CHAMA CHA NLD CHAMGEUZIA KIBAO MAKAMU MWENYEKITI WAKE ALIYEMPIGIA DEBE MAALIM SEIF, KUMHOJI KAMATI KUU
Na Said Mwishehe, Michuzi TV
CHAMA cha Siasa nchini cha Tanzania National League for Democracy (NLD) kimepinga kauli ya Makamo Mwenyekiti wa chama hicho upande wa Zanzibar Hamadi Hemedi ambaye aliyedai Chama hicho kitamuunga mkono mgombea wa urais Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha ACT Wazalendo Maalim Seif Sharifu Hamadi katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 28,2020.
Akizungumza mbele ya waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Katibu Mkuu wa Chama hicho Tanzania Bara Tozy Matwanga, amesema Makamu huyo mwenyekiti amekiuka utaratibu ,hivyo wanatarajia kumuita kwenye kika cha Kamati Kuu kwa ajili ya kumpa nafasi ya kujieleza.
"Kamati Kuu ya NLD watakaa kikao kwa ajili ya kumpa nafasi Hemedi ili aweze kujieleza kwa sababu gani ametangaza kumuunga mkono Maalim Seif bila kuwashirikisha uongozi wa chama hicho.
"Msimamo wa Chama chetu kwa upande wa Zanzibar tunaye mgombea urais Mfalme Hamisi Hassan na ndio tunamuunga mkono na kuhakikisha anashinda uchaguzi mkuu mwaka huu,"amesema na kuongeza NLD hawana mpango wa kushirikiana na vyama vyengine kama ilivyokuwa katika uchaguzi wa mwaka 2015.
Amesema kwasababu hawaoni faida zaidi ya kuwanufaisha baadhi ya watu huku akibainisha kwa sasa Mwenyekiti wa Chama cha NLD ni Taifa ni Mfalme Hamisi Hassan na si Oscar Makaidi kama ilivyokuwa inafahamika na watu wengine.
Kuhusu mwenendo wa kampeni za uchaguzi mkuu,Matwanga amesema kuna baadhi ya wagombea wanatoa lugha zinazoashiria uvunjifu wa amani,hivyo amewaomba wananchi kuwa nakini kuhakikisha uchaguzi unakuwa wa amani na salama.
Ameongeza kwamba hakuna sababu ya kuwasikiliza wanaohubiri uvunjifu wa amani na kusisitiza ni jukumu la watanzania wote kuwapuuza wanaohubiri uvunjifu wa amani."Watanzania tujiepushe na wanasiasa wanaotumia lugha za uchochozi katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu."
Kuhusu mgombea urais wa CCM Dk.John.Magufuli, amesema NLD inaheshimu sheria za Uchaguzi Mkuu, hivyo hawawezi kutoa kauli ya kusema wanamuunga mkono.mgombea urais wa Chama kingine lakini anachoweza kueleza wanampongeza Dk.Magufuli kwa kazi kubwa ambayo anefanya ya kuleta maendeleo pamoja na ujenzi wa miundombinu ya barabara.
"Tunafahamu hakuna mahali tunataka kusifu au kupongeza kazi ambazo Rais Magufuli amefanya,hivyo tunampongeza kwa kuboresha miundombinu na ukweli miundombinu ya barabara ni muhimu kwa maendeleo ya kiuchumi,"amesema Matwanga.
Katibu Mkuu wa Chama cha NLD Tanzania Bara Tozy Matwanga akifafanua jambo
No comments: