VYAMA VYA MSINGI WILAYANI NAMTUMBO WASHANGAA KUTOFANYIKA KWA UCHAGUZI CHAMA KIKUU
Na Yeremias Ngerangera…Namtumbo.
VYAMA vya msingi wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma vimelalamikia kuchelewa kwa uchaguzi chama kikuu cha ushirika (union) kwa zaidi ya miezi mitano toka kumaliza kwa uchaguzi wa viongozi wa vyama vya msingi.
Wakizungumza katika kikao kazi katika ukumbi wa Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo viongozi wa vyama hao walisema wanashangaa kwa nini uchaguzi wa chama kikuu (UNION) haufanyiki na hivi sasa ni zaidi ya miezi mitano imepita toka kumalizika kwa uchaguzi wa vyama vya msingi.
“Kikanuni mrajisi wa vyama vya ushirika amepewa uwezo wa kuvunja bodi iliyomaliza muda wake na kuweka bodi ya muda kutoka kwa wajumbe wapya waliochaguliwa kwenye vyama vya msingi huku tukisubiria uchaguzi, lakini tunashangaa kuendelea kufanya nao kazi viongozi ambao wanajua muda wao umekwisha kuna nini hapo?” Alisema bwana Hassani Darajani mwenyekiti wa chama cha msingi Mgombasi.
Aidha walitahadharisha kuwa ikitokea ubadirifu wa mali za wanaushirika zigo hilo atabebeshwa mrajisi wa vyama vya ushirika mkoa wa Ruvuma kwa kuwa yeye ndiye aliyepewa dhamana ya kuvunja bodi iliyomaliza muda wake na kuweka bodi mpya kutoka kwa wajumbe wapya waliochaguliwa kwenye vyama vya msingi.
Jafari Gunda kwa upande wake alidai wanahitaji uchaguzi wa chama kikuu ufanyike haraka kwa kuwa kuna dalili za vyama vya msingi kukopeshwa pembejeo zaidi ya makisio ya vyama vya msingi na hiyo ni hatari kwa ustawi wa vyama vya msingi kwa kuwa wanaongezewa mzigo tofauti na makisio yao.
Afisa ushirika wa wilaya ya Namtumbo bwana Emmanuel Gwao pamoja na kuwashukuru viongozi wa vyama vya msingi kwa kusimamia vyema ununuzi wa mazao kwa njia ya stakabadhi ghalani aliwataka kujipanga upya katika kujiandaa kununua mazao katika msimu ujao wa kilimo.
Bwana Gwao aliwataka viongozi hao pia kuvuta subira kwani uchaguzi wa chama kikuu upo mbioni kufanyika hivyo waondoe hofu kwa kuwa serikali ipo inasimamia, hakuna kitu kitakachoharibika alisema bwana Gwao.
Wilaya ya Namtumbo inajumla ya kata 21 zilizobahitika kupata ardhi nzuri yenye rutuba inayokubali mazao ya chakula na biashara na katika kata hizo kuna jumla ya vyama vya msingi 44 ambapo kata 19 zina vyama vya msingi 2 na kata mbili zina vyama vya msingi vitatu.
No comments: