TAKUKURU MANYARA YAJIPANGA KUZUIA RUSHWA KWENYE UCHAGUZI

 


Na Mwandishi wetu, Manyara

TAASISI ya Kuzuia na kupambana na rushwa TAKUKURU Mkoani Manyara, imejipanga kuhakikisha inafuatilia na kuzuia rushwa kwenye kipindi hiki cha kampeni za vyama na uchaguzi mkuu.

Naibu Mkuu wa TAKUKURU mkoani Manyara, Isdory Kyando ameyasema hayo mjini Babati wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya taarifa ya utendaji kazi kuanzia mwezi Julai hadi Septemba mwaka huu.

Kyando amesema wanafuatilia na kuzuia vitendo vya rushwa kwenye uchaguzi mkuu ili kuepuka kuchagua viongozi wasiofaa kutokana na vitendo vya rushwa.

Amesema TAKUKURU imejipanga kuendelea na majukumu yake katika robo ya Oktoba hadi Desemba 2020 ambapo pamoja na mambo mengine kipaumbele kitakuwa katika maeneo yafuatayo.

Amesema wataendelea na ufuatiliaji wa matumizi ya fedha zilizotolewa kwa ajili ya ujenzi wa shule za msingi na sekondari.

``Tutaendelea kufuatilia kwa karibu maendeleo ya watumishi wanaolalamikiwa mara kwa mara na tutafanya uchunguzi wa kina dhidi yao na kuchukua hatua stakii za kisheria,`` amesema Kyando.

Amesema katika kuelimisha umma wametoa jumla ya semina 56 zilizoendeshwa kwenye makundi tofauti ili kuelimisha jamii katika kupambana na rushwa.


Amesema wamefanya jumla ya mikutano 56 ilifanyika ikiwa na madhumuni ya kuelezea athari za rushwa na namna ya kupambana nayo.

``Jumla ya makala mbili ziliandikwa, makala hizi hutolewa katika jarida jarida la TAKUKURU ambalo hutolewa kila baada ya miezi mitatu,`` amesema Kyando.

Amesema TAKUKURU imekuwa sehemu ya kuimarisha vyama vya ushirika, kabla TAKUKURU haijaingilia urejeshwaji wa fedha za vyama vya ushirika vyama vingi vilikuwa taabani kifedha kiasi cha kushindwa kutekeleza majukumu na kufikia malengo kwa kuwa fedha nyingi zilikuwa mikononi  mwa watu na hawakuwa tayari kuzirejesha.

Amesema kuongezeka kwa ushiriki wa wana Manyara kwenye mapambano dhidi ya rushwa, kutoa taarifa hasa baada ya kazi kubwa kuonekana ikiendelea kufanyika katika kusimamia haki na kudhibiti vitendo vya rushwa na ubadhirifu na matumizi mabaya ya madaraka.

Amesema awali taarifa zilizokuwa zinapokewa zilikuwa chache ukilinganisha na sasa na taarifa hizi wamezipima na kubaini kuwa siyo kwamba vitendo vya rushwa vimeongezeka bali zimetokana na mwamko na ujasiri wa wana Manyara kutoa taarifa TAKUKURU kila wanapokutana na changamoto.


No comments: