WANAFUNZI VYUO VIKUU JIJINI ARUSHA WAKABILIWA NA CHANGAMOTO YA MATUMIZI YASIYO SAHIHI YA DAWA ZA NJIA ZA UZAZI WA MPANGO

 Na Pamela Mollel,Michuzi Tv,Arusha

 Wanafunzi wa vyuo vikuu jijini Arusha wanakabiliwa na changamoto ya matumizi yasiyo sahihi juu ya dawa za njia za uzazi wa mpango, hali itakayowasababishia wengi kushindwa kupata ujauzito au kuharibu via vyao vya uzazi

Akizungumza katika mkutano uliowakutanisha wadau mbalimbali wa Vijana pamoja na timu ya afya mkoa wa Arusha ,mratibu wa mipango kwa mkoa wa Arusha kutoka Shirika la JAPAIGO mradi wa TCI Tupange pamoja Bw. Waziri Njau alisema kuwa matatizo ya Afya ya Uzazi kwa vijana bado ni changamoto kubwa hivyo  mkutano huo umewaleta pamoja ili kupata suluhisho la kukabiliana na changamoto hiyo

Alisema kuwa hali katika vyuo vikuu bado ni mbaya kutokana na taarifa mbalimbali walizozipata,na wanafunzi wa ngazi ya Cheti,Stashaha wapo hatarini zaidi kwa kuwa hawana mikopo hali inayopelekea kurubuniwa  na wanafunzi wanaosoma Uzamili na Uzamivu

 Aliongeza kuwa pamoja na Mambo mengine pia mkutano huo utajadili kwa pamoja Unyanyasaji wa Kijinsia,mimba za utotoni, utoaji wa mimba zisizotarajiwana hasa vyuoni

Aidha Bw.Njau aliongeza kuwa elimu sahihi juu ya afya ya uzazi itolewe na Jamii kuondoa dhana potofu kuhusiana na afya ya uzazi kwa ujumla

"Elimu ikitolewa kisahihi itapunguza mimba zisizotarajiwa au zinazotolewa kiholela"alisema Njau.Pia alisema wazazi na walezi wavunje ukimya kwa kuwa na vijana wao karibu ili kujua masuala yao ya afya ya uzazi kwa ujumla

"Wazazi wengi hawapo karibu na watoto wao, majukumu yamewaeka mbali hawawezi kujua chochote kuhusu watoto wao,waache usiri kwenye maswala ya afya ya uzazi"alisema Njau

Naye Mdau wa vijana na maendeleo mkoani Arusha Bi Hellen Mollel alisema kuwa yeye ni muhanga wa mimba za utotoni ambapo amewatoa hofu vijana na kuwataka kupaaza sauti zao kueleza matatizo yao ili kupata suluhu; huku akiwaomba wazazi kuvunja ukimya na kuwaeleza watoto wao athari za ngono zembe.

Aidha mshauri wa wanafunzi chuo kikuu cha Tumaini Makumira Bi Restituta Tilia; alisema wanafunzi wa vyuo vikuu  wanakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo kurubuniwa hivyo amewaomba wazazi kuwaeleza watoto mazingira halisi  watakayoyaishi watakapo kuwa vyuoni

Kwa upande wake mtaalamu wa Afya ya Akili kutoka Idara ya Afya ya Akili katika hospitali ya mkoa Mount Meru Nickson Kataze amesema chanzo kikubwa cha mimba za utotoni kinaanzia kwenye afya ya akili.

Katibu wa Afya katika hospitali ya rufaa Mount Meru Angela Kimati amekiri ofisi yake kupokea kesi nyingi za udhalilishaji dhidi ya watoto; na asilimia 95 ya kesi ni za ulawiti na ubakaji.

Akifungua mkutano huo  kwa niaba ya Mganga mkuu wa mkoa wa Arusha; afisa afya ambaye pia ni mdau wa masuala ya afya ya uzazi Isaya Nangai ameshauri mradi wa TCI Tupange Pamoja uchukue hatua madhubuti ili kuweza kufufua huduma za afya ya uzazi kwa vijana kwa kuwafikia wale wa umri mdogo kuanzia miaka 14 ambao wamejiingiza katika Ngono ya wavulana.

Mratibu wa mipango Mkoa wa Arusha kutoka Shirika la JAPAIGO mradi wa TCI Tupange pamoja Bw.Waziri Njau akiongea na vyombo vya habari kuhusu mkutano uliowakutanisha wadau mbalimbali wa afya hivi karibuni jijini Arusha
Msimamizi wa kituo cha Biashara zinazochipukia kilichopo Chuo Cha Uhasibu Arusha ambaye pia ni mdau wa afya Bi.Pamela Chogo akizungumza katika mkutano huo
Mgeni rasmi kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Mkoa Arusha,Afisa afya ambaye pia ni mdau wa masuala ya afya akifungua mkutano huo jijin Arusha
Katibu wa afya Mkoa hospital ya rufaa ya mt.meru Angela Kimati akizungumza na vyombo vya habari
Mshauri wa wanafunzi Chuo cha Tumaini Restituta Tilia akiongea na vyombo vya habari
Mdau wa afya Hellen Mollel akizungumza na vyombo vya habari
Mtaalamu wa afya ya akili kutoka idara ya afya ya akili katika hospital ya mt.meru akiongea na vyombo vya habari
Profesa Ole Nguyaine akizungumza katika mkutano huo ambapo amewataka wazazi kupunguza ukali kwa watoto wao ili waweze kuwa karibu na itasaidia kujua tabia za watoto wao
Picha ya pamoja
 

No comments: