WAGANGA WA KIENYEJI WAFUNGWA JELA MIAKA MIWILI KWA RUSHWA

Na Mwandishi wetu, Babati 

WAGANGA wawili wa kienyeji Luhanga Mabeshi na Hamis Gambona wamehukumiwa kwenda jela miaka miwili na Mahakama ya Hakimu mkazi wa Babati kwa kosa la kuomba rushwa ya shilingi 500,000 na kupokea shilingi 200,000 kutoka kwa mganga wa jadi. 

Hata hivyo, mshtakiwa wa kwanza Mabeshi hakuwepo mahakamani hapo baada ya kuruka dhamana ila anaendelea kutafutwa huku mshtakiwa wa pili Gambona akipelekwa gereza la mkoa wa Manyara, Mrara ili akatumikie adhabu hiyo. 

Hakimu mfawidhi wa mahakama ya wilaya ya Babati Simon Kebello ametoa adhabu hiyo jana kwenye kesi hiyo namba CC 2019 baada ya kuridhishwa na ushahidi usiotia shaka uliotolewa na mwendesha mashtaka wa TAKUKURU Evelyine Onditi. 

Awali, washtakiwa hao walifikishwa mahakamani kwa kosa la kuomba na kupokea rushwa kwa mganga wa jadi wakidai kuwa wao ni wapelelezi kutoka umoja wa waganga za jadi na tiba asili Tanzania (Uwawata). 

Wakadai kuwa kwa vyeo vyao wanakagua waganga wanaopiga ramli chonganishi hivyo naye anahusika katika hilo awape rushwa ya shilingi 500,000 ili wasimchukulie hatua kwa kosa hilo. 

Amesema kwa sababu mganga huyo hakuwa anajihusisha na ramli chonganishi alitoa taarifa TAKUKURU na kisha kukamatwa kwa washtakiwa hao waliopokea rushwa ya shilingi 200,000 na wakafikishwa mahakamani na kuhukumiwa baada ya kutiwa hatiani. 

Mkuu wa TAKUKURU Mkoani Manyara Holle Joseph Makungu akizungumza na waandishi wa habari mjini Babati ametoa rai kwa wananchi kutoa taarifa kwao pindi wakimuona Mabeshi ili afikishwe gerezani akatumikie adhabu yake. 

Makungu amesema Mabeshi hupendelea kutembelea maeneo ya Wilaya ya Karatu Mkoani Arusha na Mkoa wa Shinyanga. 



No comments: