SERIKALI KUCHUNGUZA WALIOHUSIKA NA UDANGANYIFU WA MITIHANI YA DARASA LA SABA
KATIBU Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhandisi Joseph Nyamhanga amesema serikali imeanza kuwachunguza waliohusika katika udanganyifu wakati wa mtihani wa darasa la saba 2020 na kuwa yeyote atakayebainika atachukuliwa hatua kali.
Ameyasema hayo leo wakati akitoa tathimini ya matokeo ya darasa la saba mwaka 2020 kwa vyombo vya habari, kwenye Ofisi za TAMISEMI Mtumba Jijini Dodoma
Mhandisi Nyamhanga amesema Ofisi ya Rais-TAMISEMI inalaani vikali tabia ya udanganyifu na ukiukwaji tararibu za ufanyaji mitihani na kuwa tayari wameanza uchunguzi wa suala hilo utakaofanyika kwa wiki moja.
Amefafanua kuwa endapo kuna mtumishi wa serikali au sekta binafasi atabainika kuhusika kwa namna moja au nyingine katika udanganyifu Serikali itachukua hatua kali za kinidhamu na kisheria.
“ Kumekuwa na tabia ya mara kwa mara kwa baadhi ya shule, wanafunzi, walimu na wasimamizi wa mitihani kukiuka taratibu za ufanyikaji na uendeshaji wa mitihani ya kitaifa, tunaalani vikali tabia hiyo na uchunguzi unaendelea.”Amesisitiza Mhandisi Nyamhanga
Amesema atakayebainika atachukuliwa hatua za kinidhamu na kisheria ili iwe fundisho kwa watu wenye tabia hiyo, kwa kuwa udanganyifu huu umesababisha wanafunzi 1,059 kufutiwa matokeo na unakatisha ndoto na malengo ya vijana wetu ambao wangekuwa wataalamu wa fani mbalimbali kwa miaka ijayo.
Kwa mujibu wa taarifa ya Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA), limewafutia matokeo wanafunzi 1,059 kutoka shule 38 kutokana na tuhuma za udanganyifu wa mitihani.
Aidha, Jumla ya watainiwa 1,009, 586 walifanya mtihani ya kumaliza Elimu ya Msingi kati ya hao watahiniwa 833,672 wamefaulu ikiwa ni asilimia 82.68 ikiwa ni ingezeko la asilimia 1.18 kutoka ufaulu wa asilimia 81.50 mwaka 2019.
Hata hivyo kwa mwaka huu, watahini 14,364 sawa na asilimia 1.4 ya waliosajiliwa hawakufanya mtihani kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo utoro na ugonjwa.
Aidha, Mhandisi Nyamhanga amesema kuwa mafanikio haya yanatokana na juhudi za Serikali, wananchi, wadau wa maendeleo, ukarabati wa miundombinu ya shule, utoaji wa elimumsingi bila malipo, ununuzi na usambazaji wa vifaa vya kujifunza na kufundishia na mafunzo ya mara kwa mara ya walimu kazini.
No comments: