WABUNGE WAMTHIBITISHA MAJALIWA KUWA WAZIRI MKUU

*Apata asilimia 100 ya kura zote 350 zilizopigwa
*Amshukuru Rais na aahidi kuendelea kufanya kazi kwa bidii

SPIKA wa Bunge la 12 Job Ndugai amesema wabunge wamemthibitisha mbunge wa jimbo la Ruangwa mkoani Lindi, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa kuwa Waziri Mkuu kwa miaka mitano mingine (2020-2025) kwa kupata kura zote 350 zilizopigwa na wabunge sawa na asilimia 100.

“Kura zote zilizopigwa ni 350 hakuna iliyoharibika, hakuna kura ya hapana. Kura zote 350 zimemthibitisha Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, kwa hiyo ndugu wabunge Mheshimiwa Majaliwa amethibitishwa na Bunge hili kuwa Waziri Mkuu kwa kura 350 sawa na asilimia 100.”

Spika Ndugai ameyasema hayo leo (Alhamisi, Novemba 12, 2020) Bungeni jijini Dodoma baada ya kupokea jina la Waziri Mkuu lililowasilishwa bungeni na Mpambe wa Rais na kisha wabunge kupiga kura kwa ajili ya kulithibitisha jina hilo.

Akizungumza baada ya kuthibitishwa Mheshimiwa Majaliwa amesema amepokea uteuzi huo kwa mikono miwili na anamshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ameendelea kuwapa uhai wote na kushuhudia hayo, Pia ametumia fursa hiyo kumshukuru Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa imani kubwa aliyoionesha juu yake.

“Mheshimiwa spika naomba nitumie nafasi hii kwa dhati yangu ya moyo kumshukuru sana Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ushindi mkubwa alioupata kutoka kwa Watanzania kupitia uchaguzi ambao ulifanyika hivi karibuni kwa kushinda kwa kishindo. Uchaguzi uliofanyika kwa uhuru na haki.”

“Jambo hili si dogo, Mwenyezi Mungu ameliongoza, namshukuru Mheshimiwa Rais Dkt John Pombe Magufuli kwa imani kubwa aliyonayo juu yangu na kuendelea kuniamini. Namshukuru sana na Makamu wa Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa ushiriki wake katika kuridhia jina langu.”

“Pia, nampongeza Makamu wa Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa ushindi mkubwa alioupata katika uchaguzi huo na namna ambavyo Watanzania wameridhishwa na kazi aliyoifanya na imani waliyonayo kwamba viongozi hao wataendelea kuwatumikia vizuri zaidi.”

Ametumia fursa hiyo kumpongeza Spika wa Bunge Job Ndugai kwa kuchaguliwa bila kupingwa kuwa mbunge wa Kongwa pamoja na kurudi katika nafasi yake ya uspika baada ya kupigiwa kura nyingi na waheshimiwa wabunge, hakuna siri kwamba umefanya kazi nzuri miaka mitano iliyopita umeisaidia sana serikali na kuiwezesha kufanya mambo makubwa.

“Kazi uliyoifanya miaka mitano iliyopita tunaifahamu vizuri zaidi na Serikali itaendelea kukupa ushirikiano wa dhati. “Mheshimiwa spika niendelee kushukuru kwa kuwashukuru wabunge wenzangu, waheshimiwa wabunge wenzangu mmenifanyia jambo kubwa kwangu na familia yangu.”

“…idadi ya kura zenu mlizonipigia mmenipa changamoto sana. Haijawahi kutokea mmepiga kura kwa asilimia 100, haijawahi kutokea nawashukuru sana. Nitaendelea kushirikiana na wabunge wenzangu wote nikijua nyie ni wawakilishi wa Watanzania wanaotamani kupata maendeleo kupitia uwakilishi wenu. ”

Pia, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwashukuru wananchi wa jimbo la Ruangwa na mkoa wa Lindi, familia na CCM kwa ushirikiano alioupata katika kutekeleza majukumu yake katika kipindi cha miaka mitano na anaimani wataendelea kumpa ushirikiano katika kipindi cha miaka mitano mingine.

Awali, kabla ya kuthibitisha jina la Waziri Mkuu wabunge mbalimbali walizungumzia utendaji kazi wa Mheshimwa Majaliwa ambapo Mbunge wa Tunduma David Silinde alitumia fursa hiyo kumpongeza Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kumrudisha tena Waziri Mkuu Kassim Majaliwa katika nafasi hiyo.

Amesema kuwa Waziri Mkuu Majaliwa ni kiongozi mwenye uwezo wa kusimamia maono ya Rais Dkt. Magufuli katika kuibadilisha nchi na pia anauwezo wa kuunganisha nchi yote kupitia Bunge na hivyo kufanya kazi ya rais kuwa nyepesi.

“Sifa kuu ya kiongozi ni unyenyekevu, kujishusha na kusikiliza na sifa hizo Mheshimiwa Majaliwa anazo, ninaamini wote tutampitisha kwa asilimia 100 ili kuliambia Taifa nini tunakwenda kukifanya kwa miaka mitano baada ya miaka mitano ya mafanikio ambayo imeleta ushindi wa kimbunga.”

Amesema anaamini kwamba katika kipindi cha miaka mitano Serikali inakwenda kufanya mabadiliko makubwa katika Taifa na dunia inajua kuwa viongozi wao ni mahiri na kila mahali wanatetemeka kusikia kazi inayofanywa na viongozi hao.

“Naomba wote tumpitishe ili aweze kuongoza tena.”

Naye, Mbunge wa Ismani, William Lukuvi amesema Mheshimiwa Majaliwa ni binadamu mwenye upendo, mchapakazi asiyekuwa na majivuno na kwa mara ya kwanza ameshuhudia Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM akizunguka kwenda kuwatetea wabunge nchi nzima. “Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli ametutendea haki Watanzania Mheshimiwa Majaliwa anatosha sana kuwa Waziri Mkuu.”

Kwa upande wake, Kapten Mstaafu George Mkuchika amesema Mheshimiwa Majaliwa anamfahamu vizuri na amewahi kufanya kazi wakiwa Ofisi ya Rais –TAMISEMI kwamba ni mtu mstarabu kama Mheshimiwa Majaliwa ni mtu msikivu, asiyejikweza na hajipendekezi anatenda haki kwa kila mtu.

“Katika kipindi cha miaka mitano hakubagua wabunge katika uetekelezaji wa shughuli za bunge na ni mtu msikivu sana. Amesimamia sana katika kufufua uchumi hasa mazao ya biashara, amerejesha mamlaka ya mkonge mikononi mwa Serikali. Ameratibu vizuri shughuli za wizara zote.”

Naye, Mama Salma Kikwete Alisema Mheshimiwa Majaliwa hakuwa mbaguzi katika kipindi cha miaka mitano iliyopita na amefanya mambo makubwa, hivyo anampongeza Rais Dkt. Magufuli kwa kuwarejeshea kwani anastahiki kuwa Waziri Mkuu na hakuna anayeweza kupinga jambo hilo.

Mbunge mwingine, Fakharia Shomari alisema anamshukuru Rais Dkt. Magufuli kwa uteuzi alioufanya katika nafasi ya Waziri Mkuu kwa sababu ni uteuzi ambao walikuwa wanaufikiria ila hawakuweza kuamua kabla ya yeye kutamka. “Mheshimiwa Majaliwa amefanya ziara nchi nzima na alikuwa anafanya kazi na kila rika na jamii. “Nawaomba wabunge wenzangu tuibariki hoja ya mheshimiwa Rais.”

Kwa upande wake, Mbunge wa Bumbuli, Januari Makamba alisema Mheshimiwa Majaliwa ni kiongozi msikivu, muadilifu, mnyenyekevu, hodari, mchapakazi na ni kiongozi shupavu ambaye nafasi hiyo anaimudu na anaiweza na hakuna shaka yoyote kwamba nafasi hiyo kwamba ataitendea haki. “Kumpigia kura nyingi tunaonesha imani kwa ndugu yetu na imani na busara kwa rais.”
Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakimpongeza Waziri Mkuu Mteule na Mbunge wa Ruangwa Kassim Majaliwa baada ya Spika wa Bunge Job Ndugai kusoma jina lake baada ya kupendekezwa kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais Dkt. John Pombe Magufuli, Bungeni Jijini Dodoma, Novemba 12, 2020.

Baadhi ya wabunge wa wakimpongeza Kassim Majaliwa baada ya jina lake kupendekezwa na Rais Dkt.Magufuli kushika nafasi ya Uwaziri Mkuu.

Spika wa bunge Job Ndugai akipokea karatasi yenye jina la kupendekezwa kwa Waziri Mkuu wa Tanzania kutoka kwa Mpambe wa Rais .

Spika wa bunge la Jamhuri ya Muungano Tanzania Job Ndugai akionyesha karatasi yenye jina la kupendekezwa kwa Waziri Mkuu baada ya kupokea kutoka kwa mpambe wa Rais
Spika wa bunge Job Ndugai akisaini karatasi yenye jina la kumpendekeza Waziri Mkuu wa Tanzania baada ya kukabidhiwa na Mpambe wa Rais

No comments: