SOKOINE, SUA VYAPATA UFADHILI WA SH. BILIONI 2.3 KWA UTAFITI WA DAWA ZA MIMEA
Mkurugenzi wa Uratibu na Uendelezaji wa Utafiti, Dkt. Bugwesa Katale wa Tume ya Sayansi na Teknolojia Tanzania (COSTECH) kulia na Ofisa Mtafiti na Mratibu wa tume hiyo, Neema Tindamanyire wakisikiliza maswali ya Waandishi wa Habari (hawapo pichani) kwa ajili ya ufafanuzi wa vyuo viwili hapa nchini vilivyopata ufadhili wa Dola za Marekani milioni moja kwa ajili ya utafiti wa magonjwa ya wanyama na samaki.
Na Karama Kenyunko, Michuzi TV
CHUO Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) na Taasisi ya Afrika ya Sayansi (NMAIST) na Teknolojia ya Nelson Mandela vimepata ufadhili wa dola za Marekani milioni moja sawa na Sh. Bilioni 2.3 kwa ajili ya kufanya utafiti wa magonjwa manne, kuendelea kutafuta dawa za kupambana na Malaria kutokana na mimea.
Aidha, ufadhili huo pia utahusiana na mafunzo, ambapo fedha hizo zitatumika kufadhili Shahada ya Uzamili, Shahada ya Uzamivu (PHD) na Shahada zingine ambazo zinahusiana na masuala ya utafiti.
Hayo yamesemwa leo Oktoba 16,2020 na Mkurugenzi wa Uratibu na Uendelezaji wa Utafiti, Dkt.Bugwesa Katale wa Tume ya Sayansi na Teknolojia Tanzania (COSTECH), ambapo time hiyo ndiyo itafuatiliwa utafiti huo.
Dkt. Katale amesema fedha hizo zimepitia COSTECH, na zimetolewa na Mpango wa Vigoda vya Utafiti vya Afrika (ORTAChI,) na kazi yao kubwa ni kufuatilia miradi hiyo, kuandaa ripoti na kuhakikisha malengo yaliyokuwamo kwenye miradi hiyo yanafanikiwa.
Amesema chuo cha Sokoine kilichopo mkoani Morogoro kitafanya utafiti wa namna wa kuendeleza utambuzi wa virusi vinavyosababisha magonjwa kwa wanyama na samaki pamoja na upatikanaji wa samaki wa chanjo.
Pia, amesema chuo hicho kitafanya utafiti wa kuangalia magonjwa manne homa ya nguruwe, sotoka ya ngozi ya mbuzi na kondoo, kideli pamoja na ugonjwa unaoathiri samaki waliyopo kwenye maji asili pamoja na wale ambapo wanafugwa.
"Utafiti huu utakaofanywa na Chuo Kikuu cha Sokoine utasimamiwa na Profesa Gerald Misinzo," amesema Dkt.Katale.
Mkurugenzi huyo, amesema kwa upande wa Taasisi ya Nelson Mandela utafiti huo utafanyika kutafuta dawa za kupambana na Malaria kutokana na mimea na kuboresha ufanisi wa dawa zilizopo kwa kutumia teknolojia.
Amesema taasisi hiyo itashirikiana na Chuo Kikuu cha Western Cape cha Afrika Kusini, Baraza la Sayansi na Utafiti wa Viwanda (Afrika Kusini), Taasisi ya Utafiti ya Magonjwa ya Binadamu cha nchini Kenya na vyuo vingine.
Amesema, mpango huo utazinduliwa rasmi Oktoba 27,2020 nchini Afrika Kusini, kutokana na juhudi za kiongozi mashahuri wa Afrika Kusini, Oliver Tambo ambaye alikuwa ni mtetezi wa masuala Sayansi na teknolojia.
Dkt.Katale amesema Mpango wa ORTAChI ulianzishwa na Mfuko wa Utafiti wa Afrika Kusini (NRF) Idara ya ya Sayansi na Ubunifu kwa Ushirikiano wa Mfuko wa Oliver na Adelaide Tambo (OATF.)
Kwa upande wake, Ofisa Mtafiti na Mratibu wa COSTECH, Neema Tindamanyire amesema kuna magonjwa mengine yanawapata wanyama yanaambukiza pia wanadamu, hivyo wanavyojaribu kutafuta suluhisho ya wanyama wana magonjwa gani.
"Lakini pia tunasaidia mlaji anayekula nyama ili asipate magonjwa, kwa sababu binadamu anaweza kupata magonjwa kupitia nyama ya mnyama ambaye ana ugonjw." amesema Tindamanyire.
Pia, Tindamanyire amesema hadi kupata ufadhili huo walipitia mchakato, ambapo kwa hapa nchini vyuo vilivyoshiriki vilikuwa sita, lakini vilivyopata ni viwili tu.
" Nchi 15 zilishindana kupata ufadhili huo, lakini Tanzania tukapata vyuo viwili, ambapo nchi zingine hazijapata kabisa , kwa hiyo mchakato ulikuwa wazi kutokana na ulikuwa wa kuandika maandiko," amesema.
No comments: