HATUTOWAMISS WAPINZANI, TUTAISIMAMIA, KUISHAURI NA KUIKOSOA SERIKALI PALE INAPOBIDI-WABUNGE CCM
Charles James na Janeth Rafael, Michuzi TV
HATUWAMISS wala nini? Hii ni kauli iliyotolewa na Wabunge wa Chama cha Mapinduzi CCM kwenye mahojiano na Michuzi Blog iwapo watawakumbuka wabunge wa upinzani au hawatokua na la kuwakumbuka katika kipindi hiki ambacho Bunge linatawaliwa na wabunge wengi wa chama tawala.
Bunge hili la 12 lenye wabunge 364 lina wabunge wawili tu wa upinzani mmoja kutoka Chama cha Demokrasi na Maendeleo Chadema na mwingine wa Chama cha Wananchi CUF.
Wakizungumza na Michuzi Blog wabunge hao wa CCM wamesema kinachoangaliwa bungeni ni uwezo wa wabunge kuhoji na kuisimamia serikali, kushughulika na mambo ya kitaifa pamoja na kuwatetea wananchi wao bila kujali vyama.
Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka amesema licha ya kuwepo kwa baadhi ya wabunge wachache wa upinzani waliokua wakiyasemea vizuri mambo ya wananchi bado kutokuepo kwao hakutopunguza nafasi ya wabunge wa CCM kuwa wasemaji wa wananchi.
"CCM ni chama kinachoamini katika dhana ya kukosoa na kukosoana na kama mnavyojua kupitia muongozo wa mwaka 1981 CCM iliweka bayana kukosoa na kukosoana ni silaha ya mapinduzi na ukienda mbele inasema kukiri upungufu si dalili ya kushindwa bali ni ishara ya kujiimarisha hivyo nina imani wabunge wa CCM hatutoacha kuikosoa na kuisimamia serikali. " Amesema Ole Sendeka.
Kwa upande wake Mbunge wa Makete Festo Sanga amesema kutokuwepo kwa wabunge wa upinzani hakutowafanya wabunge wa CCM kufanya kazi kwa bidii wakitanguliza na kuweka mbele maslahi ya wananchi huku pia wakiishauri, wakiikosoa na kuisimamia serikali katika kuwatumikia watanzania wote bila kujali Itikadi za vyama vyao.
"Hatutowamiss kwa sababu tunaamini sisi tuliokuja hapa tumeaminiwa na wananchi, bunge lililopita walikuwepo lakini walikuwa wakiongoza kwa kuweka maslahi ya chama chao zaidi kuliko kuwatetea wananchi, kazi yao ilikua kupinga kila kitu hata bajeti za wizara." Amesema Mbunge Innocent Bashungwa.
No comments: