SERIKALI YAKABIDHI BAISKELI 103 KWA WAHUDUMU WA AFYA IKUNGI
Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Edward Mpogolo akikabidhi usafiri wa Baiskeli na Vipaza sauti kwa Wahudumu wa Afya ngazi ya Jamii wilayani hapo juzi kama nyenzo muhimu zitakazowasaidia. kurahisisha utekelezaji wa majukumu yao.
Mkuu wa Wilaya Mpogolo akiendesha hafla hiyo.
Na Godwin Myovela, Ikungi
SERIKALI kwa kushirikina na Umoja wa Nchi za Ulaya na Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) imetoa jumla ya baiskeli 103 kwa wahudumu wote wa afya ngazi ya jamii sambamba na ‘vipaza sauti’ vyenye idadi kama hiyo wilayani hapa, lengo ni kuwapunguzia changamoto ya usafiri wakati wakitekeleza majukumu yao.
Katika kuboresha afya ya uzazi na lishe, kupitia mradi wa ‘Boresha Lishe’ serikali kupitia halmashauri ya Ikungi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, wakiwemo mashirika yasiyo ya kiserikali ya ‘SEMA’ na ‘RECODA’ imeazimia kupunguza udumavu wa siku 1000 za mtoto-yaani tangu kutungwa kwa mimba hadi anapofikisha miaka 2.
Akizungumza katika hafla ya kukabidhi baiskeli hizo ofisini kwake jana, Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Edward Mpogolo aliwataka waliokabidhiwa baiskeli hizo kuhakikisha wanazitunza na zinatumika kwa malengo kusudiwa.
“Niwasihi muwe waangalifu na mzitunze baiskeli hizi, serikali itaendelea kuweka mazingira rafiki kwenye sekta ya afya hususani kwenye eneo hili la afya ya uzazi na lishe, azma ikiwa ni kuhakikisha tunaondoa kabisa kiwango cha utapiamlo wa udumavu kutoka asilimia 7 mpaka 0,” alisema Mpogolo.
Aidha, aliyashukuru mashirika na nchi wahisani wanaoendelea kushirikiana na serikali katika kutekeleza mradi wa Boresha Lishe kwa vijiji 43 kuzunguka Ikungi huku akisisitiza ni mradi wenye tija kwa makundi yote ya jamii wilayani hapo, na hasa akinamama wajawazito, wanaonyonyesha na watoto chini ya miaka miwili.
Naye Afisa Lishe na Mratibu wa Huduma za Jamii wilayani hapo, Agnes John, alisema Halmashauri ya Ikungi ina jumla ya Kata 28 na Vijiji 101 vyote vina wahudumu wa Afya ngazi ya Jamii, na wote wamepatiwa mafunzo ya msingi ya awali ya afya ya uzazi na lishe.
Halmashauri ya Ikungi ina jumla ya wakazi 329,520, ambapo watoto chini ya miaka mitano ni 58,707, na wanawake wenye umri wa kuzaa (miaka 15-49) wanafikia 22,884.
“Mafanikio tuliyoyapata mpaka sasa ni kujikwamua mapema kwenye rangi nyekundu, kwa miaka miwili mfululizo mpaka sasa viashiria vyote vinavyohusiana na huduma za wahudumu wa afya ngazi ya jamii vina alama ya kijani kuashiria tunafanya vizuri,” alisema John.
Aidha, mratibu huyo alisema hata kiwango cha utapiamlo wa udumavu kimepungua kutoka asilimia 7 mpaka asilimia 5, wakati kimkoa ni asilimia 29.8. Alisema ukondefu umepungua kutoka asilimia 1 hadi kufikia 0.4, wakati kimkoa ni asilimia 4.7.
No comments: