TAASISI YA MOYO JAKAYA KIKWETE (JKCI) YAWA KITIVO CHA ‘KUTENGENEZA’ WATAALAMU MABINGWA WA MOYO NDANI NA NCHI

 

Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi  ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi akizungumza na wajumbe wa baraza hilo wakati wa kikao cha  nne cha baraza kilichofanyika leo jijini Dar es salaam. Kulia ni Katibu Msaidizi wa Baraza hilo Renatha Miiruko.

Wajumbe wa  Baraza la  Wafanyakazi wa  Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakifuatilia mada ya sheria za kazi wakati wa kikao cha  nne  cha baraza hilo  kilichofanyika leo jijini Dar es salaam.Jumla ya wajumbe 59 walihudhuria kikao hicho.

Mkurugenzi wa Kurugenzi ya  Tiba Shirikishi wa  Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Delila Kimambo akieleza kazi zilizofanywa na kurugenzi yake  wakati wa kikao cha nne cha  baraza la wafanyakazi wa Taasisi hiyo  kilichofanyika leo jijini Dar es salaam.

Afisa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Mary Haule akiuliza swali wakati wa   kikao cha nne cha  baraza la wafanyakazi wa Taasisi hiyo  kilichofanyika leo jijini Dar es salaam.

Mhadhiri wa chuo kikuu cha Tumaini Dkt. Mtaki akitoa mada ya sheria za kazi  kwa wajumbe wa kikao cha nne cha  baraza la wafanyakazi wa   Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kilichofanyika leo jijini Dar es Salaam.

Mfanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Roberth Luchemba  akichangia mada ya sheria za kazi wakati wa kikao cha nne cha baraza la wafanyakazi wa Taasisi hiyo kilichofanyika leo jijini Dar es Salaam. Jumla ya wajumbe 59 walihudhuria kikao hicho.

Wajumbe wa Baraza la wafanyakazi wa  Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakiwa katika picha pamoja mara baada ya kumalizika kwa  kikao cha nne cha baraza la wafanyakazi wa Taasisi hiyo kilichofanyika leo jijini Dar es Salaam. Waliokaa katikati ni Mwenyekiti wa Baraza hilo ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI Prof. Mohamed Janabi.  

Picha na JKCI

……………………………………………………………………………….

Na Mwandishi Wetu  –  Dar es Salaam

20/10/2020 Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imekuwa kitivo mahususi cha ufundishaji wataalamu mabingwa wa moyo ndani ya nchi kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), hivi sasa inatarajia kila mwaka  ‘kutengeneza’ wahitimu 10.

Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Profesa Mohamed Janabi amesema hayo leo alipozungumza na waandishi wa habari wakati wa Kikao cha nne cha Baraza la Wafanyakazi wa Taasisi hiyo .

Amesema hatua hiyo itaisaidia Tanzania kupata wataalamu mabingwa wa moyo watakaosaidia kuendelea kuimarisha huduma za matibabu hayo nchini.

“JKCI ni Taasisi pekee kubwa ya umma inayotoa matibabu haya nchini, lakini hii si hospitali tu, imekuwa pia sehemu kubwa ya mafunzo kwa madaktari na wauguzi, kwa kuwa sisi si chuo, ndiyo maana tunashirikiana kwa ukaribu na MUHAS, mwaka huu watahitimu wataalamu saba na kuanzia mwaka ujao wa masomo tunatarajia watahitimu wataalamu 10,” amesema.

Ameongeza “Kwa mfano hizi digrii za pili za uzamili kwa mfano ‘masters in cardiology’ ya miaka miwili, asilimia 96 ya walimu wanatoka JKCI kwa ushirikiano na MUHAS tunatoa hizi kozi.

“Kuna kozi mpya ya upasuaji wa kifua ambayo imeanzishwa  walimu sita kati ya wanane wanatoka JKCI, ni hatua kubwa ambayo taasisi imepitia kuwa kitivo cha ‘uzalishaji’ wataalamu mabingwa wa moyo nchini.

“Zaidi ya asilimia 90 ya wataalamu mabingwa wa moyo nchini hivi sasa wapo JKCI, uwiano kwa nchi zetu zote Afrika bado si mzuri, kwa mfano sisi ndiyo hospitali kubwa kuliko zote si tu Tanzania bali katika Ukanda wote huu wa Afrika Mashariki na Kati”,.

“Juhudi zimefanyika kubwa sasa hivi Dodoma (Hospitali ya Benjamin Mkapa – BMH) imeanzisha kitengo cha moyo tunashirikiana nao kwa ukaribu vile vile Hospitali ya Rufaa ya KCMC nayo imeanzisha kitengo na tunafanya nao kazi kwa ukaribu,” amebainisha.

Ameongeza “Hivyo kila mwaka Tanzania tunatarajia ‘tutazalisha’ madaktari kati ya 10 na 13, hii ni namba kubwa mno.

Kuhusu Baraza hilo la wafanyakazi, Prof. Janabi ambaye pia ni Mwenyekiti wake amesema  limekuwa la mafanikio likiwaunganisha uongozi wa juu na wafanyakazi kuweza kufahamu huduma tunazotoa, changamoto ni zipi na wapi tunaelekea, lina wawakilishi 62 kutoka kila idara.

“Tunajivunia utulivu mkubwa uliopo kwenye Baraza hili, menejimenti inaongoza wafanyakazi 310 na wote wanahitaji kupata huduma wanazostahili ili wananchi wapate huduma ambazo nchi inafikiria kuzitoa kwao.

Awali, Katibu wa baraza la wafanyakazi  Dk. Samwel Rweyemamu amesema baraza hilo limekuwa likihakikisha linasimamia kwa dhati maslahi ya wafanyakazi ili kuimarisha morali ya utendaji kazi kwa maslahi mapana ya wananchi wanaowahudumia.

“Kwa mfano kila mwaka tumekuwa tukitambua mfanyakazi bora, tumependekeza pia iwe wafanyakazi watatu bora kila mwaka, yaani mshindi wa kwanza, pili na tatu ili kuwapa motisho na hamasa wafanyakazi kuendelea kufanya vema zaidi,” amebainisha.

No comments: