'UBUNGO INTERCHANGE' JIJINI DAR KUKAMILIKA DESEMBA 30,2020

Na Mwandishi Wetu, Michuzi TV.


IMEELEZWA mradi wa ujenzi wa barabara za juu katika eneo la Ubungo  jijini Dar es Salaam  unaofahamika 'Ubungo Interchange' ambao unazikutanisha  barabara tatu za Sam Nujoma, Mandela na ile ya Morogoro unaotekelezwa na Serikali kupitia TANROADS umefikia asilimia 81 na unatarajiwa kukamilika rasmi Desemba 30,2020.

Meneja wa Mradi huo, Mhandisi Barakaeli Mmari ameviambia vyombo vya habari kwamba ujenzi huo ulioanza Mei mwaka 2017 unaendelea vizuri na sasa barabara zote mbili za juu zimefunguliwa kwa majaribio wakati ujenzi ukitarajiwa kukamilika kwa asilimia 100 Desemba, 30 mwaka huu.


Akifafanua zaidi, Mhandisi Mmari amesema kwa mara ya kwanza Mei 30, mwaka huu walifungua barabara ya ghorofa ya chini ya Morogoro kwa majaribio na waliruhusu magari kupita wakati Septemba 30, 2020 barabara ya ghorofa ya pili ya Nelson Mandela / Sam Nujoma ilifunguliwa kwa majaribio.


Pia amesema ni mategemeo yao ifikapo Desemba 30, 2020 ujenzi utakuwa umekamilika kwa asilimia 100 na wananchi wataendelea kufaidi barabara hiyo yanatokana na matunda ya Serikali ya Tano chini ya Rais John Magufuli huku akisisitiza ujenzi wa barabara za juu ulikuwa na lengo la kuondoa msongamano wa magari katika makutano ya barabara hizo eneo la Ubungo.


Ambapo kutokana na msongamano mkubwa wa magari uliosababisha watu kuchelewa kufika  katika shughuli zao kwa wakati na hivyo kupoteza muda mwingi ambao ungetumika kuwaongeza kipato.


Amezungumzia jinsi madereva watakavyokuwa wakitumia barabara hizo ambapo amefafanua eneo hilo kuna barabara ngazi (ghorofa) tatu, ya chini, ya kati na ya juu."Ngazi ya chini itatumiwa na magari yanayotoka Mjini kwenda Mwenge, Mwenge-Kimara, Kimara-Buguruni na Buguruni kwenda Mjini. Pia itatumiwa na magari yote yanayopinda kushoto kwenye maungio hayo".


Wakati ngazi ya kati kwa mujibu wa Mhandisi Mmari itatumiwa na magari yanayotoka Kimara kwenda mjini na yatokayo mjini kwenda Kimara huku ngazi ya juu itatumiwa na magari yatokayo Mwenge kwenda Buguruni na yatokayo  Buguruni kwenda Mwenge.


Ameongeza barabara za juu zimejumuisha njia maalum kwa ajili ya mabasi ya mwendo kasi.Kuhusu ajira amesema wakati ujenzi ukiendelea umekuwa ukiajiri wananchi wengi wakiwemo wa kawaida mpaka wahandisi wanaoshughulika na ambao kazi za kihandisi ili  kutekeleza ujenzi huo kwa ufanisi.


Amefafanua wameajiri wafanyakazi kati ya 800 hadi 900 kwa mwezi na kati ya hao wanaotoka nje ya Tanzania ni asilimi 10 ya wafafanyakazi wote wakati wazawa walioajiriwa ni asilimia 90."Kwa hiyo ujenzi huu umeleta faida kwa watanzania wengi hasa wakazi wa Dar es Salaam”, Amesema Mhandisi Mmari.


Kwa upande wa baadhi ya wakazi wa Ubungo wametumia nafasi hiyo kuuzungumzia mradi huo  ambapo wamesema wamefurahishwa na mradi huo kwani unakwenda kumaliza kabisa msongamano eneo hilo.


Mkazi wa Ubungo Bakari Juma amesema wanaishukuru Serikali kwa hatua ya kujenga barabara za juu kumaliza changamoto ya foleni na katika kipindi hiki cha majaribio wameshuhudia magari yanavyopita bila kukaa muda mrefu kwani hakuna foleni tena.


Wakati Johnson Mwakalukwa ameongeza barabara hiyo imesaidia hata kwa wasafiri kutoka mikoani kupata ahueni kwani sasa wakifika Mbezi wanakutana na barabara ile ya njia nane na kisha wanamalizia na Ubungo Interchange."Kwa hiyo kukaa zaidi ya saa mbili kwenye foleni katika makutano ya Ubungo  hakuna tena kwa sasa."


Kabla ya ujenzi wa  barabara hizo usumbufu ulikuwa mkubwa kwa wananchi wa Dar es Salaam hasa wanaotumia barabara hiyo ambapo wengi wao walikuwa wanachelewa kwenda katika shughuli za kujitafutia kipato. 




No comments: