AMKA TWENDE GOLDEN WOMEN WAKABIDHI KITITA CHA SH. MILIONI 11 KUFANIKISHA UJENZI MATUNDU YA VYOO, BAFU SHULE YA MSINGI SINZA MAALUM
Na Said Mwishehe, Michuzi TV
KAMPUNI ya Open_Kitchen inayosimamia Mradi wa Amka Twende Golden Women ambao umekuwa ukiwezesha wanawake wajasiriamali na wafanyabiashara wadogo imekabidhi hundi ya fedha Sh.milioni 8 na vifaa vya ujenzi vyenye thamani ya Sh.miloni tatu ili kufanikisha ujenzi wa matundu ya vyoo nane pamoja na bafu katika Shule ya Msingi Sinza Maalum iliyopo jijini Dar es Salaam.
Tukio la kukabidhiwa fedha hizo ambazo kwa ujumla ni Sh.milioni 11 kwa maana ya fedha tasilimu na zile za vifaa vya ujenzi limefanyika leo katika ukumbi wa Don Bosco ulioko Oyestabay jijini na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wa maendelo wakiongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa Amka Twende Upendo Mwalongo huku mgeni rasmi akiwa Diwani Mteule wa Kata ya Kijitonyama Dama Lusangija
Pia walikuwepo wajasiriamali wanawake kutoka sehemu mbalimbali za jijini Dar es Salaam na hasa wale ambao kwa namna moja wamekuwa wakishirikiana na taasisi hiyo katika kufanikisha masuala mbalimbali yanayohusu wanawake na kusaidia jamii kwa kutoa michango ya hali na mali.
Akizungumza leo Desemba 6,2020 kabla ya tukio la kukabidhiwa kwa fedha hizo kwa Shule ya Msingi Sinza Maalum, Diwani Mteule wa Kata ya Kijitonyama Dama Lusangija amesema wamekutana leo kwa ajili ya lengo moja tu ya kukabidhi fedha pamoja na vifaa ambavyo kwa ujumla wake ni Sh.milioni 11.
Amesema fedha hizo ambazo zimetolewa na Taasisi ya Amka Twende chini ya Mkurugenzi wake Upendo Mwarongo ambaye amesaidiana na wadau wengine wa maendeleo zinakwenda kutatua baadhi ya changamoto katika shule hiyo hasa kujenga vyoo na mabafu pamoja na uzio ili watoto wanasoma hapo wawe salama.
"Kama mnavyoona shughuli hii imeandaliwa na taasisi ya Amka Twende Golden Women ambayo Mkurugenzi wake ni Upendo Mwarongo , kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo mbalimbali ikiwemo Benki ya NMB na Kampuni ya Coka Cola na wadau wengine.
"Lengo kubwa ilikuwa ni kupata fedha hizo ambazo zimepatikana na leo tunadhikabidhi kwa Shule ya Msingi Sinza maalum ambayo inasomesha watoto wenye mahitaji maalum.Lakini nitumie nafasi hii kumshukuru Rais Dk.John Magufuli kwa kazi kubwa anayofanya ikiwemo ya kuwainua wanawake na hii taasisi ambayo inamilikiwa na wanawake.
"Na wenyewe wanamuunga mkono Rais Magufuli kwa kushiriki katika shughuli za maendeleo katika jamii yetu kwa kusaidia kile ambacho wanaweza ili tu kuwa sehemu ya kutatua changamoto ambazo jamii yetu inakabiliana nazo.Hata hivyo Rais ameendele kuonesha upendo ka akina mama kwa kuendelea kuwapa nafasi kwenye Serikali anayoingoza.
"Ninachosisitiza hapa taasisi hii inamuunga mkono Rais wetu kwa kushirikiana na wadau kuhakikisha baadhi ya kero na changamoto zilizopo kwenye mitaa yetu na taasisi zetu za elimu basi zinapatiwa ufumbuzi.Pia nimshukuru Mkurugenzi Kinondoni kwa kuendelea kuwainua wanawake kupitia mfuko maalum ambao jukumu lake ni kuwawezesha wanawake kwa kuwapatia mikopo,"amesema.
Aidha ametoa mwito kwa wanachi wote kuwa taasisi za aina hiyo ya Amka Twende Golden Women ambazo ni sehemu ya wadau wa maendeleo zianzishwe nyingi zaidi ili kero na changamoto ambazo hazihitaji kuingizwa kenye bajeti ya Serikali ziweze kutatuliwa kwenye ngazi za chini.
Kwa upande wake Mwalongo ambaye ndio Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo ya Amka Twende Golden Women amesema taasisi hiyo imekuwa na programu mbalimbali za kuwasaidia wajasiriamali na wafanyabiashara wadogo wanawake na wamekuwa wakifanya hivyo kwa mwaka wa tatu mfululizo na kwamba wamegusa jamii kubwa ya wanawake kupitia taasisi hiyo.
Hata hivyo kwa mwaka huu waliona kuna haja ya kusaidia Shule ya Msingi Sinza Maalum ambayo inakabiliwa na uhaba wa matundu ya vyoo nane pamoja na mabafu kwa ajili ya watoto wanaosoma hapo ambao wana uhitaji maalum.
"Kiasi cha fedha ambacho kilikuwa kinahitajika katika kufanikisha ujenzi huo wa matundu ya vyoo na mabafu ni Sh.milioni 11, tunashukuru tumekusanya Sh.milioni nane ambazo ni fedha taslimu pamoja na vifaa vyenye vya ujenzi vyenye thamani ya Sh.milioni tatu, hivyo tumepata fedha zote ambazo zinahitajika na kazi iliyobaki ni kuanza kwa ujenzi tu,"amesema Mwalongo.
Amesema kauli mbiu ya kwa mwaka huu inasema Jamii Kwanza ambapo ameifafanua maana yake ni kwamba kokote ambako utafanya kazi jamii ndiyo inayokuzunguka , kwa hiyo wao kama wafanyabiashara , wajasiriamali wanalo jukumu la kuisaidia jamii kwanza.
"Ifahamike hii programu ya kusaidia jamii huu ni mwaka watatu na mwaka huu tuko Wilaya ya Kinondoni lakini mwakani tutakwenda Wilaya nyingine kugusa jamii yenye uhihitaji, mwaka jana tulikuwa Temeke ambako kuna akina mama wajane tuliwasaidia kwa kuhakikisha wananunua kiwanja na kuchimba kisima cha maji ili kujipatia kipato.Mwaka hu tumeamua kusaidia shule hiyo,"amesema Mwalongo.
Akifafanua kuhusu Amka Twende amesema ni programu ambayo ipo chini ya Kampuni ya Upishi ya Open_Kitchen ambayo inasaidia kuwainua wanawake katika biashara na jamii kwa ujumla.
Kuhusu changamoto ambazo wanawake wajasiriamali wanakutana nazo ni kutokuwa na elimu ya kutunza fedha na kuweka akiba ndio maana wakati wa Corona wajasiriamali wengi wanawake wameyumba kiuchumi.
"Tunao NMB ambao wako hapa kwa ajili ya kutoa elimu kwa akina mama ambayo itakuwa msaada mkubwa katika mambo yanayohusu utunzaji fedha na kuweka akiba pamoja na mambo mengine yanayohusu masuala ya fedha na ujasiriamali."
Wakati huo huo Ofisa kutoka Benki ya NMB Salma Chiwanga ametumia nafasi hiyo kufafanua kwa kina namna ambavyo benki hiyo imekuwa karibu na wanawake hasa katika kuwawezesha kutimiza ndoto zao kupitia shughuli wanazozifanya.
"Benki yetu ya NMB imeamua kuwasaidia wajasiriamali wanawake , tunacho kifurushi maalum ambacho kinamlenga wanawake wafanyabiashara wadogo na wale wafanyabiashara endelevu, kwetu sisi NMB kuna mwanamke jasiri na hivyo kuna kifurushi kinachomtosheleza mwanamke jasiri.
"Kifurushi hicho kina huduma za NMB mkononi , huduma za pamoja akaunti, tuna huduma za fanikiwa akaunti na dunduliza.Wajasiriamali na wafanyabiashara wadogo hasa wanawake tunawaambia watumie benki ya NMB kwasababu mpaka sasa benki hiyo imewapa kipaumbele kikubwa sana wafanyabiashara wadogo wadogo na wajasiriamali.
"Ahadi yetu kwa wateja wao ni kwamba mteja wao yoyote atakapokuwa amejiunga na huduma zetu na hasa atapofungua akaunti ataunganisha kwenye klabu ya wanawake ya Amka Twende Women,"amesema.
Wakati huo huo Caroline Damian ambaye ni moja ya wanufaika wa taasisi hiyo, amesema wao wanacho kikudi cha akina mama wajane ambao wanaishi na maambukizi ya HIV ambao wanaendelea na kujishughulisha na shughuli mbalimbali za ujasiriamali baada ya kuwezeshwa na taasisi ya Amka Tendwe.
"Tunamshukuru dada Upendo Mwalongo kwani kabla ya kukutana naye huko nyuma tulikuwa tunafanya biashara ya chakula lakini kwasababu tunaishi na HIV tukawan tunanyanyapaliwa, lakini hivi sasa tunajihusisha na biashara maji kwani tuliwezeshwa , tukanunua kiwanja na kisha kuchimba kisima cha maji, kwa kweli tunamshukuru Mungu kwa kuutunganisha na Upendo ambaye naye amekuwa na wadau wake ambao anatuunganisha nao wakiwemo NMB ambao wametukatia bima za watoto wetu ambao wako chini ya umri wa miaka 18."
No comments: