MAJALIWA: LETENI MTU ANAYETOKA CHAMA MAKINI

 

 

Mjumbe wa Kamati Kuu ya halmashauri Kuu ya taifa ya CCM, Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipomuombea kura mgombea Urais wa CCM, Rais DKt. John Pombe Magufuli, Mgombea Ubunge wa CCM wa Jimbo la Mchinga, Mama Salma Kikwete, na mgombea Udiwani wa CCM katika Kata ya Milola katika Jimbo la Mchinga, Magreth Namahonji katika mkutano wa Kampeni aliohutubia kwenye Kata ya Milola, mkoani Lindi, Oktoba24, 2020

Wananchi wa Jimbo la Mchinga wakishangilia Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Kassim Majaliwa wakati alipohutubia mkutano wa kampeni kwenye Kata ya MIlola kumuombea kura mgombea Urais wa CCM, Dkt. John Pombe Magufuli, Mgombea Ubunge wa Jimbo la Mchinga kwa tiketi ya CCM, Mama Salma Kikwete kwenye Kata ya Milola mkoani Lindi, Oktoba 24, 2020.

Mke wa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Mama Mary Majaliwa akimuombea kura mgombea Urais wa CCM, Rais Dkt. John Pombe Magufuli,  mgombea ubunge wa CCM katika Jimbo la Mchinga Mama Salma Kikwete (katikati) pamoja na Madiwani wa CCM katika mkutano wa kampeni  uliohutubiwa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM, Kassim Majaliwa kwenye Kata ya Milola katika Jimbo hilo, Oktoba 24, 2020.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Kassim Majaliwa  akizungumza na mgombea Ubunge wa Jimbo la Mchinga kwa tiketi ya CCM, Mama Salma Kikwete katika mkutano wa kampeni aliouhutubia kwenye Kata ya Milola katika Jimbo hilo mkoani Lindi, Oktoba 24, 2020.

 

****************************************

*Amnadi Mama Salma Kikwete, madiwani Margareth na Casmiry

MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa amewataka wakazi wa jimbo la Mchinga wawachague viongozi wanaotoka chama makini cha CCM.

Ametoa kauli hiyo leo (Jumamosi, Oktoba 24, 2020) wakati akizungumza na wakazi wa kata za Milola na Rutamba, Manispaa ya Lindi kwenye mkutano uliofanyika Milola kumuombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. John Pombe Magufuli.

“Leteni mtu ambaye anatoka kwenye chama makini. Mkipata mtu wa CCM atakuja mwenyewe Bungeni apate kuwasemea masuala yenu. Msimlete mtu wa kusema HAPANA kwa kila jambo. Tunapata nao shida sana,” amesema.

Akiwa Milola, Mheshimiwa Majaliwa aliwanadi mgombea ubunge wa jimbo la Mchinga, Mama Salma Kikwete, mgombea udiwani wa kata ya Milola, Bibi Margareth Namahochi na akiwa njiani kuelekea Lindi mjini, alimnadi mgombea udiwani wa kata ya Rutamba, Bw. Casmiry Mbinga.

Mheshimiwa Majaliwa aliwataka wakazi hao wasichague viongozi kwa presha na ushabiki hata kama ni ndugu zao. “Leo tunahitaji viongozi wenye uwezo wa kwenda kukaa meza moja na wazee, watu wenye umri wa kati na vijana. Kwa hiyo, tarehe 28 Oktoba, ambayo ni Jumatano ijayo ninawasihi mwende mkawachague viongozi wa CCM. Mwende mkampigie kura nyingi Dkt. Magufuli kwa sababu mipango yake imo humu ndani,” alisema huku akionesha Ilani ya CCM ya 2020-2025.

Aliwataka wakazi hao wamchague Dkt. Magufuli na waache michanganyo ya zamani kwani imewanyima maendeleo kwa kipindi kirefu. “Hebu tufanye tuone fursa ambayo Rais ametupa, tuache michanganyo, imetunyima maendeleo kwa muda mrefu.”

Naye Mama Salma Kikwete akiomba kura kwa wakazi hao, alisema hakuna Serikali ambayo imewahi kushindwa kuongoza hivyo akawaomba wampe kura ili aweze kutekeleza vipaumbele tisa ambavyo ameviandaa kwa maendeleo ya jimbo hilo.

“Chagueni viongozi wa CCM ambao tunazungumza lugha moja. Tunataka tushirikiane kuhimiza vipaumbele vya wananchi ambavyo ni afya, elimu, miundombinu, maji, nishati, kilimo, uvuvi, ufugaji na michezo.”

Naye, mbunge mteule wa jimbo la Mtama, Bw. Nape Nnauye alipopewa nafasi kumuombea kura Dkt. Magufuli aliwataka wakazi hao waache ushabiki wa kisiasa na wajifunze kutoka nchi jirani ambayo wananchi wake walipata maafa baada ya uchaguzi na wagombea wakabakia na makundi.

Naye aliyekuwa mbunge wa viti maalum wa CUF kisha akahamia CCM, Bibi Riziki Lulida aliwaonya wakazi hao waache ushabiki wa kisiasa kwa sababu hauna manufaa kwa jimbo la Mchinga na yeye ameyaona madhara ya upande wa pili.

“Mimi ni shuhuda wa mambo ya upande wa pili. Nilirudi CCM kwa mapenzi yangu. Nilikengeuka lakini sasa nimerudi nyumbani. Nataka niwaambie, mkifanya makosa ya ushabiki, mtajutia kupoteza kura zenu.”

“Tarehe 28 ikifika, wanawake wote twende tukampigie kura Mama Salma Kikwete ili idadi ya wanawake iongezeke ndani ya Bunge. Mkimpa kura mgombea mwanaume mtakuwa mmejiabisha ninyi wenyewe.”

Aliwasihi waichague CCM kwa sababu ina sera zinazoeleweka. “Wale wengine wanatuletea sera za ushoga? Chagueni CCM hao wengine wanataka tuangamie sababu dini zote zinakataa ushoga. Tusiwachague hao, la sivyo tutaangamia kwa kuruhusu sodoma na gomora,” alisisitiza.

No comments: