DC KITETO AIFAGILIA TAKUKURU
Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, Kanali Patrick Songea, aliyevaa miwani akizungumza kwenye hospitali ya wilaya hiyo baada ya kufanya ziara ya kushtukiza.
………………………………………………………………………………..
Na Mwandishi wetu, Kiteto
Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, Kanali Patrick Songea ameipongeza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU kwa kufanikisha uokoaji wa shilingi milioni 200 zilizofanikisha ununuzi wa mashine ya ultrasound ya shilingi milioni 46 kwenye hospitali ya wilaya hiyo.
Kanali Songea ameyasema hayo Novemba 14 alipofanya ziara ya kushtukiza kwenye hospitali ya wilaya hiyo.
Amesema lengo la ziara hiyo ya kushtukiza ni kukagua utoaji huduma ya afya kwa wananchi na kukagua mradi wa ujenzi wa wodi ya watoto na wanawake na duka la dawa. Ameipongeza TAKUKURU kwa kuwepo kwa mashine hiyo kwani mwaka 2018 walifuatilia na kudhibiti zabuni ya chakula cha shule ya sekondari ya Kiteto ambapo waliokoa fedha zilizosababisha kununuliwa kwa mashine ya hospitali hiyo.
Amesema TAKUKURU Wilayani Kiteto waliokoa shilingi milioni 200 kati ya hizo shilingi milioni 46 kwenye mchakato wa zabuni ya chakula cha shule hiyo ambazo zilitumika kununulia mashine hiyo ya hospitali. Mkuu huyo wa Wilaya amesema TAKUKURU walidhibiti fedha hizo baada ya wazabuni waliopandisha bei kinyume na taratibu.
Pia, Mkuu huyo wa Wilaya ameipongeza TAKUKURU Wilayani Kiteto kwa kuwafikisha mahakamani daktari na mtaalamu wa dawa ya usingizi wa hospitali hiyo kwa madai ya rushwa.
Amesema kitendo hicho kimeifanya serikali kupata imani kubwa kutoka kwa wananchi kwani malalamiko katika sekta ya afya wilayani humo ni mengi hivyo hatua zilizochukuliwa ni sahihi.
No comments: