FATHIYA, BINTI MWENYE VIPAWA, MAPENZI NA KLABU YA SIMBA HADI HADI KUPEWA UBALOZI
UNAPOZUNGUMZIA Soka la Bongo siku zote lazima utazungumzia miamba ya kabumbu, Yanga na Simba. Timu hizi zimejenga ushindani mkubwa katika historia ya mpira wa Tanzania hadi kuitana Watani wa Jadi.
Timu hizi zimeanzishwa zamani sana, walianza Yanga SC mwaka 1935 wakafuata Simba SC iliyoanzishwa mwaka 1936, wote hawa ni wa kongwe! Tanzania kuna timu nyingi zinazoshiriki Ligi Kuu, Daraja la Kwanza na Daraja la Pili bila kusahau daraja la tatu na la nne. Lakini Simba na Yanga ni kongwe zaidi, zilianzishwa zamani sana!.
Historia, hulka, kasumba za ushabiki wa Soka la Bongo, siku zote huwa hivi...yeyote utakaye muuliza Wewe ni mpenzi wa timu gani? Utaambiwa ‘Mimi ni Shabiki wa Simba SC au Mimi Shabiki wa Yanga SC’ na ‘Wengine hujificha kabisa’ licha ya kuwepo timu nyingi kina Azam FC, Mtibwa Sugar, Kagera Sugar, Tanzania Prisons, Gwambina, Ruvu Shooting na nyingine nyingi.
Hivi karibuni Michuzi Media Group waendeshaji wa Blog pendwa Ulimwenguni ya Michuzi Blog na Michuzi Online TV tulibahatika kumtembelea Shuleni kwa, Fathiya Saleh Ramadhan binti mdogo mwenye umri wa miaka Saba, mwenye vipaji lukuki na mwenye mapenzi makubwa na Klabu ya Soka ya Simba ambao ni Mabingwa Watetezi wa Ligi Kuu Soka Tanzania Bara msimu huu. Kwa hakika! tulisikia mengi na kupata vitu vingi kwa binti huyo mwenye vipaji vya ajabu ikiwa kuimba, kucheza na kuzungumza mithiri ya Msemaji wa timu fulani za Soka hapa nchini.
Fathiya anasoma Darasa la Pili (Grade Two) katika Shule ya Kingdom Heritage Model School iliyopo Ukonga, Banana jijini Dar es Salaam, tulizungumza naye vitu vingi kupitia Mahojiano ya Michuzi TV, Pia tulizungumza na Mzazi wake, Mama yake mzazi, Bi. Fatuma Ramadhan, Mwalimu Mkuu sambamba na Mwalimu wake wa Taaluma wa Shule hiyo anayosoma.
KITAALUMA
Fathiya Salehe licha ya vipawa vyake kwenye jamii inayomzunguka na mapenzi yake kwa Simba SC, ametajwa kuongoza Darasani, tena kushika nafasi ya kwanza kati ya Watoto wapatao 50 pale mitihani inapokuja.
Suala hilo la kuongeza wenzake Darasani limethibitishwa na Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Mwl. Charles Nkayi ambaye amesema wamegundua Vipaji vya Fathiya, pia ni Mtoto mzuri ambaye kila muhula anaongoza wenzake, ana jiamini sana kwa vitu anavyofanya katika Masomo na shughuli mbalimbali za Shule.
“Fathiya Saleh ana ‘confidence’ ya hali ya juu hata ukimuangalia unaweza ukadhani ni Mtu mkubwa jinsi anavyoongea, sambamba ukiongea naye unaweza kudhani ametumwa wakati sio kweli, pia kwenye upande wa Kuimba kupaji anacho!”, ameeleza Mwalimu Nkayi.
“Nilikuwa simfahamu kama sasa hivi ninavyo mfahamu, alikuwa hajajitokeza hapa shuleni kama Watoto wengine. Lakini nilivyomuona kwenye Vyombo vya Habari ndio nimemfahamu vizuri na vipaji vyake”, ameeleza Mwalimu Nkayi.
Mwalimu Nkayi amesema pamoja na vipawa vyake lazima Fathiya awezeshwe Kielimu na endapo atawezeshwa kielimu vitu vingine vitafuata na kumsaidia maishani.
Mwalimu wa Taaluma wa Shule hiyo, Denis Magari ameeleza kuwa Fathiya ni Mtoto mzuri darasani toka apokelewe mwaka 2019 akiwa darasa la kwanza, amekuwa akishika namba moja kati ya Watoto zaidi ya 50. Pamoja na vipawa vyake lakini bado yupo vizuri Kitaaluma, ni Mtoto ambaye akiendelezwa vizuri anaweza kuwa Kiongozi Mkubwa Tanzania.
“Ni kweli mimi mwenyewe Shabiki wa Simba SC na kuna siku ile ya mchezo wa Simba na Yanga, nilikuwa natoka kwenye Geti la Uwanja na nikaona Mtoto anafanyiwa mahojiano na Waandishi wa Habari lakini sikutaka kufuatilia sana lile jambo baadae niligundua ni yeye Fathiya alikuwa anafanyiwa Mahojiano na Wana Habari”, ameeleza Mwalimu Magari.
Mwalimu huyo akiwa na Tabasamu na furaha ameeleza “Nilimsikia akielezea Penalti ambayo Yanga SC walipewa akawa anakataa Panelti sio halali, Waandishi wa Habari wakamuuliza kwa sababu gani? akasema kwa akili ya Kitoto alisema Yanga wamepewa Pesa, akawa anaongea vitu fulani ambavyo Waandishi wa Habari waliendelea kumhoji na hapo ndio niliendelea kumfuatilia zaidi na kumfahamu Fathiya.”
“Mimi kama Mwalimu wa Taaluma nilitaka na nitapenda asiishie kwenye shughuli za nje ya Taaluma lakini aendelee kufanya vizuri darasani kama lengo kuu lililomleta shuleni. Tukimuendelea anaweza kuwa Msanii mkubwa hapa nchini au Kiongozi mkubwa kwa sababu yuko vizuri nje ya Taaluma na Darasani kwa ujumla”, ameeleza Mwalimu Magari.
KAULI YA MAMA YAKE MZAZI (MAMA FATHIYA)
Mama mzazi wa Fathiya, Bi. Fatuma Ramadhan ameeleza kuwa ameanza kutambua vipawa vya Mtoto huyo tangu akiwa na umri wa mwaka mmoja na nusu, amesema Fathiya aliweza kuongea mapema kwa kunyoosha maneno. Kwa maana hiyo nilimuona anaelewa kwa haraka ndipo alipolazimika kumpeleka shule akiwa na umri huo.
Bi. Fatuma amesema kwa haraka aliweza kushika Kalamu, kujieleza kwa namna mbalimbali. Hata alipofika umri wa miaka miwili; “Ukimuuliza wewe ni Simba Au Yanga, alijibu Mimi ni Chui, nikagundua kuwa anaelewa Chui ni mnyama na Simba ni mnyama, na alipofika umri wa miaka 4, nilikuwa namuuliza wewe ni Simba au Yanga alisema yeye ni Simba Sports Club”, ameeleza Mama yake Fathiya.
Ameeleza Fathiya alipofika umri wa miaka 5 alianza kwenda Uwanjani na mchezo wake wa kwanza ukiwa Simba SC dhidi ya Kagera Sugar mechi ya kufunga msimu wa mwaka 2017-2018. Mechi hiyo Simba ilipoteza bao 1-0 mbele ya Rais John Pombe Magufuli. Siku hiyo Fathiya alikuwa na hamu kubwa kuonana na Msemaji wa Simba SC, Haji Manara, alikuwa akiuliza “Haji Manara yuko wapi?, This is Simba Brother”.
Mama Fathiya amesema tangu hapo baada ya mechi ya Simba na Kagera ulikuwa utaratibu wa kwenda naye Uwanjani pale Simba SC inapocheza na timu mbalimbali katika Uwanja huo wa Benjamin Mkapa au Uwanja wa Uhuru.
FATHIYA AKIWA MKUBWA UNATAKA AWE NANI?
Mwandishi wa Michuzi Media Group, Janeth Raphael aliuza swali kwa Mama Fathiya, na kujibiwa “Kwa upande wangu nasema anaweza kuwa Msemaji, kaweka vitu vingi vinavyohusiana na Simba SC, amevijua vingi kwa upeo wa hali ya juu kuliko umri wake. Uwezo wa kuongea anao nadhani baadae anaweza kuwa Msemaji lakini naona ana vitu vingi, ‘Dancing’, Kujieleza, hata kufanya vizuri darasani yuko vizuri”, ameeleza Mama Fathiya.
Mapendekezo yangu aje kuwa Kiongozi mkubwa au Kiongozi wa Simba SC au Mwanamke Shupavu ‘Super Woman’.
“Naishauri Jamii, Watoto kuzaliwa na Vipawa ni baraka zake Mwenyezi Mungu, Sisi Wazazi lazima tuwashike mikono, tuwape msukumo zaidi, kwa hiyo lazima tuwashike mikono tuangalie vipaji vyao, Uwezo wao kwa kuangalia M/Mungu amewapa kitu gani”, Mama Fathiya ametoa ushauri kwa Jamii.
BABA YAKE YUKO WAPI?
Mama Fathiya ameeleza kuwa mara nyingi yeye ndio yupo karibu na Mtoto kutokana na shughuli za utafutaji maisha zinazomtinga Baba yake. Ameeleza kuwa huwa anampa taarifa Baba yake kuhusu maendeleo ya Fathiya kila anacho kifanya, katika hali hiyo Baba anafurahishwa na kile anachokifanya Binti huyo.
0713 01 72 90
No comments: