DK CHAULA: TUTUMIE TEHAMA KWA MAENDELEO YA NCHI YETU


KATIBU Mkuu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano sekta ya Mawasiliano, Dk Zainab Chaula amewataka walimu nchini kutokata tamaa ya ufundishaji na badala yake waifanye kazi hiyo kwa moyo mkunjufu huku wakijua wao ni zaidi ya walezi, wazazi wanapokua na wanafunzi mashuleni.

Kauli hiyo ameitoa jijini Dodoma wakati akifunga mafunzo ya Tehama kwa walimu 297 kutoka mikoa yote Nchi nzima ambayo yalitolewa na Taasisi ya Mfuko wa Mawasiliano kwa wote ambapo amesema kwa dunia ilipofikia tehama haiepukiki katika kila eneo la utendaji kazi.

Dk Chaula amewataka walimu hao kutumia mafunzo hayo ya wiki moja waliyoyapata katika kuboresha maisha yao, taaluma zao na kuwa msaada kwa watoto wanaowafundisha huko mashuleni lengo likiwa kuzalisha kizazi chenye uelewa wa tehama.

" Zamani watu tulikua tunamaliza darasa la saba au hata kidato cha sita na hatujui hata kuwasha Kompyuta, sasa hivi serikali inatoa mafunzo kwenu walimu ambayo siyo tu yatawasaidia nyie peke yenu bali yanaenda kuwa msaada kwa wale wanafunzi mliowaacha mashuleni mwenu.

Ombi langu kwenu nendeni mkawape na wengine haya mliyojifunza kwa siku tano hapa, kuna walimu wenzenu hawajapata bahati ya kupata mafunzo haya kwa sababu tusingeweza kuchukua wote lakini kupitia nyinyi na wao wakafaidike, kupitia nyinyi pia wanafunzi wetu wakapate uelewa wa tehama pia," Amesema Dk Chaula.

Dk Chaula amewapongeza walimu hao kwa kumaliza mafunzo hayo salama huku akiwapa changamoto Mfuko wa Mawasiliano kwa wote kuhakikisha awamu ijayo wanafikia kundi kubwa la walimu nchi nzima kwani kwa kasi ya Rais Dk John Magufuli ya kuifanya Tanzania kuwa Nchi ya viwanda ni wazi kila sekta inahitajika kuwa na uelewa wa tehama.

Mafunzo hayo yamefanyika katika Chuo cha Dodoma yakishirikisha walimu 297 ambapo kati yao asilimia 73 wakiwa walimu wanaume na asilimia 15 wakiwa walimu wanawake.

Walimu kutoka mikoa mbalimbali nchini wakimsikiliza Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano sekta ya Mawasiliano, Dk Zainab Chaula wakati akifunga mafunzo ya siku tano ya Tehama kwa walimu hao.
Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano, Dk Zainab Chaula akizungumza na walimu waliohitimu mafunzo ya siku tano ya Tehama jijini Dodoma.
 

No comments: