WATANZANIA WAASWA KUSAMEHE


Na Mwandishi wetu, Mirerani 

WATANZANIA wametakiwa kusamehe ili waweze kupata amani mioyoni mwao kwa kujiepusha na magonjwa na kuwa karibu na Mungu katika maisha yao ya kila siku. 

Wito huo umetolewa leo Septemba 13 Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara na Padri Elias Kimaro wa Kanisa Katoliki Parokia ya Bikira Maria Mama wa Rozali Takatifu kwenye Dominika ya 24 ya mwaka A wa Kanisa. 

Padri Kimaro amesema msamaha ni tiba ya moyo hivyo watanzania wanapaswa kutoa msamaha kwa wote waliowakosea ili waanze ukurasa mpya wa maisha mioyoni mwao. 

Amesema msamaha huleta amani, umoja na utulivu kwani vita na vurugu hutokea kwa sababu ya jambo dogo kushindwa kusameheana na kuanza maisha upya. 

Amesema wanapaswa kujifunza kusamehe kwani msamaha ni tiba ya moyo kuliko kubeba mizigo ya kukumbuka makosa ya zamani ambayo huwezi kuyarekebisha zaidi ya kusamehe. 

"Unakuta mtu amekukosea anaishi kwa furaha, lakini wewe badala ya kusamehe unabeba moyoni na kupata ugonjwa wa moyo, kisukari kisha unakufa kwa kuweka vitu kifuani," amesema Padri Kimaro. 

Amesema Mungu ni mwema anawasamehe binadamu pindi wanapokosea hivyo binadamu nao wanapaswa kusamehe bila kuhesabu ni mara ngapi amefanya msamaha. 

"Neno la Injili ya leo kwenye kitabu cha Mathayo 18:21 linatufundisha namna Yesu alivyotufundisha kusamehe saba mara sabini nasi tusamehe wakosaji wetu kama Mungu anavyo tusamehe," amesema Padri Kimaro. 

Amesema tangu mtu azaliwe, awe kijana hadi kuwa mzee amefanya dhambi nyingi lakini Mungu amesamehe kwani nini binadamu asimsamehe mwenzake. 

"Msamaha una hatua nyingi ikiwemo ya kwanza, ya pili na kuendelea hivyo kwa kuanzia anza kujisamehe wewe mwenyewe kwa makosa uliyoyafanya kipindi kilichopita na kuanza upya," amesema Padri Kimaro.
Padri Elias Kimaro wa Kanisa Katoliki Parokia ya Bikira Maria Mama wa Rozali Takatifu ya Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, akiongoza sala ndani ya ukuta unaozunguka migodi ya madini ya Tanzanite hivi karibuni.

No comments: