa na Chama cha Kisukari Tanzania (TDA) hospitali ya Mkoa wa Temeke, Dar es Salaam.
Muuguzi kutoka Chama cha Kisukari Tanzania (TDA) Elizabeth Likoko(aliyesimama mbele) akitoa elimu kuhusu ugonjwa wa kisukari kwa watoto na vijana wakati wa kliniki ya kisukari hospitali ya Mkoa wa Temeke, Dar es Salaam.
Muuguzi kutoka Chama cha Kisukari Tanzania (TDA) Elizabeth Likoko(kushoto) akitoa ushauri kwa mwanafunzi wa Chuo cha Afya naSayansi ya Tiba, City College of Health and Allied Science cha Dar es Salaam.
 

No comments: