SPIKA NDUGAI ATAMANI BUNGE 'LIVE', "HAKUTOKUA NA KAMBI RASMI YA UPINZANI"


Charles James, Michuzi TV

MUDA mfupi baada ya Spika wa Bunge, Job Ndugai kuapa, ameeleza matamanio yake ya kuwaona wabunge wakionekana wakichangia ndani ya Bunge huku pia akieleza kutokuepo kwa kambi rasmi ya upinzani.

Akizungumza baada ya kuapishwa, Spika Ndugai amesema ni matamanio yake kuona wabunge wakionekana wakichangia huku akieleza kuwa anaamini kwa sababu serikali ni sikivu italichukua na kulifanyia kazi ombi hilo.

Kwa upande mwingine, Spika Ndugai amesema Bunge hili halitokua na kambi rasmi ya upinzani kwa sababu wabunge wa upinzani hawajafikia asilimia 12 ya wabunge wote kama inavyotakiwa.

Aidha Spika Ndugai amewataka wabunge wote kufanya kazi kwa bidii katika kuwatumikia watanzania na kuisimamia serikali pamoja na kuishauri lakini pia akiwasihi kutokubali kukopeshana.

" Hili la kukopeshana sikupaswa kulisema lakini nimeona niliseme, usikubali kumkopesha mtu, Bunge lililopita tulipata tabu sana na ishu za wabunge kukopeshana, niwashauri usimkopeshe mtu na mkikopeshana basi mimi sipo," Amesema Spika Ndugai.



Spika wa Bunge, Job Ndugai akizungumza na Wabunge mara baada ya kuchaguliwa kuliongoza Bunge hilo kwa kipindi kingine.

Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini CCM, Anthony Mavunde akila kiapo cha uaminifu mbele ya Spika wa Bunge, Job Ndugai.
 

No comments: