DKT. ABBAS AWATOLEA UVIVU CHADEMA BBC, APANGUA HOJA
Msemaji Mkuu wa Serikali ya Tanzania, Dkt. Hassan Abbasi ameliambia Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) kuwa Watanzania wamemaliza uchaguzi na sasa wanaendelea na michakato ya kidemokrasia, kisheria na kikatiba ya kujenga taasisi za nchi ili kazi iendelee na kamwe hawapotezi muda na kile alichokiita "maigizo" ya baadhi ya viongozi wa upinzani hasa Chadema.
"Hivi ninavyoongea na wewe mchakato unaofuata ni Bunge kuanza, watachagua Spika, watapelekewa Jina la Waziri Mkuu kumthibitisha na kisha Rais atazindua Bunge," hao walioshindwa uchaguzi na kuanza tuhuma ni maigizo yao ambayo tumeyazoea kila mara wanaposhindwa.
Akijibu mahsusi madai ya baadhi ya viongozi wa Chadema kama Tundu Lissu na Godbless Lema kuhofia usalama wao na hata kujaribu kuomba hifadhi ya ukimbizi nje ya nchi Dkt. Abbasi alishangazwa na madai hayo na kuhoji wametishiwa usalama wao na nani, wapi na lini?
"Mkataba wa Kimataifa wa Mwaka 1951 unaohusu Haki na Hadhi za Wakimbizi kwa mfano unaainisha bayana taratibu za kuwa mkimbizi, huwezi kuamka asubuhi tu ukajitangaza wewe ni mkimbizi au una kesi ya jinai ukataka kukimbia nchi kisa kudai ukimbizi.
"Mtu anaibuka anadai ametishiwa maisha lakini juzi tu katoka kushiriki kampeni siku 60 na amelindwa salama kabisa leo kashindwa anakwambia anahofia maisha. Mkimbizi gani anavuka mpaka mbele kaandaliwa gari ya kumchukua? Haya ni maigizo," alisema Dkt. Abbasi.
Amesisitiza kuwa Serikali ya Tanzania itaendelea kuenzi misingi ya amani na kuwataka Watanzania kuendelea kuchapa kazi, anayehofu usalama wake atoe taarifa kwenye vyombo vya dola na amewataka wananchi kuachana na maneno ya watu waliokosa kuaminiwa na umma sasa wanatafuta kuonewa huruma.
Msemaji Mkuu wa Serikali ya Tanzania, Dkt. Hassan Abbasi
No comments: