MFUMO WA N-CARD WAONGEZA UKUSANYAJI MAPATO UWANJA WA BENJAMIN MKAPA


Na Shamimu Nyaki - WHUSM, Morogoro

MFUMO wa kisasa wa N-Card unaotumika katika kutoa tiketi Uwanja wa Benjamin Mkapa umesaidia kuboresha ukusanyaji wa mapato katika Uwanja huo.

Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi ameyasema hayo Novemba 28, 2020 mkoani Morogoro wakati akifungua kikao cha Baraza la Wafanyakazi Wizara hiyo.

Akifafanua kuhusu uboreshaji mifumo ya ukusanyaji wa mapato katika uwanja huo, Dkt. Abbasi ametolea mfano baadhi ya mechi zilizochezwa uwanjani hapo kabla ya mfumo kutumika mwaka 2019 na baada ya Mfumo wa N-Card kutumika mwaka 2020.

''Mwaka 2019 mechi ya Simba na Biashara United tulikusanya takriban milioni 19.05 , lakini mwaka 2020 baada ya kuanza kutumia mfumo huo wa kisasa wa kukusanya mapato katika mechi ya timu hizo tulikusanya milioni 44.720.'' amesema Dkt. Abbasi.

Ameongeza kuwa mwaka 2019 Mechi kati ya Yanga na Coastal Union kiasi cha takribani shilingi milioni 18 kilikusanywa ambapo mechi kama hiyo iliyochezwa mwaka 2020 ilikusanyamillioni 45.

Vile vile, mechi kati ya Yanga na Namungo mwaka 2019 kiasi cha shilingi milioni saba kilikusanywa lakini mfumo wa N-Card umesaidia mapato kuongezeka ambapo mwaka 2020 mechi hiyo imekusanya takriban milioni zaidi ya 30.

Kutokana na mafanikio hayo katika ukusanyaji wa mapato kupitia mifumo ya kisasa, Katibu Mkuu Dkt. Abbasi ameziagiza Taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo kuanza kutumia mifumo mbalimbali kukusanya mapato.

Aidha, Dkt. Abbasi amesema kuwa Wizara yake imepata mafanikio kufuatia maboresho yaliyofanywa katika Bajeti ambapo ameeleza kuwa kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021, bajeti ilipata ongezeko la takriban shilingi bilioni tisa.

Mafanikio mengine ambayo Dkt. Abbasi alieleza kuwa ni pamoja na kuiboresha Kampuni ya Magazeti ya Serikalini (TSN.)

Kwa upande mwingine, Dkt. Abbasi amesema kuwa maamuzi yaliyofanywa na Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuihamisha COSOTA kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara kuja katika Wizara yake matokeo yameanza kuonekana ikiwemo kuboresha kanuni za COSOTA ili wadau wa Sekta ya Sanaa wanufaikemabadiliko chanya.

Katika Sekta ya Michezo, Dkt. Abbasi ameeleza kuwa sekta hiyo ni nyeti katika kuendeleza michezo, hivyo mashirikisho na Vyama vya Michezo lazima yaonyeshe mpango mkakati wa kuendeleza michezo huku akisistiza kuwa Timu ya Taifa ni ya nchi hivyo Serikali lazima ishiriki kwa hatua zote za maandalizi ya timu hiyo ndani na nje ya nchi.

Dkt. Abbasi ameeleza kuwa Wizara tayari imeanza kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Mwaka 2020 katika maeneo yanayowahusu ikiwemo maandalizi ya kuzindua Bodi ya Mfuko wa Sanaa ambao utakuwa na mchango mkubwa wa kuleta mageuzi katika sekta hiyo ikiwemokutoa elimu pamoja na mikopo kwa wasanii.

Katika upande wa kuimarisha utendaji kazi na kuongeza ari na morali ya kufanya kazi, Dkt. Abbasi ameeleza kuwa Wizara imefanya mabadiliko makubwa ikiwemo kuongeza vitendea kazi na kuboresha mazingira ya kufanyia kazi.

Naye Mwenyekiti wa TUGHE Wizara, Bw. Mfaume Said amemshukuru mwenyekiti huyo ambaye ni Katibu Mkuu kwa juhudi zake za kuboresha mazingira ya kufanyia kazi, maslahi ya watumishi pamoja na ushirikishwaji wa watumishi katika masuala mbalimbali yanayohusu utumishi ndani ya Wizara.

Naye Mwakilishi wa TUGHE Mkoa wa Dodoma, Bw. Msubishi Mwasandende amesema Wizara hiyo imefanya mabadiliko makubwa ambayo yameimarisha ari ya wafanyakazi katika kutekekeza majukumu yao.

Kikao hicho cha Baraza kinafanyika Novemba 28 hadi 29, 2020 ambacho pamoja na mambo mengine mada mbalimbali ziliwasilishwa ikiwemo Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Mwaka 2020 - 2025.

No comments: