JITIHADA ZA JPM KATIKA UJENZI WA TAIFA LA VIWANDA ZAZIDI KUUNGWA MKONO
Mkurugenzi wa Taasisi ya Furahika Education College David Msuya, akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na programu za mafunzo ya ufundi zitakazotolewa bure na taasisi hiyo, amesema mpango huo ni katika kuunga mkono jitahada za Rais Dkt. John Magufuli katika ujenzi wa Taifa la viwanda, leo jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya vijana wakiwa katika mafunzo yanayotolewa bure na Taasisi na Furahika Education College iliyopo Buguruni Malapa jijini Dar es Salaam.
Na Leandra Gabriel, Michuzi TV
TAASISI ya Furahika Education College iliyopo Buguruni Malapa jijini Dar es Salaam, Imeunga mkono jitihada za Rais Dkt.John Joseph Magufuli za kujenga Tanzania ya viwanda kwa kutoa bure mafunzo ya ufundi ili kuzalisha wataalamu wengi watakaosimamia na kuendesha viwanda pamoja na kutoa ajira kwa watanzania wengi zaidi.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam Mkurugenzi wa Taasisi ya Furahika Education College David Msuya amesema kuwa jitihada za Rais Magufuli zikiungwa mkono uchumi na ujenzi wa Taifa la viwanda utafikiwa kwa kiwango cha juu na bora zaidi na hiyo ni pamoja na kuzalisha wataalamu watakaosimamia miradi mbalimbali ya kimaendeleo.
"Taasisi hii imesajiliwa na VETA na tumeanzisha programu ya kutoa mafunzo ya ufundi ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono jitihada za Rais Magufuli ambaye amekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha ujenzi Taifa lenye uchumi imara unaochagizwa na viwanda nchini...Tukiwa na wataalamu wa kutosha na viwanda ajira nyingi zitapatikana." ameeleza Msuya.
Msuya amesema kuwa, kozi za ufundi zitatolewa kwa vijana waliomaliza darasa la saba hadi kidato cha nne bila malipo yoyote isipokuwa rasilimali zitakazotumika katika mafunzo.
"Mafunzo haya yanatolewa bila ada, wazazi wawalete vijana wao watakachochagia ni rasilimali zitakazotumika wakati wa utoaji wa mafunzo hivyo wazazi na walezi ni vyema wakawaleta vijana wao wapate mafunzo haya." Amesema.
Amesema kuwa kozi hizo zitatolewa kuanzia Oktoba 19 mwaka huu zikiwa pamoja na ufundi Cherehani, Useremala, Ujenzi, ufundi wa Magari, Mafunzo ya Hoteli, Kompyuta, Mapambo na urembo pamoja na Muziki.
"Tunatambua vijana wana ndoto mbalimbali, kupitia kozi zitakazotolea tunaamini watafikia malengo yao, tuna walimu wa kutosha, studio na vifaa vya kufundishia na kwa wahitimu wa kozi ya Cherehani watapewa bure mashine ili wakaanzie mashine." Ameeleza.
Vilevile amesema kuwa Taasisi hiyo inatoa bure huduma za ushonaji wa sare za shule kwa watoto yatima na kupitia mafunzo hayo vijana waliotoka katika mazingira magumu na walemavu watapewa vipaumbele zaidi.
No comments: