DC Kanoni apiga marufuku sherehe,kongamano siku mbili kabla ya uchaguzi
Na Amiri Kilagalila,Njombe
Wananchi wilayani Wanging'ombe mkoani Njombe wameagizwa kutofanya sherehe au kongomano lolote siku mbili kabla ya uchaguzi ili siku hizo wazitumie kufanya maandalizi ya uchaguzi mkuu utakaofanyika hivi karibuni.
Agizo hilo limetolewa na mkuu wa wilaya ya Wanging'ombe Lauter Kanoni wakati wa kufunga kikao cha kamati ya amani ya wilaya hiyo kilichofanyika jana na kushirikisha wadau mbalimbali wakiwemo viongozi wa madhehebu ya dini.
Aliagiza hayo baada ya kufuatia mkuu wa wilaya hiyo wiki iliyopita kufanya mkutano katika kijiji kimoja kwa ajili ya kujadili masuala ya msingi akitarajia zaidi ya wananchi miambili watashiriki kwenye mkutano huo lakini waliojitokeza walikuwa kumi tu.
Alitoa maelekezo kwa viongozi wa madhehebu ya dini, watendaji wa kata na vijiji na maafisa tarafa ili siku mbili hizo wananchi watumie kujipanga na kwenda kupiga kura kuchagua viongozi watakaowaongoza katika kipindi cha miaka mitano.
"Nimetoa maelekezo tarehe 27 na 28 hakuna harusi, kongamano wala sherehe itakayofanyika ndani ya wilaya hii nataka wananchi wafanye maandalizi ya kupiga kura" Alisema Kanoni.
Aliwaomba viongozi hao kuwaasa vijana kupima na kuchagua viongozi watakaofaa na kuepuka uchochezi, vurugu zisizo za lazima na ahadi nyingine ambazo hazitekelezeki.
Afisa uchaguzi wilaya ya Wanging'ombe Christopher Masaka alisema tayari mawakala wa vyama vya siasa kwenye wilaya hiyo wameshaapishwa ambapo zoezi hilo lilianza juzi tarehe 21 na litakamilika tarehe 23 mwezi huu.
Aliwasisitiza wananchi kuondoka maeneo ya kupigia kura mara baada ya kumaliza zoezi hilo kwani kuendelea kubaki wakati wameshapiga kura tafsiri yake ni uvunjifu wa amani.
"Viongozi wa madhehebu ya dini wanapokuwa maeneo yao wawasisitize waumini kushika na kuelewa yale yaliyojadiliwa kwenye mkutano huu"
Nae mrakibu msaidizi wa jeshi la polisi nchini Malimi Ndulu alisema hali ya usalama kuanzia ngazi ya wilaya hadi taifa ipo vizuri hivyo aliwatoa hofu wananchi waendelee na shughuli zao na wajitokeze kwa wingi siku ya uchaguzi ili wakachague viongozi wanaowataka.
" Ukisikiliza katika nchi yetu kuna viashiria vya ugaidi kuna baadhi ya watu wanakuja kututembelea na tunawakaribisha lakini kumbe siyo wema na baadhi ya nyumba za ibada zinatumika vibaya" Alisema Malimi.
No comments: