TARURA YADHAMIRIA KUUNGANISHA WILAYA YA RUANGWA NA LIWALE
Ujenzi wa Daraja la Mto Mbwemkuru lenye urefu wa Mita 75 lililopo
Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi linalojengwa na Wakala
wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) ukiwa unaendelea. Daraja
hili ni mpango wa kuunganisha Wilaya ya Ruangwa na Wilaya ya Liwale
kwa lengo la kurahisisha shughuli za kiuchumi kwa wananchi wa maeneo
hayo.
Ujenzi wa Daraja la Mto Mbwemkuru lenye urefu wa Mita 75 lililopo
Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi linalojengwa na Wakala
wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) ukiwa unaendelea. Daraja
hili ni mpango wa kuunganisha Wilaya ya Ruangwa na Wilaya ya Liwale
kwa lengo la kurahisisha shughuli za kiuchumi kwa wananchi wa maeneo
hayo.
Na Bebi Kapenya, Lindi
WAKALA wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), umeendelea
kuboresha miundombinu ya barabara na madaraja katika Halmashauri ya
Wilaya ya Ruangwa Mkoa wa Lindi ikiwemo ujenzi wa daraja la Mto
Mbwemkuru lenye urefu wa mita 75 linalojengwa katika barabara ya
Chikwale hadi Liwale kwa gharama ya Shilingi Bilioni 4.5.
Meneja wa TARURA Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, Mhandisi Mashaka
Nalupi alisema mradi wa ujenzi wa daraja la Mto Mbwemkuru umetokana na
mpango wa kuunganisha Wilaya ya Ruangwa na Wilaya ya Liwale kwa lengo
la kurahisisha mawasiliano kwa wananchi wa maeneo hayo na kuwezesha
shughuli zao za kiuchumi na kijamii kwa haraka.
“Wilaya hizi mbili ni maarufu sana katika kilimo cha korosho na ufuta,
lakini pia wananchi wa vijiji vya Nangurugai, Mirui, Narungombe,
Machang’anja na Chikwale watapata faida ya kiuchumi kwasababu mazao
yao ya biashara yataweza kuvushwa kutoka upande wa Liwale kwenda
Ruangwa ambapo kuna soko kubwa la mazao ya biashara pale Ruangwa
mjini”, alisema Meneja huyo.
Mhandisi Nalupi ameeleza kuwa hadi sasa TARURA Halmashauri ya Wilaya
ya Ruangwa imeshapokea fedha Shilingi Bilioni 1.6 kwa ajili ya ujenzi
wa daraja la Mto Mbwemkuru na ujenzi utakuwa wa Awamu II ambapo Awamu ya kwanz itakuwa ujenzi wa daraja lenyewe kwa kutumia Mkandarasi anayeitwa Nyumbani Construction Company Limited kwa mkataba wa Bilioni 1.6 na Awamu ya pili itakuwa ni ujenzi wa Makalavati makubwa upande wa Liwale kwa Mkandarasi anayeitwa Lumo Cones ambaye ameshaingia mkataba na ujenzi unatarajia kuanza hivi karibuni.
Naye, Bw. Abdallah Nampundai Mkazi wa Ruangwa ameishukuru Serikali kwa
ujenzi wa daraja hilo kwani utanufaisha wananchi kusafirisha mazao yao
na kufanya biashara zao.
“Kwa sisi wafanyabiashara na wakulima tunatoa mazao yetu kutoka
Ruangwa kupeleka Liwale na tunatoa Liwale kupeleka Kilwa hivyo
kukamilika kwa daraja hili kutatusaidia sana kupitisha mazao yetu kwa
urahisi.” amesema Bw. Nampundai.
Kwa upande wake, Bw. Leonard Abel Mkazi wa Kijiji cha Nangurugai
ameishukuru TARURA kwa ujenzi wa daraja hilo kwani litakapokamilika
litarahisisha usafiri kwasababu wanapata changamoto nyingi mvua
ikinyesha ikiwemo kupoteza ndugu zao kwavile Mto huo una mamba wengi
hasa kipindi cha mvua hivyo kukamilika kwake kutawasadia sana kwenye
suala la usafiri.
Mbali na ujenzi daraja la mto Mbwemkuru, TARURA Halmashauri ya Wilaya
ya Ruangwa imekamilisha ujenzi wa Barabara za Lami Ruangwa mjini jumla
ya Kilomita 8.32 kwa fedha za Mfuko wa Barabara pamoja na fedha za
mradi wa Mfuko wa Umoja wa Ulaya, pia wameweka taa za barabarani jumla
ya Km 7.62 mradi uliofadhiliwa na REA (Wakala wa Umeme Vijijini).
Aidha, Meneja huyo alisema kuwa wameweza kuunganisha sehemu kubwa ya
Mji wa Ruangwa kwa barabara za Lami ambapo imeweza kurahisisha
mawasiliano kwa watumiaji wa barabara na kuimarisha shughuli za
kiuchumi kwa wananchi wa maeneo hayo kwavile biashara zimeendelea
kufanyika hadi nyakati za usiku kwasababu ya uwepo wa taa za
barabarani.
TARURA Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa inaendelea na kazi mbalimbali
za kuboresha miundombinu ya barabara na madaraja ili kuboresha
upatikanaji wa huduma za kijamii na kiuchumi kwa urahisi.
No comments: