DEMOKRASIA, UWAZI NDANI YA CHAMA KARATA YA TURUFU KWA CCM KUELEKEA KATIKA UCHAGUZI MKUU WA OKTOBA 28
Na Said Mwishehe,Michuzi TV-Geita
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) hivi karibuni kilifanya tathmini ya sku 10 za awali tangu kianze kampeni za urais, ubunge na udiwani. ambapo hali inaonekana ni shwari kwa upande wao.
Pengine watu wanaweza kudhani wanajikosha, au wanatafuta namna ya kucheza na saikolojia za watu, lakini ukweli utabaki kuwa CCM bado ni chama imara na kikubwa barani Afrika.
Binafsi si mgeni katika kampeni za urais, niliwahi kushiriki kampeni mbalimbali za ngazi ya udiwani, ubunge na hata urais huko nyuma.
Nilichokishuhudia mwaka huu wa Uchaguzi Mkuu 2020 kuna mambo makubwa yanafanyika kimya kimya. Chama kipo imara sana chini ya Mwenyekiti wake Dk.John Magufuli kuliko wakati mwingine wowote kinyume na matarajio ya wengi.
Nadhani watu wanakumbuka habari za wajumbe, watia nia wa ubunge na udiwani walivyokatwakatwa hata kwa wale ambao walipata kura nyingi kwenye chaguzi za ndani.
Watu walidhani kutakuwa na ombwe ndani ya Chama, kutakuwa na chuki zisizo na msingi kutokana na baadhi ya wabunge wakongwe kushindwa kurejea bungeni.
Nilichokishuhudia kwenye kampeni hizi, ambapo hadi sasa tumeshapita majimbo zaidi ya 20 katika mikoa minane, hakuna hata mgombea ubunge ambaye jina lake halijarejea lakini akashindwa kuzungumza maneno ya hekima.
Mathalani, tulipofika mkoani Simiyu Wilaya ya Bariadi, tulikutana na Mtemi Chenge, maneno aliyoyazungumza yaliwagusa wengi kinyume na maneno yaliyokuwa yakisambaa kwenye mitandao ya kijamii kuwa Chenge hakufurahishwa na kilichotokea.
Akizungumza mbele ya Mgombea urais na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi( CCM) Dk.John Magufuli baada ya kufika jimbo la Bariadi mkoani Simiyu ,Chenge alianza kwa kumshukuru Dk.Magufuli kwa heshma ambayo amempatia kusimamia mbele ya wananchi.
Hata hivyo Chenge anasema kwa mwaka 2005 alipata bahati ya kuteuliwa na Chama chake kugombea ubunge jimbo la Bariadi ambalo lilikuwa chini ya upinzani,akafanikiwa kuligomboa.
"Ni kuhakikishe kwamba wembe ule ule kura zitakuwa za kutosha, nataka nimhakikishie mgombea wetu wa ubunge jimbo la Bariadi kijana wetu Endrew Kundo anashinda kwa kishindo na tunashinda kwa nafasi ya urais, tunajua kata saba tumepita bila kupingwa lakini tutakwenda kote huko kuhakikisha unashinda.
"Rais Magufuli wewe umeitendea haki Bariadi, umeitendea haki Simiyu, umeitendea haki Tanzania bila Katiba wewe ungekuwa unasubiri kuapishwa tu kwa ajli ya miaka mingine mitano, alisema Chenge.
Hata hivyo kwa Dk.Magufuli alitumia nafasi hiyo kumzungumzia Chenge huku akitumia nafasi hiyo kukumbusha historia ya mwaka 1995 kati yake yeye na Chenge.Pia alisema wabunge waliokuwepo katika majimbo ya mkoa huo akiwemo Chenge wamefanya kazi zao vizuri lakini katika siasa huwa kuna vipindi.
"Change huyu mimi ni kaka yangu.Hata hivyo katika siasa kuna awamu, kuna awamu ya Mzee Al Hassan Mwinyi,Benjamin Mkapa ,mzee Jakaya Kikwete na sasa ni awamu yake.Kwahiyo nataka kusema zamu ya ubunge hivi sasa ni mhandisi Mkundo , mtemi Chenge kazi ziko nyingi sana na ndugu zangu wa Bariadi na Simiyu maneno yanayopitishwa na wapinzani achacheni nayo,"amesema.
Ukweli maelezo ya Chenge mbele ya Dk.Magufuli na ufafanuzi wa Dk.Magufuli kwa Chenge umenifundisha mambo mawili makubwa.Mosi ni demokrasia ambavyo imetawala katika Chama hicho kufanya maamuzi yake na kufanya mambo yake.Pili ni uwazi na ukweli ambao Dk.Magufuli amekuwa nao katika kukiongoza Chama hicho.
Kimsingi, hoja yangu inasimamia hapa; Chama kipo imara zaidi katika upande wa demokrasia. kikubwa kilichofanyika hadi kuwalainisha nafsi zao si jambo dogo. Ni kitu kikubwa kilichohitaji nguvu ya ziada na maneno ya busara kweli kweli, ambayo mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dk. Magufuli anayo.
Katika kampeni zake za urais nimemsikia Dk.Magufuli si zaidi ya mara moja akisema kazi zipo nyingi, kuna idara zinahitaji wakurugenzi na kuna mashirika yanahitaji wenyeviti wa bodi na wajumbe na kama hiyo haitoshi kuna wilaya nyingi zinahitaji watu wa kuziongoza na mikoa ya kimkakati inayohitaji watu imara wa kuyasimamia.
Mwaka huu CCM chini ya Dk.Magufuli imekuwa makini katika kuchambua,kuchuja na kujadili wagombea wake wanaowania nafasi za uongozi.Hata hivyo nikumbushe tu kabla ya kuanza chaguzi za ndani watia nia walikumbushwa kuwa kupata kura nyingi si ushindi bali Chama ndicho chenye maamuzi juu ya nani anafaa kuwa mpeperusha bendera.
Hakuna uonevu wala rushwa katika hilo bali Chama kinahitaji kuwa na mtu imara ambaye akisimama atakuwa na sababu nyingi za kukifanya chama kishinde.
Nikiri pamoja na mambo mengine yanayoendelea ya kuomba kura, kutoa ahadi, kueleza utekelezaji wa Ilani iliyomalizika na kuna Ilani ya Uchaguzi Mkuu , binafsi niliamua kufanya tathmini kuhusu watiania ambao majina yao yaliondolewa aidha wakati wa kura za maoni au kuondolewa na Kamati Kuu.
Ukweli nimebaini uwepo wa demokrasia, nimebaini uimara wa CCM,nimebaini umoja na mshikamano kwa Wana CCM,nimebaini jinsi ambavyo Dk.Magufuli na viongozi waliopo chini walivyokuwa makini kuhakikisha Chama kinabakia imara.Ndio nimebaini namna ambavyo wagombea ubunge ambao majina yao yameondolewa wasivyokuwa na kinyongo.
Wameridhika, wameungana na sasa wanasonga mbele.Kila ambako Dk.Magufuli amepita kuomba kura na kuwanadi wagombea wote katika majimbo ambayo amepita wanafuraha.CCM imeonesha demokrasia ya hali ya juu.Huko nyuma baada ya kufanyika michakato ya kura za maoni tulikuwa tukishuhudia jinsi ambavyo yalikuwa yakiiibuka makundi miongoni mwa wana CCM.
Makundi hayo yalisababisha kuidhoofisha CCM wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu.Hata upinzani walikuwa wanasubiria kuona nani amepitishwa na Chama hicho na nani ameachwa.Kwa mwaka huu hali imekuwa tofauti, ukomavu wa demokrasia chini ya Mwenyekiti wao Dk.Magufuli .Hakuna makundi,hakuna mpasuko na wala hakuna malumbano.
Akiwa jimbo la Buchosa,Dk.Magufuli aliweka wazi sabababu za kupitishwa jina la Erick Shigongo kugombea ubunge katika jimbo.Kwa kukumbusha tu Dk.Charles Tizeba ndio alikuwa Mbunge wa Buchosa lakini baada ya mchakatato wa ndani ya Chama jina lake halijapata nafasi ya kupitishwa.
"Mnafahamu wakati wa mchakato wa kura za maoni ndani ya CCM kulikuwa na makundi na ni kawaida, mnaweza kumfuata mwanamke hata wanaume watano lakini atakeyeoa ni mmoja, na ndio maana kwenye mchakato wa jimbo la Buchosa ulikuwa mchakato mzuri , wa demokrasia kama Chama kinavyopanga.
"Wagombea ubunge wakafungana, kura zikalingana , kura zikishalingana ni jukumu la viongozi wa juu kuamua.Kura ambazo alipata Tizeba ndio hizo hizo alizopata Shigongo.Hivyo Kamati Kuu uamuzi ukaja katika hao wagombea nani kajipigia kura?Ni mjumbe wa halmashauri kuu ambaye ni Tizeba , kwa hiyo tukatoa kura yake moja , nataka kueleza ukweli, sitaki kuwaficha, tulipoitoa Tizeba akawa wa pili.Leo tunaye hapa na anamuombea kura Shigongo.
Dk.Magufuli akawaambia wananchi wa Buchosa kuwa Tizeba amefanya kazi yake, na anakumbuka alimpeleka kwenye jimbo hilo kuweka jiwe la msingi."Kazi huwa ni kuachiana, kulikuwa na mzee Nyerere amefanya kazi yake akaondoka, akaja mzee Mwinyi,akaja mzee Mkapa, akaja mzee Kikwete akakaa miaka yake 10 akaondoka.
"Na mimi nimekuja na nina miaka mitano, ndio maana nawaomba nimalizie, Tiziba amefanya ubunge kwa miaka 10, sio kwamba hana maana, kazi serikalini ziko nyingi, lisitokee kundi hapa sijui la Tizeba, sijui la Shigongo wote hawa ni wa kwangu ni sawa na wote ni CCM,alisema Dk.Magufuli.
Maelezo ya Dk.Magufuli sio tu kwamba yanazungumzia kukomaa kwa demokrasia lakini ninachokiona jinsi ambavyo wana CCM wanapata majibu ya maswali yao ambayo huenda walikuwa wanajiuliza kwanini Tizeba ameachwa.
Hata hivyo kilichotokea kwa Tizeba kwa kura zake kufungana na Shigongo na kisha kubainika Tizeba alijipigia kura,ndicho ambacho kilitokea kwa Kangi Lugola katika jimbo la Mwibara.Lugola kura zake zilifungana na za Charles Kajege.
Kabla ya kutoa ufafanuzi kuhusu jina la Lugola kuondolewa Dk.Magufuli aliwaambia wananchi kwamba Kangi Lugola ni mwanafunzi wake kwani alimfundisha akiwa Sengerema sekondari."Akiwa shuleni alikuwa kiongozi mzuri, alikuwa analala kwenye bweni la Mirambo.
"Ukweli , watu Mwibara mheshimiwa Lugola na mwenzake walifungana kwenye kura , walifungana kura kwani yeye na Kajege walipata kura 173 , walipofungana tukahesabu nani mjumbe wa halmashauri kuu ya kamati ya siasa ya Wilaya tutakuta Kangi Lugola ni mjumbe kwa hiyo yeye amejipigia na ukitoa kura yake moja anakuwa ameshaondoka
"Ni utaratibu wa kawaida tu, yule mwingine sio mjumbe na huyu ni mjumbe amejipigia kura na ukiondoa ya Kangi Lugola anabaki na kura 172, nikasema huyu ni mtu mzuri namhafamu , na kazi ziko nyingi, wala hakubabaika, Lugola kula samaki wako vizuri. CCM iko, kwa hiyo ndugu zangu wa Mwibara nimeona niongee haya kwa uwazi."
Hakika kwa Dk.Magufuli amefanikiwa kuimarisha umoja na mshikamano,ameimarisha nidhamu ndani ya Chama, amewajenga wana CCM kukubali na kuamini katika kweli.Ndio katika kampeni za mwaka huu ,kazi imekuwa rahisi, waliopata nafasi na wasio wapata nafasi wote wanashirikiana kuomba kura za mgombea urais wa CCM, wameungana kuomba kura za madiwani, wameungana kuomba kura za madiwani.Hiyo ndio CCM inayoongozwa na Dk.Magufuli, kiongozi hodari.
Akiwa jimbo la Busanda, Dk.Magufuli katika ile ile dhana ya kusema ukweli alipata nafasi ya kuelezea sababu za jina la Kulwa Biteko kutopitishwa licha ya kuwa aliongoza kura za maoni.Jina ambalo lilipitishwa kugombea ubunge ni Mhandisi Tumain Magesa.
"Mhandisi Magesa alikuwa Mkuu wa Wilaya Kiteto kule Manyara, nafahamu michakato ya kwenye Chama chetu, lakini maamuzi ni ya Kamati Kuu na NEC, sisi ndio tunachambua vizuri.Katika michakato yoyote fainali inatolewa na Kamati Kuu, mgombea aliyeongoza hapa alikuwa Kulwa Biteko na pacha wake yuko hapa, ambaye ni Waziri wangu wa Madini na anafanya kazi nzuri sana.
"Tukafanya uchambuzi ukifika Bukombe unaliza mbunge wa hapa ni nani unaambiwa Dotto Biteko, ukifika hapa Busanda unaambiwa ni Kulwa Biteko hiyo hapana, maana yake itafika mahali mbunge wa chato, nani nani Magufuli, ukienda Geita unakuta mbunge wa hapa ni nani nani Magufuli.
"Lakini pili tulichojadili, ukiwa mbunge lazima utoke mahali ulopozaliwa, sana kama Kulwa alizaliwa hapa, Biteko hawezi kuzaliwa sehemu nyingine, mapacha wanazaliwa sehemu moja, kama hawa ni mapacha haiwezekani wazaliwe sehemu tofauti, mmoja azaliwe Bukombe na mwingine Busanda, kwa hiyo Kulwa sio kwamba ana makosa," amefafanua.
Dk.Magufuli ameongeza Kulwa Biteko anafanya kazi Wizara ya Mambo ya Nje, yeye ni mhasibu kule Msumbiji, ndio mshika fedha wake."Tukasema hizi kazi lazima tuwagawe pacha wake aendelee kuwa Mbunge , na Kulwa andelee kukaa Msumbiji anisaidie kukusanya fedha za mambo ya nje."
Hata hivyo nafasi ya pili katika mchakato wa kura za maoni katika jimbo hilo alikuwa ni Lolencia Bukwimba ambaye alikuwa Mbunge wa jimbo hilo kwa miaka 12, na katika kampeni zake za kwanza Dk.Magufulii alimfanyia kampeni lakini safari hii alizidiwa kura katika mchakato wa kura za ndani ya Chama hicho.Hivyo Kamati Kuu iliamua kupitisha jina la Magesa aliyekuwa ameshika nafasi ya tatu.
Hii ndiyo CCM ambayo mwenyekiti wake Dk. Magufuli aliota kuiona tangu siku ya kwanza alipokabidhiwa kiti hicho na mwenyekiti mstaafu Jakaya Kikwete. Kampeni zinakuwa na umoja zaidi kutokana na maridhiano yaliyokuwepo.
No comments: