MAFUNZO YATOLEWAYO VETA NI NGUZO MUHIMU KATIKA UJENZI WA TAIFA LA VIWANDA
Na Leandra Gabriel, Michuzi TV
MAMLAKA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imeeleza kuwa mafunzo ya ufundi stadi ni nguzo muhimu kwa uchumi wa viwanda kwa kuwa mafundi stadi ndio waendeshaji wa moja kwa moja wa viwanda na shughuli mbalimbali za uzalishaji.
Akizungumza na wanachama wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Dar es Salaam (DCPC,) Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo Dkt. Pancras Buluju amesema kuwa VETA imekuwa ikitoa mafundi mahiri na wenye tija wa uzalishaji bidhaa za viwandani.
"Mafundi wanaotoka hapa wanakuwa wameiva vilivyo na wenye uwezo wa kuanzisha viwanda vidogo na vya Kati na kuweza kujiajiri na kuajiri wengine, hii ni nguzo kubwa ya ujenzi wa Taifa la viwanda pia Serikali kunufaika na mapato zaidi yatokanayo na kodi na mauzo." Amesema Buluju.
Amesema kuwa elimu ya mafunzo stadi yamekuwa na umuhimu mkubwa hasa katika kutoa suluhisho la changamoto ya ajira pamoja na kukuza uchumi wa Jamii na kupunguza umaskini.
"Ufundi Stadi ni mkombozi mkubwa katika kukabiliana matatizo la ajira kwani ujuzi na ufundi stadi unampa mhitimu fursa ya kuajiriwa na kujiajiri pia VETA imejikita katika kutoa mafunzo kwa vikundi mbalimbali vya vijana na akina mama kwa lengo la kuinua uchumi na kuiendeleza jamii." Ameeleza.
Aidha amesema kuwa Mamlaka hiyo imeendeleza juhudi za upatikanaji wa elimu na mafunzo ya ufundi stadi na hiyo ni pamoja na lengo la Serikali la kufikia mwaka 2025 kila Wilaya na Mkoa nchini kuwa na Chuo cha ufundi stadi cha VETA.
"Malengo yetu ni kuwafikia wananchi kote nchini na Serikali katika mwaka wa fedha 2019/2020 Serikali ilitenga zaidi ya shilingi bilioni 48 kwa ajili ya kujenga vyuo vipya 29 katika Wilaya mbalimbali na tayari ujenzi unaendelea katika hatua mbalimbali." Amesema.
Pia amesema kuwa Mamlaka hiyo imeendelea na ujenzi wa vyuo vipya na kukarabati vyuo vilivyopo ili kila mtanzania mwenye uhitaji wa mafunzo ya ufundi stadi aweze kuyapata kwa urahisi katika eneo alilopo na wanataraji kuongeza udahili kutoka wanafunzi Laki saba hadi milioni moja kwa mwaka.
Dkt. Pancras amewashukuru waandishi wa habari kwa kuendelea kuhabarisha umma kuhusu elimu, fursa na Mafunzo yanayotolewa na Mamlaka hayo.
No comments: