WAWILI KIZIMBANI KWA KUISABABISHIA TCRA HASARA YA SH.MILIONI 267.6



 

Na Karama Kenyunko, globu ya jamii 

WAKAZI wawili wa jijini Dar es Salaam,  wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka manne likiwemo la kuisababishia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) hasara ya Sh. milioni 267.6.

Katika hati ya mashtaka iliyosomwa mahakamani hapo na wakili wa serikali Mwandamizi Wankyo Simon akisaidiana na wakili wa serikali Jackline Nyantori na Yusuph Abood imewataja washtakiwa hao kuwa  ni Baraka Mtunga (43)a mhandisi na  mkazi wa Mikocheni na Mfanyabiashara Rajabu Katunda (42)  anayeiishi Kinondoni.

Mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Kassian Matembele imedaiwa kati ya Desemba 13, 2019 na Septemba 28 mwaka huu katika maeneo ya Hifadhi ya Taifa ya Saadan  katika kijiji cha Kajanjoo wilayani Bagamoyo mkoani Pwani na maeneo ya jiji la Dar es Salaam, washtakiwa kwa pamoja waliongoza genge la uhalifu kwa lengo la kujipatia faida.

Imeendelea kudaiwa kuwa siku na mahali hapo hapo  washitakiwa hao walisimika na kutumia vifaa vya mawasiliano vya kielektroniki bila kuwa na leseni ya TCRA huku poa wakidaiwa kutumia vifaa vya kielektroniki kusambaza mtandao wa intaneti bila kuwa na leseni.

Aidha katika shtaka la nne lililosomwa na wakili Nyantori inadaiwa washtakiwa wakiwa na nia ya kukwepa kulipa malipo halali ya mtandao, walisambaza huduma ya mtandao (WiFi) isivyo halali na kuisababishia kwa TCRA hasara ya Sh 267,656,794.30.

Katika shtaka la sita inadaiwa washtakiwa hao kwa pamoja walijihusisha na miamala hiyo ya kifedha huku wakijua fedha hizo ni zao la makosa ya kutumia vifaa vya mawasiliano kwa ulaghai na uhalifu wa kupangwa.

Hata hivyo washtakiwa hawakuruhusiwa kujibu kitu chochote mahakamani hapo kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi ambazo kwa kawaida kusikilizwa mahakama Kuu.

Kwa  mujibu wa upande wa mashtaka upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika hivyo waliomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa na kesi hiyo imeahirishwa hadi Oktoba 27 mwaka huu, na washtakiwa wamerudishwa rumande kwa sababu mashtaka yanayowakabili hayana dhamana kisheria.


No comments: