NBC yazindua akaunti ya ‘NBC Kua Nasi’ kuwawezesha wafanyabiashara wadogo
· Serikali yaipongeza, yataka iongeze nguvu katika utoaji elimu.
.Katika kuhakikisha wafanyabiashara wadogo wanakuza biashara zao, benki ya Taifa ya biashara (NBC) imezindua huduma mpya ijulikanayo kama ‘NBC Kua Nasi’ huku Serikali ikiitaka kuongeza juhudi katika utoaji wa elimu ya fedha.
Akaunti ya ‘NBC Kua Nasi inawawezesha wajasiriamali wadogo kutunza pesa zao kwa usalama zaidi bila gharama za uendeshaji.Pia, inaambatana na utoajia wa elimu ya fedha ili kuwaongezea ufanisi wa uendeshaji wa biashara.
Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Godwin Gondwe alisema hatua hiyo ni muhimu katika utekelezaji wa mipango ya Serikali ikiwamo kuhakikisha kila mtanzania anafikiwa na huduma nafuu za kibenki.
“Akaunti hii ni fursa kwa vijana, akina mama na wajasiriamali wote; kwanza unaweka fedha zako na hakuna malipo ya mwezi.Pili, akaunti hii inaambatana na kutoa elimu ya kibenki, hii ni sehemu ambayo tulikuwa hatujaitilia mkazo hasa kwa wajasiriamali waodogo,” alisema Gondwe.
Aliitaka benki hiyo kuongeza nguvu zaidi katika kuwaelimisha wajasiriamali kufahamu namna bora ya usimamizi wa fedha ili waweze kukua zaidi.
“Mwaka jana tumetoa zaidi ya Sh2.6 bilioni za mikopo kwa wajasiriamali wadogo, hii huduma imekuja wakati muafaka ili waweze kufahamu namna bora zaidi ya kutunza fedha,” alisema.
Mkurugenzi wa Fedha wa NBC, Waziri Barnabas alisema akaunti hiyo inawawezesha wafanyabishara wadogo kukuza biashara zao kwa kuweka pesa kwa urahisi na unafuu kwani huduma hiyo inapatikana mahali popote kwa njia ya simu (NBC Kiganjani).
Alisema kupitia ‘NBC Kua Nasi’ wafanyabiashara wadogo kama mamalishe, madereva bodaboda,wasindikaji pamoja na wasusi wataweza kuhifadhi pesa zao kwa urahisi zaidi na kuacha kukaa na pesa taslimu njia ambayo si salama.
“Makundi haya yanaajiri watu wengi sana na ufikaji wa huduma za kifedha kwao umekuwa mgumu na mara nyingi wanakaa na fedha mkononi hivyo akaunti hii ni sehemu ya mpango wa benki yetu katika kuhakikisha tunawafikia watu wengi zaidi kuwapatia huduma za kifedha zinazoendana na shughuli zao za kiuchumi,” alisema Barnabas.
Aidha, mteja ataweza kupata riba ya hadi asilimia 2 atakapoweka fedha kwenye akaunti hiyo ndani ya mwaka.
Mmoja wa wafanyabiashara, Dativa Ngowi alisema huduma hiyo itakuwa msaada mkubwa kwa kupunguza gharama za uendeshaji za kila mwezi pamoja na makato ya kutoa pesa.
Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Godwin Gondwe na Mkurugenzi wa Fedha wa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC), Waziri Barnabas wakizindua huduma mpya ijulikanayo kama ‘NBC Kua Nasi’ katika hafla iliyofanyika kwenye tawi la benki hiyo Mbagala jijini Dar es Salaam.Kushoto ni Abel Kaseko, Mkuu wa Bidhaa na Mauzo wa NBC.AKaunti hiyo ni maalumu kwa wafanyabiashara wadogo kuwawezesha kuweka akiba kwa urahisi zaidi.
Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Godwin Gondwe akizungumza na wafanyakazi wa NBC pamoja na wafanyabiashara wadogo wadogo wa Wilaya hiyo wakati benki hiyo ilipozinuda huduma mpya ijulikanayo kama ‘NBC Kua Nasi’.Huduma hiyo inawawezesha wajasiriamali kuweka akiba ya pesa za mauzo kwa unafuu na usalama zaidi.
Mkurugenzi wa Fedha wa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) Waziri Barnabas akizungumza wakati wa uzinduzi wa huduma mpya ya benki hiyo ijulikanayo kama ‘NBC Kua Nasi’ ambayo inawawezesha wafanyabiashara wadogo kukuza biashara zao kupitia huduma nafuu za kibenki.Uzinduzi huo ulifanyika katika tawi la benki hiyo Mbagala jijini Dar es Salaam.
No comments: