Maelfu ya wananchi kuhudhuria mkutano wa kimataifa Arusha .
Na Jane Edward, Michuzi TV,Arusha
Maelfu ya wananchi kutoka mikoa mbalimbali wanatarajiwa kuhudhuria mkutano mkubwa wa injili wa kimataifa unaotarajiwa kufanyika novemba 19 hadi 22 mwaka huu katika viwanja vya relini vilivyopo mjini hapa.
Akizungumzia kuhusiana na maandalizi ya mkutano huo, Mratibu wa mkutano huo Arusha,Mwinjilisti Erik Levoyer alisema kuwa,shughuli za maandalizi ya mkutano huo zinaenda vizuri na wanatarajia maelfu ya watu kuhudhuria mkutano huo kwa ajili ya kusikiliza neno la Mungu pamoja na kuponywa matatizo mbalimbali .
Mwinjilisti Levoyer alisema kuwa,mkutano huo utahudumiwa na wahubiri wawili wa kimataifa ambao ni Mwinjilisti Daniel Kolenda na Nathan Morris kutoa nchini Marekani.
Alisema kuwa, kabla ya mkutano huo kufanyika wainjilisti wapatao 25 wanazunguka katika maeneo mbalimbali jijini Arusha ikiwemo masokoni,stendi ya mabasi, mashuleni,na kwenye mitaa mbalimbali kwa lengo ya kuwahudumia wananchi pamoja na kuhubiri injili.
"Mkutano huu umeandaliwa na huduma ya marehemu , Mwinjilisti Reinhard Bonnke ambaye kwa mara ya mwisho alikuja hapa Tanzania,mkoani Arusha mwaka 1996 kuhubiri injili ikiwa ni moja ya malengo yake kuhakikisha waafrika wanaokolewa kupitia injili ."alisema Mwinjilisti Levoyer.
Aliwataka wananchi wa mkoa wa Arusha na mikoa jirani kuhakikisha wanashiriki kwa wingi katika mkutano huo mkubwa wa injili ili waweze kupokea uponyaji na kusikiliza injili .
Naye Mratibu wa mkutano huo kwa Arusha,Askofu wa kanisa la Maranatha Mianzini,Eric Mukwenda alisema kuwa,maandalizi ya mkutano huo yamekamilika ambapo wanatarajia maelfu ya wananchi kuhudhuria mkutano huo na kupata uponyaji pamoja na kumjua Mungu pia.
Askofu Mukwenda alisema kuwa,mkutano huo ambao umeandaliwa na huduma ya marehemu Mwinjilisti Bonnke kwa kushirikiana na umoja wa madhehebu Arusha uliwahi kufanyika tena mwaka 1996 mkoani Arusha na kuleta manufaa makubwa kutokana na maelfu ya watu kuokolewa na kuponywa shida mbalimbali.
Aliwataka wananchi mkoani Arusha na mikoa jirani kuhudhuria kwa wingi katika mkutano huo ili waweze kufunguliwa na kutatuliwa shida zao.
No comments: