BARAZA LA WAFANYAKAZI LA HOSPITALI YA RUFAA YA MKOA WA SHINYANGA LAZINDULIWA

Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi la Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Shinyanga, Dk. Rose Malisa ambaye ni Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa mkoa wa Shinyanga akizungumza wakati wa Uzinduzi wa Baraza la Wafanyakazi la Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga. Wa kwanza kushoto ni Katibu wa Chama Cha Wafanyakazi (TUGHE) mkoa wa Shinyanga, Gaudensi Kadyango akifuatiwa na Kaimu Mwenyekiti wa TUGHE mkoa wa Shinyanga, Rajabu Masanche akifuatiwa na Mwakilishi wa Mganga Mkuu mkoa wa Shinyanga, Timoth Sosoma.
Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi la Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Shinyanga, Dk. Rose Malisa ambaye ni Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa mkoa wa Shinyanga akizungumza wakati wa Uzinduzi wa Baraza la Wafanyakazi la Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga.
Mwakilishi wa Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Timoth Sosoma akizungumza wakati akizindua Baraza la Wafanyakazi la Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga.
Mwakilishi wa Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Timoth Sosoma akizungumza wakati akizindua Baraza la Wafanyakazi la Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga.
Katibu wa Chama Cha Wafanyakazi (TUGHE) mkoa wa Shinyanga, Gaudensi Kadyango akitoa mada ya wajibu na majukumu ya wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi la Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga na umuhimu wa Chama cha Wafanyakazi.

Kulia ni Katibu Msaidizi wa Baraza la Wafanyakazi la Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Shinyanga Allan Luvanda akifuatiwa na Katibu wa Baraza hilo, Clementina Salutari na Mwenyekiti wa Baraza hilo Dk. Rose Malisa. Wa kwanza kushoto ni Kaimu Mwenyekiti wa TUGHE mkoa wa Shinyanga, Rajabu Masanche. 
Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi la Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga wakipiga picha ya pamoja baada ya Uzinduzi wa Baraza la Wafanyakazi la Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga.

Na Kadama Malunde 
Mwakilishi wa Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Timoth Sosoma amezindua rasmi Baraza la Wafanyakazi la Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga ambalo litakuwa na jukumu la kujadili mikakati mbalimbali ya kuimarisha na kuboresha utendaji na uwajibikaji ndani ya hospitali utakaowezesha hospitali kutoa huduma kwa wananchi kwa haraka,uwazi,urahisi,gharama nafuu wakati wowote.

Uzinduzi huo umefanyika leo Jumatano Novemba 4,2020 katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga na kuhudhuriwa na wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi la Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga pamoja na viongozi wa Chama Cha Wafanyakazi (TUGHE) mkoa wa Shinyanga.

Akizindua Baraza hilo la Wafanyakazi, Mwakilishi wa Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Timoth Sosoma amesema baraza hilo litakuwa chachu ya kuboresha huduma za afya katika hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Shinyanga huku akiwasisitiza wajumbe kuwa waadilifu na kuzingatia maadili ya utumishi wa umma.

“Hiki ni kikao cha kwanza cha Baraza la Wafanyakazi tangu mabadiliko ya kuwa chini ya Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto. Mkiwa sehemu ya historia hii ni matumaini yangu kuwa nafasi mliyopewa mtaitumia vizuri kwa ajili ya kushauri namna bora ya kuboresha utendaji kazi na kujenga mahusiano baina ya Mwajiri na Mwajiriwa”,amesema Sosoma.

“Madhumuni ya kuundwa kwa mabaraza ya wafanyakazi ni kuishauri serikali kuhusu usimamizi wa kazi na rasilimali,utekelezaji wa majukumu,kulinda haki na wajibu wa Waajiri na Wafanyakazi,kutoa ushauri kuhusu kujenga hali bora za kazi na maslahi na kusimamia haki na ustawi katika sehemu za kazi”,ameongeza Sosoma.

Amesema Baraza la Wafanyakazi kama vyombo vya ushauri na usimamizi yana wajibu wa kuhakikisha kuwa waajiri na watumishi wanatambua wajibu na haki zao na wanazingatia maadili ya utumishi wao kuleta mabadiliko ya utendaji kazi yenye tija, staha na upendo.

“Maadili ni kitu muhimu cha kuzingatia katika utendaji kazi. Ni lazima kila mtumishi wa umma kujiepusha na vitendo vinavyoashiria ukosefu wa maadili kama vile rushwa,utovu wa nidhamu,utoaji wa siri za serikali na huduma mbaya kwa wagonjwa”,amesisitiza Sosoma.

Aidha amewataka wajumbe wa Baraza hilo kufanya vikao walau mara mbili kwa mwaka kwa mujibu wa sheria ili kuepusha fursa kwa wafanyakazi kukuza majungu mahala pa kazi na kwamba vikao hivyo havipaswi kupuuzwa hivyo viandaliwe katika viwango vinavyokidhi malengo na makusudio ya sheria.

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi la Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Shinyanga, Dk. Rose Malisa amewaomba wajumbe wa baraza hilo kuzingatia majukumu yao ambayo ni pamoja na kuwashirikisha wafanyakazi wa serikali katika utekelezaji wa shughuli za hospitali kwa ushirikiano na uongozi wa hospitali na kuishauri Menejimenti juu ya ufanisi wa kazi na hatua zinazofaa kuchukuliwa kuboresha huduma za afya na maslahi ya wafanyakazi.

Aidha Dk. Malisa ambaye ni Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa mkoa wa Shinyanga amewataka wajumbe wa baraza hilo kuwa chachu ya mabadiliko katika kuboresha huduma za afya katika hospitali na kuendelea kutoa elimu ya afya kwa jamii.

Kwa upande wake, Katibu wa Chama Cha Wafanyakazi (TUGHE) mkoa wa Shinyanga, Gaudensi Kadyango amewataka wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi la Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga kufanya kazi kwa bidii,kujipenda na kuwa mfano bora kwa watumishi wengine wa umma.

Aidha amewakumbusha watumishi wa umma kuzingatia maadili ya kazi yao ikiwa ni pamoja na kuepuka kutumia lugha mbaya kwa wateja na kuendekeza matumizi ya simu za mkononi wakati wa kazi.

Uzinduzi wa Baraza la Wafanyakazi la Hospitali ya Rufaa mkoa wa Shinyanga umekwenda sanjari na uchaguzi wa viongozi Baraza hilo ambapo Clementina Salutari amechaguliwa kuwa Katibu na Allan Luvanda kuwa Katibu Msaidizi.

No comments: