SERIKALI IWAANGALIE WAHITIMU SHULE BINAFSI KATIKA UTOAJI WA MIKOPO- DKT. RWAKATARE

Mkurugenzi wa shule za St. Mary's Dkt.Rose Rwakatare akizungumza na waandishi wa habari wakati wa mahafali ya 19 ya shule hiyo ambapo ameiomba Serikali kuwaangalia wanafunzi wanaohitimu masomo yao katika shule binafsi katika suala zima la utoaji wa mikopo ya elimu ya juu, jijini Dar es Salaam.Mkuu wa Chuo kikuu kishiriki cha elimu Mkwawa (MUCE) Prof. Ester Dungumaro Akizungumza mwishoni mwa wiki wakati wa mahafali ya 19 ya shule ya St. Mary's na kuwataka wahitimu kuwa na maadili mema na Uzalendo kwa taifa, jijini Dar es Salaam.

Wanafunzi wa St.Mary's wakitoa burudani.Walimu wa shule ya St.Mary's Mbezi juu jijini Dar es Salaam wakiwa katika picha ya pamoja katika mahafali ya 19 ya shule hiyo.Baadhi ya wazazi waliohudhuria mahafali hayo yaliyofanyika mwishoni mwa wiki Mbezi juu jijini Dar es Salaam.

    Na Leandra Gabriel, Michuzi TV
    MKURUGENZI wa shule za St. Mary's, Dkt. Rose Rwakatare ameiomba Serikali kuwaangalia wanafunzi waosoma shule binafsi katika suala la utoaji wa mikopo ya elimu ya juu kwa kuwa sio kila mwanafunzi anayesoma katika shule hizo anauwezo wa kukidhi gharama za masomo katika ngazi zote za elimu.

    Akizungumza katika mahafali ya 19 ya kidato cha nne ya shule ya St.Mary's Mbezi juu jijini Dar es Salaam Dkt. Rose amesema kuwa Serikali imekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha watoto wanapata elimu bora na itakayoweza kuwakomboa.

    "Tunaishukuru sana Serikali kwa kuendelea kutuamini na kushirikiana nasi katika kuhakikisha vijana wetu wanapata elimu bora, tunaiomba pia iwaangalie wanafunzi wanaohitimu masomo yao katika shule binafsi katika suala zima la utoaji wa mikopo ya elimu ya juu...si kila anayesoma katika shule hizi anauwezo kuna wanaopata ufadhili na baadaye ukakoma tunaiomba Serikali kupitia bodi ya mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu kusaidia hili." Ameeleza.

    Pia amesema kuwa Taasisi hiyo imeendelea kutoa elimu ambayo imezalisha matunda bora zaidi na hiyo ni kutokana na juhudi za walimu na wazazi ambao wamekuwa wakionesha ushirikiano pindi wanapohitajika.

    "Niwahakikishie wazazi kuwa mmewekeza katika jambo muhimu sana kwa vijana hawa...mtegemee matunda bora kutoka kwao." Amesema.

    Aidha amesema kuwa wakielekea kufanya mtihani wao wa taifa utakaoanza Novemba 23, tayari walimu na watahiniwa hao wamejiandaa na wapo tayari kufanya mtihani huo.

    Kwa upande wake Mkuu wa Chuo kikuu kishiriki cha elimu Mkwawa (MUCE,) na mgeni rasmi wa mahafali hiyo Prof. Ester Dungumaro amesema kuwa mchango wa Serikali katika kuhakikisha vijana wanapata elimu bora ni mkubwa sana hivyo ni vyema vijana wakatumika nafasi hiyo kusoma kwa bidii na kuwa na maadili mema.

    "Nafasi mliyoipata ni adhimu, elimu imepewa kipaumbele ili msome na kuweza kujikomboa, msichezee nafasi hii msome kwa bidii, mzingatie maadili mema na si kuiga tabia mbovu na mkawe wazalendo kwa taifa." Amesema Prof. Dungumaro.

    Aidha ameipongeza taasisi hiyo ya elimu inayosimamia shule za St. Mary's kwa kutoa wanafunzi bora ambao ni nguvu kazi yenye tija kwa jamii.

    "Nitoe pole kwa familia ya St. Mary's kwa kumpoteza Askofu Rwakatare lakini maono yake bado yanaishi, niwapongeze walimu na wanafunzi kwa kuendelea kuyaishi maono hayo hasa katika suala zima la utoaji wa elimu." Amesema.

    Aidha ametumia wasaa huo kumpongeza Rais Dkt. John Joseph Magufuli na Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuchaguliwa tena kuongoza taifa la Tanzania.

No comments: